KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

Bush aanza maisha ya uraiani



TEXAS, MAREKANI
UNAWEZA kuwa mpango wa kujilinda au kujipanga. Hata hivyo, uamuzi wa Rais wa zamani wa
Marekani, George W. Bush kutulia katika ranchi yake ya Texas, ilhali anayo makazi mazuri katikati ya jiji la Washington.
Hatua hiyo ya Bush kuamua kukaa nje ya jiji hilo lenye pilikapilika nyingi za kisiasa na kiuchumi,
inamfanya kuwa Rais pekee mstaafu kutumia muda wake mwingi kuwa ‘shambani’ kwake, akikagua na kusimamia shughuli za kilimo.
Ingawa kiongozi huyo anaweza kuwa na nia nzuri ya kushughulikia mambo yake binafsi, katika jimbo alikokulia, uamuzi wake umeibua hisia na mitazamo tofauti, miongoni mwa wadadisi wa mambo.
Baadhi ya watu wanadai mwanasiasa huyo ameamua kujichimbia Texas kwa lengo la kutaka kufunika madhambi aliyofanya wakati wa utawala wake, ikiwemo kutosimamia ipasavyo masuala ya mikopo na kusababisha mtikisiko wa uchumi duniani.
Shutuma dhidi ya Bush zimekuwa zinachapishwa katika vyombo mbalimbali duniani, na kutokana na hatua hiyo, anatajwa kuwa ndiye kiongozi aliyeondoka madarakani akiungwa mkono na asilimia chache zaidi ya wananchi.
Wakati anahitimisha utawala wake, Januari 19, mwaka jana, kiongozi huyo alikuwa akiungwa na
asilimia 21 ya wapigakura wa taifa hilo, ambapo asilimia 56 hawakutaka aongezwe muda (iwapo katiba ingekuwa inaruhusu) na asilimia 23 walipendekeza ashitakiwe akiwa uraiani.
Kura hizo ambazo ziliendeshwa na gazeti la New York Times zilionyesha jinsi Wamarekani
walivyochukizwa na utawala wake na hasa kujikita katika vita nchini Afghanistan na uvamizi aliuofanya Irak.
Utafiti wa gazeti hilo ulionyesha kuwa, chuki dhidi ya mwanasiasa huyo zilikuwa nyingi katika ofisi za umma na binafsi, ambapo nyingi ziliguswa katika mabadiliko yaliyovipa nguvu vikosi vya upelelezi kuzichunguza, kwa nia ya kuangalia uhusiano na taasisi za kigaidi duniani.
Pia zilionyesha tangu taifa hilo lilipopata uhuru wake, zaidi ya miaka 200 iliyopita, halikuwahi kujikuta katika mazingira magumu yaliyoambatana na uhasama kutoka nje.
“Aliongeza chachu ya uhasama na kusababisha Marekani iwe na maadui wengi wa kimataifa na humu ndani. Bush aliwafanya Wamarekani wa dini za Kikristo na Uislamu kutofurahia maisha na uhuru waliokuwa nao siku za nyuma, “ lilisema gazeti hilo.
Baadhi ya watu wanasema, usafi wa serikali yake aliuharibu alipoamua kuivamia Irak kijeshi, mwanzoni mwa 2003 na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na kuondoa kabisa utulivu uliokuwepo.
Wanamrushia lawama mwanasiasa huyo kutokana na mauaji ya raia wengi wakati wa harakati za
kuuteka mji mkuu wa Baghdad. Katika harakati hizo ambapo majeshi ya Marekani yalishirikiana na baadhi ya nchi za magharibi, yanadaiwa kuua zaidi ya watu 30,000.
Katika uvamizi huo uliochukua siku 19 hadi kutekwa kwa mji huo, majeshi hayo yaliharibu mali na majengo yanayokisiwa kuwa na thamani ya sh.trilioni 17, fedha ambazo kupatikana kwake
itawachukua miaka mitatu watu wa kawaida kuzipata.
“Bush anastahili kushitakiwa, uchunguzi dhidi yake ufanywe kwa uwazi na uhuhusishe taasisi huru za kimataifa. Naamini kwamba mwisho wa siku watagundua mambo mengi machafu yaliyofanywa na vikosi vya Marekani huko Irak, “anasema mchambuzi wa mambo ya kimataifa wa Marekani, Jones Gregory.
Ingawa gazeti la Washington Post linasema utawala wa Bush uliimarisha misingi iliyoachwa na Bill Clinton ya Ikulu ya nchi hiyo kuwa karibu na wananchi, wanaoushutumu wanamtaka mwanasiasa huyo kujitokeza kukiri makosa na kuomba radhi kwa makosa yaliyofanyika.
Gazeti hili linasema, kiongozi huyo mstaafu amefanya makosa kutoonekana mara kwa mara ilhali
anakabiliwa na shutuma nyingi zinazotaka ufafanuzi kujisafisha.
Tangu alipoondoka madarakani, Bush ameonekana hadharani chini ya mara 15, tofauti na watangulizi wake ambao katika kipindi cha mwaka mmoja waliendelea kuhudhuria makongamano, mikutano na kutoa mihadhara mingi.
Mathalani, ndani ya mwaka mmoja, Clinton alifanya mikutano 25 na waandishi wa habari, kutoa
mihadhara 47, kuhudhuria mikutano na makongamano 14 na kutoa misaada ya kibinadamu 53. Kazi hizo zote zilifanyika akiwepo.
“Rekodi hiyo ni ya juu zaidi kwa marais wastaafu, kwani hata baba yake (George Bush) alionekana hadharani mara 32. Lakini mwanawe (George W. Bush) imekuwa tofauti, kwa kuwa mwaka mzima kajichanganya na jamii mara 13, “linasema gazeti hilo.
Hata hivyo, kilicho wazi hadi sasa ni kuwa, umahiri wa Bush katika kujibu maswali ya waandishi wa habari na kujenga hoja katika mada mbalimbali kwa ajili ya kushawishi jamii, ni mkubwa kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kutawala taifa hilo.
Doa kubwa katika historia ya kiongozi huyo linatajwa kuwa lile la kutupiwa kiatu na mwandishi mmoja wa Irak, katika siku za mwisho mwisho za utawala wake. Tukio hilo linadaiwa kuwa baya zaidi katika historia ya viongozi wa Marekani, likifuatia matukio ya kuuawa yaliyowahi kuwakumba baadhi yao.
Wasaidizi wake wanasema, mwanasiasa huyo ameamua kutumia muda wake wa mwaka mmoja
kupumzika ili kujiandaa kwa harakati na changamoto nyingine za maisha.
Kazi kubwa anazozifanya ni kusoma vitabu (vingi vikiwa alivyozawadiwa madarakani) ambavyo alikosa muda wa kutosha kuvisoma. Pia anasimamia shughuli zake za kilimo na ufugaji katika ranchi yake.
“Muda si mrefu kiongozi huyo ataanza kuonekana hadharani na kufanya kazi nyingi za jamii alizopanga na atakazopangiwa kuzifanya. Kuwa madarakani kwa miaka minane na kukumbana na changamoto nyingi halikuwa jambo rahisi. Ndiyo maana aliamua kupumzika, “ anasema mmoja wa wasaidizi wake kwa sharti la kutotajwa jina.
Wiki mbili zilizopita, mwanasiasa huyo alijumuika na marais wa zamani katika Ikulu ya nchi hiyo
kupanga mikakati ya kuwasaidia wahanga wa Haiti, walioathiriwa na tetemeko la ardhi.

No comments:

Post a Comment