KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 30, 2011

Dede achomoza na vibao viwili vipya


MWIMBAJI nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Shaabani Dede ameibuka na vibao viwili vipya, vitakavyojumuishwa kwenye albamu mpya ya bendi hiyo. Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Dede alivitaja vibao hivyo kuwa ni ‘Vita dhidi ya dawa za kulevya’ na ‘Suluhu’. Dede alisema vibao hivyo ni zawadi aliyowaandalia mashabiki wa Msondo Ngoma baada ya kurejea kwenye bendi hiyo wiki mbili zilizopita. Mwimbaji huyo mkongwe alirejea Msondo Ngoma akitokea bendi ya Mlimani Park Orchestra, ambayo alidumu nayo kwa zaidi ya miaka 20. Wakati huo huo, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti amesema wameamua kuiimarisha zaidi bendi hiyo kwa kumsaka mpuliza saxaphone mpya. Kibiriti alisema tangu Shabani Lendi alipoamua kurejea kwenye bendi yake ya zamani ya Mlimani Park, wamekuwa wakipiga nyimbo zao bila kutumia ala hiyo. Alisema kwa sasa wamepanga kufanya maonyesho ya kumtambulisha Dede mikoani ili kuwadhihirishia mashabiki wao kwamba bendi hiyo bado ipo imara. Kibiriti alisema tayari wameshafanya ziara mkoani Tanga na mwishoni mwa wiki hii watatembelea Ikwiriri mkoani Pwani. “Kama nilivyosema awali, lengo letu kubwa ni kumtambulisha Dede pamoja na vibao vyetu vipya, vilivyomo kwenye albamu yetu mpya, tutakayoizindua baadaye mwaka huu,”alisema.

No comments:

Post a Comment