KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 4, 2011

Simba, Yanga nani zaidi kesho?


Na Rashid Zahor
HAYAWI hayawi yamekuwa. Baada ya subira na majigambo ya muda mrefu, hatimaye miamba miwili ya soka nchini, Simba na Yanga leo inakutana katika mechi ya ligi kuu ya Vodacom, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo linalogusa hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, linatarajiwa kuwa kali na gumu kwa vile kila timu imepania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Yanga iliichapa Simba bao 1-0.

Je, Yanga itaendeleza ubabe wake kwa Simba ama vijana hao wa Msimbazi watalipiza kisasi kwa wenzao wa Jangwani?

Swali hilo na mengineyo kadhaa ndiyo yaliyotawala hisia za mashabiki wa klabu hizo mbili, ambao baadhi yao huangua kilio, kupatwa na huzuni au hata kushindwa kula kila timu yao inapofungwa.

Hadi sasa, Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 17, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37 kutokana na michezo 16. Azam ni ya tatu kwa kuwa na pointi 36 katika mechi 18 ilizocheza.

Simba itaingia uwanjani ikitokea mafichoni Zanzibar, ilikokwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo wakati Yanga itatokea kambini Bagamoyo mkoani Pwani.

Mechi hiyo itakuwa mtihani wa kwanza kwa Kocha Sam Timbe wa Yanga, aliyeanza kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini ni ya kawaida kwa Kocha Patrick Phiri wa Simba, ambaye ameshazoea mikikimikiki ya timu hizo mbili.

Timbe alikaririwa juzi akisema kuwa, amemkabidhi jukumu la kuiongoza timu hiyo, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’, ambaye amerejea kwenye kiwango chake cha kawaida baada ya kusimamishwa kwa miezi kadhaa na kocha wa zamani, Kostadin Papic.

Kocha huyo kutoka Uganda alisema, timu yake itawakabili wapinzani wao, ikiwa haina hofu kwa kuwa wanatambua vyema umuhimu wa mechi hiyo na wamejiandaa kwa kila hali kuibuka na ushindi.

Hata hivyo, Timbe alisema timu yake itamkosa kiungo mchezeshaji, Ernest Boakye kutokana na kuwa majeruhi. Alisema mchezaji huyo anasumbuliwa na maumivu ya goti la kushoto.

Kwa upande wa Simba, itawakosa kiungo Hillary Echessa na beki John Owino kutokana na kuwa majerehu. Pia itamkosa kiungo Mohamed Banka, aliyetimuliwa kambini kwa makosa ya utovu wa nidhamu. Lakini itakuwa na faraja kubwa baada ya mshambuliaji wake nyota, Emmanuel Okwi kupona maumivu ya kifundo cha mguu na kurejea uwanjani.

Ushindani mkali katika mechi ya leo unatarajiwa kuwa kwa washambuliaji, Jerry Tegete, Davis Mwape wa Yanga, Mbwana Samatta na Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba, ambao kila mmoja amepania kufunga mabao.

Pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam, ambaye anatambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA). Atasaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Maxmillian Mkongolo wa Rukwa. Mwamuzi wa akiba atakuwa Army Sentimea wa Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 30,000 kwa jukwaa la VIP A, sh. 20,000 jukwaa la VIP B, sh. 10,000 jukwaa la VIP C, sh. 7,000 na sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa na bluu na sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya kijani mzunguko.

Timu zinatarajiwa kupangwa hivi:

Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi, Ibrahim Job, Nsa Job, Kigi Makasi, Davis Mwape, Jerry Tegete.

Simba: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Jerry Santo, Rashid Gumbo, Mbwana Samatta, Patrick Ochan, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Nico Nyagawa.

Msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom hadi sasa ni kama ifuatavyo:

P W D L GF GA Pts
Yanga 17 11 5 1 23 4 38
Simba SC 16 12 1 3 31 14 37
Azam 18 11 3 4 33 12 36
Mtibwa Sugar 18 8 6 4 18 17 30
Kagera Sugar 18 8 5 5 18 15 29
JKT Ruvu 18 6 7 5 17 16 25
Toto African 18 5 5 8 16 21 20
African Lyon 18 4 7 7 14 23 19
Polisi Dodoma 18 4 5 9 8 16 17
Ruvu Shooting 17 3 6 8 12 19 15
Maji Maji 18 2 6 10 10 19 12
AFC 18 3 2 13 12 36 11

No comments:

Post a Comment