KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 25, 2011

KWA NINI WAIMBAJI WA KIKE BONGO HAWADUMU?

LUIZA Mbutu
NYOTA Kinguti

LADY JayDee


Janet Isinike

Amina Remy


Amina Ngaluma

MUZIKI wa dansi una historia ndefu hapa nchini. Ulianza kupigwa tangu miaka ya 1950, lakini idadi kubwa ya wanamuziki katika miaka hiyo ilikuwa ni wanaume. Ni wanawake wachache sana waliojitokeza katika fani hiyo wakati huo.
Mabadiliko yalianza kujitokeza mwanzoni mwa miaka ya 1980, ambapo walijitokeza waimbaji wengi wa kike, ambao waliongezea ladha na utamu wa muziki, hasa kutokana na sauti zao maridhawa na miondoko yao stejini.
Kujitokeza kwao kuliwafanya mashabiki wengi wa muziki waanze kuamini kwamba, mambo yangeanza kuwa murua kwenye kumbi za burudani. Hiyo ilitokana na ukweli kwamba, sauti za waimbaji wa kike ni kachumbari tosha katika muziki wa aina yoyote.
Huenda pia waliamini hivyo kutokana na ukweli kwamba kwa miaka kadhaa iliyopita, kabla ya miaka hiyo ya 1980, muziki huo, hasa kwenye uimbaji, ulikuwa umetawaliwa zaidi na wanaume, hata kama nafasi ya uimbaji ilipendeza zaidi kuwakilishwa na mwanamke.
Ni kuanzia hapo ndipo walipoanza kujitokeza baadhi ya waimbaji wa kike waliong’ara na kujipatia sifa na umaarufu katika kila pembe ya Tanzania. Miongoni mwao alikuwepo Tabia Mwanjelwa, aliyeng’ara katika bendi ya Maquiz Original.
Waimbaji wengine wa kike waliojitokeza wakati huo ni pamoja na Nana Njige, aliyekuwa bendi ya Magereza, Rukia Mtama, aliyekuwa akimiliki bendi ya Ram Choc, Emma Mkelo, aliyekuwa bendi ya Super Rainbow na Kida Waziri , aliyekuwa Vijana Jazz.
Vilevile walikuwepo Nyota Kinguti, aliyekuwa Bicco Stars na sasa yupo The Kilimanjaro, Betty Enock, ambaye alipotelea Arabuni na Titty Shang, ambaye aling’ara kwa muda mfupi katika bendi ya Lulu Orchestra.
Pamoja na kujitokeza kwa waimbaji wengi wa kike, matarajio waliyokuwa nayo mashabiki wa muziki wa dansi yalianza kufifia kutokana na baadhi yao kushindwa kudumu muda mrefu katika bendi walizokuwa wakiimbia na wakati mwingine kushindwa kuimba katika hali ya kuvutia.
Baadhi yao baada ya kung’ara kwa kipindi kifupi, walitoweka wasijulikane mahali walipo. Na kwa wale walioendelea na muziki, walishindwa kung’ara na kufikia viwango vya waimbaji wenzao waliong’ara barani Afrika kama vile Mbilia Bel, Tshala Muana, Yvonne Chakachaka na wengineo.
Katika nyimbo nyingi za muziki wa dansi zilizoimbwa na waimbaji wa kike, baadhi yao walishindwa kuimba kwa sauti kike hasa. Sauti zao zilikuwa hazina utamu na mvuto wowote masikioni mwa mashabiki.
Zipo sababu nyingi zilizowafanya waimbaji hao wa kike kushindwa kudumu katika bendi zao kwa muda mrefu ama kutokuwa na maendeleo ya kuridhisha. Na mara nyingi walikuwa wakizua sokomoko kubwa katika bendi zao kiasi cha kuzifanya baadhi kudiriki kutamka bayana kwamba hazihitaji tena wanamuziki wa kike.
Dosari moja kubwa, ambayo ilionekana kujitokeza sana kwa waimbaji wa kike ni kujihusisha zaidi kimapenzi na wanamuziki wenzao, hasa viongozi. Tabia hiyo ilikuwa ikizua matukio mengi, si kwa waimbaji wa kike tu, bali hata wenzao wa kiume.
