KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 17, 2011

Rage: Lazima tuiue TP Mazembe


WAKATI kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na timu ya TP Mazembe, uongozi wa klabu hiyo umetaja mbinu watakazozitumia kuwaua wapinzani wao. Katika makala hii ya ana kwa ana,iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage anaelezea kuhusu mbinu hizo.

SWALI: Hongera kwa ushindi mnaoendelea kuupata katika michuano ya ligi kuu msimu huu. Nini siri ya mafanikio hayo?
JIBU: Siri ya mafanikio hayo ni juhudi zinazofanywa kwa pamoja na kila mmoja wetu na pia kutimiza malengo tuliyopangiana. Kuanzia wachezaji, makocha na viongozi sote tupo pamoja na tumekuwa tukifanyakazi kwa ushirikiano mkubwa.
Mbali na hayo, bado tuna imani kuwa tutaweza kufanya vizuri zaidi kwa vile wachezaji wetu wote wana ari ya kuhakikisha wanajenga heshima ya klabu yetu kwa mara ya pili mfululizo.
Ukweli ni kwamba ushindi wetu unaweza kuchangiwa na mshikamano uliopo kati ya wanachama, viongozi pamoja na mashabiki, ambao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi uwanjani na kuwashangilia kwa nguvu wachezaji kitu, ambacho kimeongeza juhudi ya ushindi.
SWALI: Hivi karibuni ulisikika ukieleza kwamba mtaunda kamati ya kuhakikisha mnaivua ubingwa TP Mazembe. Je, kazi hiyo tayari mmeifanya? Ni kina nani wanaounda kamati hiyo?
JIBU: Simba ni klabu kubwa, imefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunashinda mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe hapo Jumamosi.
Miongoni mwa mipango tuliyofanya ni pamoja na kuwepo baadhi ya watu ambao wameunda kamati ya kusaka ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Afrika.
Lakini nasikitika kwamba siwezi kukutajia majina ya wajumbe wanaounda kamati hiyo kwa vile wameomba wasitajwe hadharani.Lakini kamati hiyo ipo na inaendelea na kazi na tayari imeweza kufanya mambo makubwa, ikiwa ni pamoja na kupata siri za ushindi wa wapinzani wetu hasa wanapokuwa nyumbani kwao Congo.
Miongoni mwa siri hizo ni pamoja na kuifahamu kwa undani timu hiyo wakiwemo wachezaji wao wapya, ambao wanacheza ligi kuu ya nchini humo na mfumo wao wa uchezaji.
SWALI: Ukiacha kamati hiyo kunasa siri za ushindi wa TP Mazembe huko kwao, je mmepata CD au kanda za video za michezo mbalimbali ya timu hiyo ya Congo?
JIBU: Ni kweli tumeweza kupata baadhi ya CD za michezo ya TP Mazembe na benchi letu la ufundi pamoja na wachezaji wamefanyia kazi kujua mbinu za kuweza kuwasambaratisha na kwa kweli tunaondoka Ijumaa kwenda Congo tukiwa tumechukua tahadhari zote.
Miongoni mwa tahadhari hizo ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa ubalozi wetu kule Congo ili kukwepa hujuma zozote za nje na ndani ya uwanja na pia kwenye makazi yetu, ambayo tutafikia ambako tayari tumetuma watu wetu kuweka mazingira sawa.
Pia tumeweza kuwatumia baadhi ya Watanzania, ambao wanaishi Congo kwa ajili ya kujua mambo mengi ya TP Mazembe. Kwa kweli tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaweka rekodi ya kuivua ubingwa timu hiyo kama tulivyofanya kwa Zamalek.
SWALI: Mnatarajia kwenda Congo kwa usafiri gani na siku ipi?
JIBU: Tumepanga kuondoka nchini siku ya Ijumaa kwenda Congo na taratibu zote za kukodi ndege maalumu zinaendelea. Pia wanachama wetu wanaendelea kujiandikisha majina yao pale makao makuu ya klabu, mtaa wa Msimbazi.
Wapo baadhi ya viongozi wa serikali na wabunge, ambao wameonyesha nia ya kutaka kuongozana na sisi kwenda Congo ili kuwapa hamasa vijana wetu waweze kushinda mchezo huo.
Napenda kukuhakikishia kwamba tumepanga kuweka rekodi huko Congo, lazima tuwashangaze watu, hasa wale ambao wanatuponda na kutuombea mabaya.
SWALI: Watu gani ambao wanawaombea mabaya wakati nyinyi ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa? Au ni Yanga?
JIBU: Wapo watu wachache ambao wanataka sisi tutolewe katika mashindano haya, lakini tutakwenda na kupambana na hao TP Mazembe hadi hatua ya mwisho.
Siwezi kusema ni watu gani hao,lakini kwenye soka mambo hayo yapo na watafunga mdomo wenyewe baada ya kusikia habari za huko Congo.
SWALI: Unaweza kutupatia majina ya wachezaji, ambao mmepanga kwenda nao huko Congo?
JIBU: Sina orodha ya wachezaji ambao watakwenda Congo kwa vile kazi hiyo inafanywa na viongozi wa benchi la ufundi, lakini nategemea kuipata Jumatano au Alhamisi.
Hata hivyo,baadhi ya wachezaji ambao ni wagonjwa kama Uhuru Suleiman,Joseph Owino wao nina hakika hawawezi kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
SWALI:Je tokea mmeanza maandalizi ya mchezo dhidi ya TP Mazembe mnapata ushirikiano kutoka Shirikisho la soka nchini (TFF) na Serikalini?
JIBU:Hakika napenda kuwashukuru viongozi wa Serikali,TFF kwa vile tupo nao bega kwa bega kuhakikisha Simba inapeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano hayo ukumbuke sisi ndio wawakilishi pekee tulio bakia katika michuano ya kimataifa.
Tumeona wenzetu Yanga wametolewa katika mzunguko wa kwanza,Zanizbar Ocean View na KMKM zote zimetoka,nawaomba mashabiki wote wa soka nchini kuiombea dua Simba.

No comments:

Post a Comment