KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

New Manchester Band kumekucha




Dogo Hija na Amina Renny



Bawily Salum (kushoto) na Saidi Kosa
Wapiga magita Peter Kanuti na Saidi Ramadhani



Amina Renny


BENDI mpya ya muziki wa dansi ya New Manchester mwishoni mwa wiki iliyopita ilifanya utambulisho wa nyimbo zake katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) mkoani Pwani.
Katika onyesho hilo lililohudhuriwa na wanachuo wa TASUBA na baadhi ya wakazi wa mji huo, bendi hiyo, inayotumia miondoko ya 'Wana-Kamtekenya', ilitia fora kutokana na kuporomosha vibao vyake vitano vipya kwa umahiri mkubwa.
Licha ya wanamuziki wa bendi hiyo kutokuwa na umri mkubwa na maumbile yao kuonekana kuwa madogo, walionyesha ufundi wa hali ya juu katika kuimba na kupiga ala za muziki na kuwafanya mashabiki wengi wajimwage ukumbini kucheza.
Bendi hiyo, ambayo ilikuwepo kambini mjini Bagamoyo kwa wiki mbili, ililianza onyesho hilo kwakuporomosha kibao cha ‘Kijuba wa mtaa’, ambacho kilipambwa kwa sauti tamu za waimbaji Bawily Salum, Charles Patrick, Saidi Kosa, Yohana Zungufya na Amina Renny.
Mbali na sauti tamu za waimbaji hao, burudani nyingine murua ilikuwa upigaji wa gita la sololililokuwa likidonolewa na Peter Kanuti, ambaye kuna wakati alilipiga likiwa mgongoni.
Kanuti aliweza kulifanya gita hilo litoe mlio wa kusikitika, kubembeleza, kuliwaza, kuhamasisha nawakati mwingine kuamsha hisia.
Mpiga drums Riziki Salehe, maarufu kwa jina la Chocholii naye aliwaacha hoi mashabiki kutokana na kuzicharaza ngoma hizo kwa ufundi wa hali ya juu huku baadhi ya wakati zikisikika kama vile zilitaka kupasuka.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa pia kwa mpiga kinanda Ramadhani Koha, ambaye aliipapasa ala hiyo kwa mbwembwe nyingi na kuifanya itoe milio mbalimbali inayohamasisha kucheza.
Baada ya kibao hicho, bendi ya New Manchester iliporomosha kibao kingine kinachokwenda kwa jina la ‘Sina’ kabla ya kushusha kibao cha ‘Jakaya Kikwete’, ambacho kinaelezea mafanikio mbalimbali ya serikali ya awamu ya nne.
Mwanzoni, kibao hicho cha JK kilipigwa kwa miondoko ya ngoma za Lizombe ya Songea na Pigilia ya Lushoto kabla ya kukolezwa ala za miondoko tofauti.Kibao kilichofungakazi kilikuwa ‘Urithi wa baba’.
Kibao hicho kiliwafanya wanachuo wengi pamoja na mashabiki kujimwaga ukumbini kucheza huku wakiinyonganyonga miili yao kwa kufuatisha mipigo ya ala.
Rapa Papaa Kosa ndiye aliyekuwa kivutio kikubwa kutokana na umahiri wake wa kughani hukuakiwahamasisha mashabiki kucheza.
Baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho walishindwa kuvumilia na kujikuta wakijimwaga stejini kucheza sanjari na wanafunzi wao.
Wanamuziki wengine wa bendi hiyo walioshiriki kwenye onyesho hilo ni mpiga gita la besi SaidiRamadhani, mpiga gita la rhythm Juma Yegela na mpiga tumba, Selemani Hamad.
Akizungumza wakati wa onyesho hilo, rais wa bendi hiyo, John Mponda alisemawaliamua kuiweka kambini kwa wiki mbili mjini Bagamoyo ili iweze kupata mafunzo mazuri zaidi ya muziki.
Alisema onyesho hilo lililenga kuitambulisha bendi hiyo kwa vyombo vya habari na pia kwa wanachuo wa TASUBA ili waweze kuiona na kuitolea tathmini.
Mponda, ambaye pia ni mhadhiri wa taasisi hiyo alisema, bendi hiyo itazinduliwa rasmi keshokutwa katika onyesho litakalofanyika makao makuu yake, New Manchester Pub, Mbagala-Kilungule, Dar es Salaam.
Alisema yeye na ndugu zake wawili wameamua kuanzisha bendi hiyo kwa lengo la kuwapa ajirawanamuziki vijana na wanaochipukia na wenye vipaji ili waweze kujitegemea.
“Ninachoweza kusema ni kwamba sisi tumeianzisha tu hii bendi, lakini wamiliki ni wanamuzikiwenyewe,”alisema.
Mponda alisema wameanzisha bendi hiyo bila kuwashirikisha wanamuziki wengi wakongwe kwakuhofia usumbufu na kusisitiza kuwa, dhamira yao kubwa ni kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza.
Wanafunzi kadhaa wa TASUBA waliipongeza bendi hiyo kwa kusema kuwa, licha ya uchanga wake, imefanya mambo makubwa na yanayostahili kuwa mfano wa kuigwa.
Rais wa serikali ya wanachuo ya taasisi hiyo, Timothy Chelula alisema viongozi wa bendi hiyowalifanya vizuri kuiweka kambini Bagamoyo, ambako imepata mafunzo ya hali ya juu ya kimuziki.
Chelula alisema vitu vilivyofanywa na wanamuziki wa bendi hiyo wakati wa onyesho hilo ni uthibitisho wa wazi kwamba, itakuwa matawi ya juu na moto wa kuotea mbali.

No comments:

Post a Comment