KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

MWANA FA: Maisha Ulaya si mepezi



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khamis Mwinjuma amesema maisha kwa waafrika katika nchi za Ulaya si mepesi au rahisi kama watu wengi wanavyofikiria.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Channel 5 hivi karibuni, Khamis, maarufu kwa jina la Mwana Falsafa alisema, binafsi hawezi kuishi mahali popote zaidi ya Tanzania.
Mwana FA alisema picha za video na za sinema zinazoonyesha mandhari ya miji ya Ulaya, ndizo
zinazowazuzua vijana wengi wa Afrika, lakini maisha ya huko kwao ni magumu.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mtangazaji wa kituo hicho, Jimmy Kabwe, aliyetaka kujua kwa nini hakuamua kuzamia na kuishi Ulaya kama wanavyofanya vijana wengi wa kiafrika.
Mwana FA alirejea nchini mwanzoni mwa mwezi huu akitokea Uingereza, ambako alikwenda kwa masomo mwaka jana katika Chuo cha Coventry.
Alisema aliamua kwenda kusoma Uingereza badala ya kuendelea na masomo yake Tanzania kwa
sababu alikuwa akitafuta elimu iliyo bora zaidi kutokana na kile alichodai kwamba mazingira ya
masomo nchini humo ni mazuri.
“Mimi ni mwoga sana wa maisha ya baadaye, hivyo nimeamua kuanza maandalizi mapema, ndo
sababu niliamua kuweka kando muziki kwa mwaka mmoja ili kujiendeleza kimasomo,”alisema.
Akiwa huko, msanii huyo mkali wa mashairi yanayogusa hisia alisema, hakuacha kujihusisha na muziki moja kwa moja na kwamba alikuwa akitunga nyimbo mpya kila mwezi.
“Ninazo nyimbo 23 mpya, ambazo bado sijazirekodi. Bado navuta subira, sina haraka ya kuingia
studio. Natarajia kuanza kuzirekodi hivi karibuni,” alisema.
Mwana FA alisema amepania kutoka kimuziki kivingine akiwa na nguvu mpya kwa lengo la kuwapa mashabiki wake ladha mpya.
“Nataka nikitoka, iwe kivingine. Watu waone kweli huyu mtu alikuwa mpya,”alisema.
Mwana FA alianza kujipatia umaarufu kimuziki nchini mwaka 2002 alipoibuka na singo yake ya
kwanza, inayojulikana kwa jina la ‘Ingekuwa vipi’. Kibao hicho kilishika nafasi za juu kwenye chati za vibao bora katika vituo mbalimbali vya radio nchini.
Alianza kujihusisha na muziki tangu mwaka 1993 alipokuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Mdote ya Muheza, Tanga kwa kushiriki kwenye maonyesho ya jukwaani.
Msanii huyo na kaka yake walihamishiwa Tanga mwaka 1990, ambako walihitimu masomo ya elimu ya msingi katika shule hiyo.
Akiwa kidato cha pili, Mwana FA aliunda kundi la Black Skin kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake, Robilus na Getheerics. Waliunda kundi hilo mwaka 1995 na lilidumu hadi mwaka 1997.
Mwana FA alishika nafasi ya tatu katika shindano la kumsaka mkali wa miondoko ya hip hop mkoani Tanga mwaka 1996. Alirejea Dar es Salaam mwaka 1998 na kujiunga na Taasisi ya Teknolojia (DIT), ambako alisoma kwa miezi minne.
Aliacha masomo katika chuo hicho na kujiunga na shule ya sekondari ya kiislamu ya Ununio kwa ajili masomo ya kidato cha tano na cha sita. Mara baada ya kumaliza masomo hayo mwaka 2000, ndipo alipojitosa zaidi katika fani ya muziki.
Alirekodi albamu yake ya kwanza mwaka 2002, inayojulikana kwa jina la ‘Mwanafalsafani’ kwa
udhamini wa studio ya Mawingu Records, iliyokuwa chini ya DJ Bonie Love.
Mwaka 2003, Mwana FA alinyakua tuzo ya msanii bora wa miondoko ya hip hop ya Kilimanjaro,
kufuatia kibao chake cha ‘Alikufa kwa ngoma’ kufanya vizuri.
Hadi sasa, Mwana FA amerekodi albamu tatu, ikiwemo ‘Unanitega’, ambayo ilishinda tuzo ya albamu bora ya hip hop katika tuzo za Kilimanjaro mwaka 2007.
Mwaka 2007, Mwana FA kwa kushirikiana na Ambwene Yesaya ‘AY’ walirekodi albamu ya pamoja inayojulikana kwa jina la ‘Habari ndio hiyo’. Mwaka jana, alishinda tuzo ya mtunzi bora wa nyimbo.

No comments:

Post a Comment