KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

JK awapa somo wasanii wa Bongo

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wasanii nchini kujithamini wao na kazi zao ili waweze kunufaika.
“Kilio chenu nimekisikia siku nyingi juu ya kunyonywa kwa mapato ya kazi yenu, najua mnavuja jasho, lakini hamfaidiki na matunda yake, naahidi kuendelea kulishughulikia jambo hili,” amesema.
Rais Kikwete alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam wakati alipoungana na wasanii mbalimbali nchini katika tamasha la Zinduka, maalumu kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa malaria.
Aliwatoa hofu wasanii na kuwapongeza kwa jinsi walivyoweza kujipanga na kufanya jambo la msingi la kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo.
“Ningependa mjue kuwa, mimi nyimbo na kazi zenu zote nazifuatilia, nyimbo za bongo fleva mimi ni msikilizaji mzuri sana. Zamani mimi nilikuwa nacheza Sikinde, Saboso na Rhumba, kwa nyimbo za bongo fleva ya sasa, mnanikosha sana, nawapa hongera,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wasanii kujipanga na kutimiza malengo waliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na kuitumia vyema mitambo mipya na ya kisasa ya studio, aliyowaletea.
“Kilio chenu cha studio ya kisasa mlichokuwa mnakitoa muda mrefu nimewatimizieni, mshindwe
wenyewe. Na kwa suala la kuibiwa kazi zenu na kuwafanya kukosa mapato, naahidi kulitokomeza kabisa hilo kwa kuunda kikosi maalumu cha kushugulikia kero zote,” alisema.
Alisema wasanii wa filamu na muziki, ndiyo wanaoongoza kwa kudhulumiwa kazi zao na kuwataka wasubiri neema inayokuja baada ya uamuzi wake wa kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kazi za sanaa.
Alisema kikosi hicho kitakuwa chini ya wasanii wenyewe, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Hakimili (COSOTA), Jeshi la Polisi na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. Alisema lengo la kikosi hicho ni kuhakikisha kero hizo zinatoweka kabisa nchini.
Katika Tamasha hilo, wasanii wa muziki wa kizazi kipya, wakiwemo Profesa Jay, Banana Zorro, Joe Makini, Rehema Chalamika ‘Ray C’, Chegge na mwanamuziki mkongwe kutoka Zanzibar, Kidude binti Baraka ‘Bi. Kidude’ walishiriki kutoa burudani kwa mashabiki.
Wasanii na wanamuziki hao wanatarajiwa kuzunguka nchi nzima ili kutoa ujumbe na kugawa neti
katika kampeni hiyo, inayojulikana kwa jina la ‘Zinduka’.

No comments:

Post a Comment