KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 10, 2011

BASATA kuboresha tuzo za muziki za Kili

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) linatarajia kuzipa taswira mpya tuzo za muziki za Tanzania, kuanzia zile zitakazofanyika mwaka 2012.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema mjini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii kuwa, tayari bodi ya baraza hilo imeshapitisha uamuzi wa kuboresha tuzo hizo.
Materego alisema hayo wakati wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye ukumbi za baraza hilo uliopo Ilala Sharrifu Shamba mjini Dar es Salaam.
Alisema lengo la uamuzi huo ni kuzifanya tuzo hizo ziwe na mvuto, ubora na kuwa maarufu katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki kutokana na jinsi zitakavyoandaliwa na kufanyika.
“Baraza kila mara limekuwa likifanyiakazi mapendekezo na michango ya wadau, hivyo kuanzia tuzo za muziki za mwaka 2012, kutakuwa na marekebisho makubwa yatakayoshirikisha wadau wengi na lengo kuu ni kuzipa taswira mpya na kuzifanya zizidi kuwa na ubora,” alisisitiza.
Materego alisema wamekuwa wakizifanyia maboresho tuzo hizo kila mwaka, lakini baadhi ya wadau wamekuwa wakizilalamikia kwa madai kuwa, hazijakidhi ubora na hadhi inayotakiwa.
Alitoa mwito kwa wadau kujikita kwenye kutoa changamoto za kujenga, lakini huku wakielewa kwamba, tuzo hizo hazina muda mrefu kiasi cha kuweza kumaliza changamoto zote zilizopo.
“BASATA iko wazi muda wote kupokea changamoto na michango ya wadau, ndiyo maana kwenye mpango mkakati wa Baraza wa mwaka 2011-2014, tumebeba kwa kiwango kikubwa ushauri uliopatikana kwenye jukwaa hili la sanaa,” alisema Materego.
Awali, msanii Witness anayepiga muziki wa miondoko ya hip hop aliwasilisha mada kuhusu uzoefu wake kwenye tuzo mbalimbali za muziki barani Afrika.
Katika mada yake hiyo, Witness alieleza kukerwa kwake na tabia ya vyombo vya habari na kumbi za burudani nchini kupiga nyimbo za nje kwa kiwango kikubwa pasipo kuzipa nafasi zile za nyumbani.
“Ukienda Afrika Kusini radio na kumbi zao za burudani hupiga kwa asilimia kubwa muziki wao na hiki ndicho kinaufanya muziki na wanamuziki wa nchi hiyo kuvuma na kutambulika dunia nzima. Hapa kwetu ni tofauti, utakumbana na miziki ya akina 50 Cent na Ja Rule, kuna haja ya hili kusimamiwa kikamilifu,” alisema.

No comments:

Post a Comment