Mara nyingi iliwahi kutokea mwanamuziki wa kike alipojihusisha kimapenzi na kiongozi wa bendi, alijiona yupo matawi ya juu na kuwadharau wenzake. Aliweza kufanya anavyotaka, kutozingatia mazoezi na pia ilikuwa si ajabu kwake kufika mazoezini wakati anaotaka.
Hata hivyo, uzuri wa wanamuziki hao wa kike nao ulichangia kuwaponza, kwani mara nyingi ilipotokea baadhi yao kung’ara kimuziki, kila mwanaume alitaka kumtongoza. Awe mwanamuziki, mfanyabiashara au mtu wa kawaida, kila mmoja alitaka ampate kimapenzi.
Wakati mwingine, baadhi ya wanamuziki hao wa kike waliamua kuacha kabisa muziki na kuamua kuolewa pale ilipotokea mwanaume wake kumkataza kuendelea kujihusisha na fani hiyo. Matokeo yake ni kwamba wengi wa wanamuziki hao wa kike walikuwa hawadumu katika bendi zao.
Pamoja na hayo, sio siri kwamba waimbaji wengi wa kike wakati huo hawakuwa wakitilia maanani kazi ya muziki. Wengi walikuwa wakiuchukulia muziki kuwa ni kazi ya kihuni, hivyo mara nyingi kusababisha hata wao wenyewe wasijiheshimu.
Hali hiyo ilisababisha wanawake wengi wenye vipaji vya uimbaji kuhofikia kujitokeza hadharani ama kukatishwa tamaa kutokana na falsafa kwamba muziki ni uhuni.
Pengine ni vyema kwa wakati huu tulionao, wanamuziki wa kike waanze kubadilika kwa kuelewa wajibu wao katika suala zima linalohusu muziki. Wasiichukulie fani hiyo kuwa ni ya kihuni. Hizo dosari zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara juu yao inafaa ziepukwe.
Mwanamuziki pekee wa kike, ambaye hadi sasa anastahili kupongezwa kutokana na kudumu kwenye fani kwa miaka mingi ni Nyota Kinguti. Tangu alipoanza muziki akiwa Bicco Stars na sasa The Kilimanjaro, Nyota hajawahi kutetereka na uwezo wake kimuziki umekuwa ukiongezeka badala ya kushuka.
Waimbaji wengine wa kike, ambao angalau wamejitahidi kudumu kwenye fani hiyo kwa kipindi kirefu ni Luiza Mbutu, Khadija Mnoga na Janet Isinike wa Twanga Pepeta na Amina Ngaluma, ambaye kwa sasa yupo Arabuni na Judith Wambura ‘Lady JayDee’ anayemiliki bendi ya Machozi.
Wapo wanamuziki wengine wa kike wanaopiga muziki wa kizazi kipya, lakini hawapaswi kulinganishwa na wenzao wa dansi kwa vile muziki wao unatengenezwa zaidi kwa kutumia njia ya kompyuta. Hawapigi muziki wa dansi ambao ni laivu kwenye steji.
Ni vyema wanamuziki wa kike nchini kutambua kuwa, wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu na kutokata tamaa mapema kwani hakuna maendeleo ya ghafla na ya haraka.Wanapaswa kutilia maanani mazoezi na kujifunza mbinu za muziki zitakazowawezesha kutunga na kuimba kwa sauti tamu kama wanavyofanya wenzao wanaong’ara hapa Afrika.
Inafaa pia kwa wanamuziki wetu wa kike kuithamini kazi hiyo kwa kuiona kuwa sawa na zingine, tena isiyopaswa kuchezewa. Isiwe tu wanapotoka stejini, basi wanajiona na kazi ndio imekwisha.
Ni vyema pia kwa wanamuziki wetu wa kike kujiheshimu wakati wote. Iwapo watajiheshimu wawapo kwenye bendi zao, ni rahisi pia kwao kuheshimika kwa mashabiki.
Ieleweke kuwa, maendeleo ya wanamuziki wa kike na kung’ara kwao kimuziki, kutaamsha hamasa kwa wanawake wengi wenye vipaji kujitokeza, badala ya ilivyo hivi sasa, ambapo wengi wanasita kwa kuiona fani hiyo ni ya kihuni.

No comments:

Post a Comment