KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, March 22, 2011

Majina ya wasanii wa Five Stars waliofariki

Na Latifa Ganzel Morogoro

WASANII 13 wa kundi la Muziki la Five Star’s Modern Taarab wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa kati yake mmoja vibaya baada ya gari yao aina ya Toyota Coaster waliyokuwa wakisafiria kutoka Mbeya, kuelekea jijini Dar es salaam kuacha njia na kulivaa lori lililokuwa limesimama na kupinduka, wakikwepa kukutana uso kwa uso na lori lililokuwa likija mbele.
Ajali hiyo iliyothibitishwa na Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro Ibrahim Mwamakula, zilibainisha ajali hiyo kutokea Machi 21, majira ya saa 2.30 usiku, ndani ya eneo la hifadhi ya taifa ya Mikumi, kilometa karibu sita kutoka lango kuu la kuingilia hifadhi hiyo kutoka upande wa Doma.
Mwamakula alisema kuwa watu 12 walikufa papo hapo na mwingine mmoja alifia njia wakati akipelekwa hospitali ambapo kati yao kumi ni wanaume na watatu wanawake.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni Mwendo kasi wa gari hiyo aina ya Costa iliyokuwa imewabeba wasanii ,yenye namba za usajili T 351 BGE iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Hassan anayedaiwa kutoroka baada ya ajali, na uzembe wa dereva huyo kujaribu kulipita gari jingine bila kuwa na uangalifu.
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya Costa hiyo kujaribu kulipita lori aina ya scania lililokuwa limebeba mbao lililokuwa limesimama barabarani baada ya kuharibika lenye namba za usajili T848 APE na tela namba T 556 BDL mali ya Meshack Rajab Mvamba, na kukutana mbele yake na lori aina ya scania lenye namba T 182 BKB na tela namba T 530 BHY ambalo katika kuikwepa Costa hiyo na lenyewe lilipinduka
Kwa upande wake Rais wa bendi hiyo Ally Juma (25) maarufu kama “Ally J” ambaye ni miongoni mwa majeruhi walionusurika,alisema gari hiyo ilikuwa na watu 24 wakiwemo wasanii 21, madereva wawili na abiria mmoja, na walikuwa wakitokea Mkoani Mbeya kwenye maonesho ambapo Jumapili walifanya wilayani Kyela mkoani humo na kabla, siku ya Ijumaa walifanya maonesho Makambako, Mikumi siku ya alhamisi na Kilosa Mkoani Morogoro siku ya jumatano.
Miongoni mwa waliopoteza maisha yumo mwanamuziki Issa Kijoti na kiongozi wa bendi hiyo Nassoro Madenge , waimbaji wa bendi hiyo Husna Mapande na Hamisa Omary ambaye ni mke wa msanii Mussa Mipango, mpiga solo Shebe Juma, mpiga gitaa la base Omary Hashim, mbeba vyombo Omary maarufu kama Tolu,Mfanyakazi wa bendi hiyo Ngereza Hassan, wapiga kinanda Tizzo Mgunda na Hamma Kinyoya, mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Maimuna na mcheza shoo wa kundi la “Kitu Tigo” la Ilala ambaye jina lake halijaweza kujulikana mara moja na hao wote walikufa papo hapo katika eneo la ajali.
Mwingine aliyekufa akipelekwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu ni Haji Mzaniwa (32) mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye ni mbeba vyombo katika bendi hiyo.
Majeruhi katika ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro ni pamoja na mwimbaji Mkongwe na mgeni aliyekuwa amefanya onesho moja tu katika bendi hiyo, Mwanahawa Ally (55), Suzana Benedict (32),Zena Mohamed (27), Samila Rajab (22), Ally Juma (25), Rajab Kondo (25), Mwanahawa Hamis (38), Shaban Hamis (41) na Msafiri Mussa (22) wote wasanii na wakazi wa jijini Dar es salaam.
Hata hivyo baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo,Mohamed Hawanga ambaye ni mtumishi wa Hifadhi ya Mikumi, Justine Simon aliyekuwa safarini kuelekea Mafinga na Jatemi Lembilinyi aliyekuwa akielekea Iringa wakitokea Dar es salaam, walisema kama sio jitihada za dereva wa lori lililokuwa likija mbele kukwepesha gari hiyo na kuipeleka porini, huenda angekutana na Costa hiyo uso kwa uso, na watu wote wangeweza kupoteza maisha katika tukio hilo.
Maiti zote pamoja na majeruhi walipelekwa usiku wa manene katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwajili ya kuhifadhiwa huku majeruhi wakipatiwa matibabu.
Ndugu na jamaa wa marehemu hao walifurika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya mkoa wa morogoro kwaajili ya kuzitambua maiti zao na kuchukua kwaajili ya mazishi.

No comments:

Post a Comment