KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Usajili Yanga utatisha!

Papic akabidhi majina kwa Manji
Wachezaji wapya hadharani Juni
Watakaotemwa kupewa barua Mei 15
MFADHILI mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amekutana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic na kuzungumzia usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Manji na Papic wamekutana zaidi ya mara nne kuanzia Jumamosi iliyopita na jana walikuwa na kikao kizito cha kupanga mikakati ya usajili.
Mbali na kikao hicho kujadili masuala ya usajili, pia kililenga kumaliza tofauti zilizozuka kati yao na kusababisha Papic atishie kubwaga manyanga baada ya mkataba wake kumalizika.
Hali ya kutokuelewana kati ya Manji na Papic, ilizuka baada ya mfadhili huyo kumpigia simu kocha huyo kutoka Serbia na kumweleza kuwa, angeacha kumlipa mshahara kuanzia jana.
Manji alimweleza Papic kuhusu uamuzi wake huo siku moja kabla ya Yanga kumenyana na Simba katika mechi ya marudiano ya ligi kuu ya Vodacom na kupata kipigo cha mabao 4-3.
Kauli hiyo ya Manji ilimweka Papic kwenye wakati mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa, aliwaleta wachezaji wane kutoka nje kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, sambamba na msaidizi wake kutoka Serbia.
Kocha huyo msaidizi, Medic Momcilo ‘Moma’ alitua nchini wiki mbili zilizopita na jana alikutana na Manji kwenye ofisi za mfadhili huyo zilizopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumzia mkataba wake. Wachezaji walioletwa na Papic kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ni Issack Boakye, anayechezea timu ya New Aedubase United ya Ghana anacheza nafasi ya ulinzi na Kenneth Asamoah, anayechezea klabu ya FK Jagodina ya Serbia.
Wengine ni Sylivester Selaph Mokaine kutoka klabu ya Back Aces ya Afrika Kusini na Osai Boakye kutoka klabu ya Aduna ya Ghana. Tayari wachezaji hao wamesharejea kwao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Manji alikiri kukutana na Papic mara kadhaa na kuongeza kuwa, amemuagiza atumie kipindi cha likizo yake kusaka wachezaji wengine zaidi wenye vipaji.
Alipoulizwa iwapo ni kweli amemaliza tofauti zilizojitokeza kati yake na Papic, mfadhili huyo alisema kwa sasa hana tatizo na kocha huyo na wataendelea kufanyakazi pamoja kwa lengo la kuipatia mafanikio klabu hiyo. Tayari Manji ameshaingia mkataba na wachezaji wanne waliofanyiwa majaribio na Papic. Wachezaji hao waliondoka nchini jana na juzi kurejea kwao kwa ajili ya kushughulikia taratibuza uhamisho wa kimataifa kabla ya kurudi nchini Juni mwaka huu.
Kuna habari pia kuwa, baadhi ya wachezaji wa hapa nchini walioichezea Yanga msimu huu, wameshakutana na Manji na kutia saini mikataba mipya.
“Mchakato wa usajili Jangwani umeshaanza kwa tahadhari na siri kubwa. Manji amekutana na Papic na kuzungumza kwa kirefu kuhusu suala hilo na kimsingi amewakubali wachezaji wote waliopendekezwa na kocha huyo,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga.
Kuna habari kuwa, kipa Yaw Berko kutoka Ghana ametia saini mkataba mpya wa kuichezea Yanga kwa miaka miwili. Awali, Yaw alikuwa na mkataba na klabu hiyo wa miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment