KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

PHIRI AWAFUNIKA MAKOCHA WENZAKE LIGI KUU

KOSTADIN Papic
PATRICH Phiri

Na Fred Majaliwa
SAFARI ndefu ya kusakwa timu bingwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2009/2010 ilifika tamati jana, huku Simba ikitwaa kombe ikisaliwa na mechi mbili mkononi.
Mabingwa hao walikabidhiwa kombe hilo Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa shangwe nyingi baada ya kufanikiwa kuisambaratisha Yanga kwa mabao 4-3 katika mechi iliyokuwa ya kuelekea kukamilisha ratiba.
Timu zote zilimaliza mechi za ligi kuu jana kwa kushuka katika viwanja tofauti, lakini hadi kufika hatua hiyo kuna makocha walioonyesha kiwango kupitia timu zao na wengine walidorora na kujikuta wamefukuzwa.
PATRICK PHIRI


Ni kocha wa Simba aliyepata mafanikio yasiyo na mfano kutokana na kuipa ubingwa timu hiyo bila ya kupoteza mechi hata moja.


Simba hadi inatwaa kombe la Vodacom, ilishinda mechi 18 na kutoka sare mara mbili.Ilisaliwa na mechi mbili ambazo ni dhidi ya Yanga na Mtibwa iliyochezwa jana, na japokuwa Phiri katika michezo hiyo hakuwepo kutokana na kwenda kwao Zambia kuzungumza na Chama cha Soka cha huko (FAZ) kuhusu kukabidhiwa mikoba ya timu ya taifa ‘Chipolopolo’, pasipo pingamizi anastahili kuwa kocha bora.


Kuiongoza Simba kushinda mechi 11 za mzunguko wa kwanza bila ya kufungwa, kigezo kimojawapo cha kuleta ushawishi kocha huyo alambe tuzo hiyo, pia kutwaa ubingwa timu ikibakiwa na mechi mbili za kumaliza ligi, kunatosha kumfanya Phiri kuwa kocha bora.


Mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa timu hiyo amekuwa anaongoza kwa ufungaji mabao katika ligi kuu ya msimu huu akichuana na nyota wa Yanga Mrisho Ngasa na John Boko ‘Adebayor’ wa Azam, ni ushawishi mwingine wa kutazama mafanikio yake katika timu za ligi kuu.


Mgosi ana mabao 16, Ngasa na Adebayor wana magoli 14 kila mmoja. Pia Kaseja ndiye golikipa pekee aliyecheza mechi nyingi za Simba na kufungwa mabao machache. Ametunguliwa mara 12.Ingawa hayo ni mafanikio ya wachezaji binafsi, Phiri hawezi kuwekwa kando kwa kuwa ndiye kocha wa Simba aliyefundisha kikosi kizima ambacho kilitandaza soka ya uhakika uwanjani.


Ni wazi akiondoka kwenye timu hiyo ataacha pigo kubwa kwa sababu hata mashindano ya Kombe la Shirikisho wanayocheza Simba mwaka huu na kung’ara baada ya kuitoa Lengthens ya Zimbabwe katika raundi ya kwanza yamechangiwa na ufundi wake, ambapo alikuja msimu wa 2008/2009 timu ikiwa nafasi ya sita na aliikwamua hadi ya pili, nyuma ya Yanga.
KOSTADIN PAPIC


Inawezekana alikubalika haraka kwa wachezaji au walishika vyema mafunzo yake baada ya kikosi cha Yanga kuonyesha mabadiliko makubwa uwanjani katika muda mfupi kinyume ilivyotarajiwa na wengi.


Baada ya kukabidhiwa mikoba na Dusan Kondic aliyefukuzwa kutokana na kuvurunda baadhi ya mechi za mwanzoni mwa ligi kuu, mtihani wake wa kwanza ulikuwa katika mechi ngumu ya watani wa jadi, Simba na Yanga Oktoba 31 mwaka jana.


Licha ya kulazwa bao 1-0, wachezaji wote walisakata kandanda vizuri hali iliyoleta matumaini mapya kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ya Jangwani kuwa timu imeiva.Chini ya Kondic Yanga haikuwa na ‘jeuri’ ya kupiga migongeo hata sita mfululizo, wachezaji walikuwa wanakimbiza mpira na kutumia nguvu kubwa kusaka ushindi, lakini Papic alipofika alikataa uchezaji huo na kufundisha upigaji pasi ili kumiliki mpira na kufunga mabao ya malengo.


Mechi za mzunguko wa kwanza si kipimo sahihi cha kutosheleza kupima uwezo wake katika makocha walioongoza timu za ligi kuu msimu huu kutokana na kufika wakati timu ilikuwa chini Kondic na ilishaanza kupoteza mwelekeo mapema, lakini anastahili kupimwa raundi ya pili.


Katika hatua hiyo ameng’ara kwa kuigandisha Yanga katika nafasi ya pili iliyokuwa inawaniwa pia na Azam kwa nyakati tofauti. Katika mechi 10 za raundi ya pili, ameiongoza timu hiyo kushinda mechi 10 na kufungwa moja dhidi ya Simba.


Alimaliza jukumu lake jana kwa kucheza na Prisons Mbeya.Yanga kubadilishana na Simba katika mashindano ya kimataifa mwakani kwa maana yenyewe kucheza Kombe la Shirikisho na mabingwa hao kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo mwaka huu walicheza watoto wa Jangwani na kutolewa na Lupopo, bado kunamfanya asitoke kwenye orodha ya makocha waliofanya vizuri msimu huu, japokuwa alikuja wakati ligi imeshaanza kutimua vumbi.


Papic kama atakuwepo Yanga katika msimu ujao timu hiyo inaweza kufanya makubwa zaidi kwa kuwa atapata muda wa kutosha kusajili wachezaji anaowataka na kuwaondoa wasiokuwa na mchango kwa timu hiyo.


Mara nyingi kocha huyo amekuwa anasema nyota wa kulipwa kama Robert Mba, Kabongo Honore na Steven Bengo, Obren Circovic, Wisdom Ndhlovu na wengineo wasiokuwa na manufaa kwa timu waondoke. Kama uongozi utampa ushirikiano katika kufanya mabadiliko mbalimbali kwenye timu ana nafasi ya kufanya maajabu msimu ujao.
SALUM MAYANGA


Si vibaya kumuita kocha kijana aliyemudu kutoa upinzani katika ligi kuu ya msimu huu licha ya kushindwa kutimiza malengo aliyokusudia ya kutwaa ubingwa.


Akisaidiwa na aliyekuwa mlinzi wa kulia wa timu hiyo Mecky Maxime katika kuliongoza benchi la ufundi la Mtibwa baada ya mchezaji huyo kustaafu mwaka juzi, Mayanga amehimili purukushani za ligi hiyo hadi kushika nafasi ya tatu.


Mtibwa ya Turiani, Morogoro, katika mechi 21 ilizocheza imevuna pointi 33 baada ya kushinda mechi tisa, sare sita na kufungwa michezo ya idadi hiyo.


Kocha huyo kama ataachwa aendelee kushusha programu zake za kufundisha katika timu hiyo anaweza kuivika Mtibwa Sugar taji la Vodacom, lakini atafanikiwa hilo endapo atapewa ‘fuko’ la fedha za kutosha kufanya usajili wa nguvu.


Mayanga anakabiliwa na changamoto ya kusajili wachezaji wapya na wenye ari ya soka na kuwapumzisha baadhi ya wakongwe ambao hawaendani na kasi ya mchezo wa mpira wa miguu kwa sasa.


Zuberi Katwila na Moja Liseki ni miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa kukaa kando kupisha vijana wa kumsaidia kocha huyo kuwapa uhondo wa furaha wakata miwa wa Manungu, Mayanga aliyecheza mpira Mtibwa Sugar hadi kusomea ukocha akiwa hapo, akipewa nafasi atashangaza timu nyingi za ligi kuu na mashindano mengine.
ITAMAR AMORIN


Kocha mwingine wa kigeni aliyeonyesha akiwezeshwa anaweza kama alivyodhihirisha hivyo katika timu ya Azam FC, ambayo licha ya kupungua makali katika mzunguko wa pili ameifikisha nafasi ya nne msimu huu.


Azam ilimaliza ligi kwa kuchuana na Manyema Rangers jana, lakini kusua sua katika baadhi ya mechi za raundi ya pili hakutokani na wachezaji kucheza chini ya kiwango bali ugumu wa ligi hiyo, ambayo kila timu ilikuwa inakwepa kushuka daraja.


Kocha huyo aliiweka Yanga roho juu katika mbio ya nafasi ya pili kufuatia Azam kuing’ang’ania na kumaliza ligi wakiwa nyuma ya vinara Simba na Jangwani wakibaki nyuma ya lamba lamba hao.


Amorin alionyesha kila dalili kuwa ataipa Azam tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani, lakini kukwama katika baadhi ya mechi kwenye mzunguko wa pili kulimwangusha na kutoa mwanya kwa Yanga kuchukua nafasi hiyo kutokana na kurudi na kasi mpya ya kushinda kila mechi.


Ana wachezaji wazuri na kama timu hiyo itamaliza ligi ikiwa ya tatu au ya nne atapaswa kupongezwa kutokana na Azam kuwa na wachezaji mahiri na waliong’ara kwenye ligi hiyo kama John Boko aliyekuwa anachuana na kina Mgosi na Ngasa katika vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora msimu huu.


Mabao 14 aliyofunga Boko ni heshima kwa timu na kocha huyo na mbinu anazopewa mchezaji huyo mrefu na Amaron zimechangia awe mali hata machoni mwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo na kumuita katika baadhi ya mechi.


Timu yake ilikuwa inacheza mpira wa kuvutia uwanjani na kuzipa hofu timu vigogo za Simba na Yanga, ambapo kocha huyo kijana kama alivyo Mayanga msimu ujao akipewa nafasi ya kuongeza mabadiliko kikosini mwake, haitashangaza kuona Azam wanawalamba wapinzani wao katika kila mechi.


Tangu alipokabidhiwa timu hiyo msimu wa 2008/2009 alionyesha mabadiliko makubwa katika timu kutofautisha na Mbrazil mwenzake Neider dos Santos pamoja na msaidizi wake mzalendo Sylvester Marsh ambao walishindwa kuipa mafanikio timu hiyo kiasi cha kunusurika kushuka daraja.Bado ana nuru ya kuifikisha Azam kwenye kilele cha mafanikio kwa siku za usoni.
CHARLES KILINDA


Msimu huu wachezaji wake wameendelea kuchechemea kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza ambao JKT Ruvu walimaliza wakiwa nafasi ya sita, japokuwa kabla ya mechi ya jana dhidi ya African Lyon walikuwa wa tano katika msimamo.


Sifa na heshima ya timu hiyo imeporomoka katika msimu huu kufuatia kubebeshwa mabao mengi katika mechi tisa walizopoteza na kabla ya mechi ya mwisho ya jana, JKT ilikuwa imebamizwa jumla ya mabao 28 huku ikishinda 26.


Ladha ya soka ya maafande hao waliocheza vyema msimu wa 2008/2009 chini ya Kilinda msimu huu haikuonekana kabisa, lakini tatizo la majeruhi linaweza kuwa kikwazo kwa kocha huyo aliyewahi kucheza katika timu ya Yanga miaka ya nyuma.


Katika baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza Kilinda alisema majeruhi waliharibu malengo yake na katika mzunguko wa pili walikuwa nyanya zaidi kwa kupoteza mechi nyingi.Huenda mazoea ya kukaa miaka mingi na wachezaji bila ya kuwaondoa au kuongeza damu changa nyingine kama walivyofanya kwa Kazimoto, imechangia kikosi hicho kuyumba katika ligi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa.


Kilinda hajafanya vibaya sana kiasi cha kutajwa hafai isipokuwa anatakiwa kufanya mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa nia ya kuleta nguvu mpya, lakini itapendeza naye akitazama programu zake kwa nini hazikuzaa matunda kama ilivyokuwa msimu uliopita?
CHARLES MKWASA


Amefanya kazi nzuri ya kuinusuru African Lyon kushuka daraja baada ya kukabidhiwa timu ikiwa katika hali ngumu. Ilimaliza mechi za mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi saba na ilikuwa ya pili kutoka mkiani.


Mkwasa japokuwa kuna kipindi alikuwa na jukumu la kuinoa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, chini ya kocha msaidizi Seleman Matola timu hiyo iliendelea kusaka pointi za kuibakisha ligi huu na kufanikiwa katika hilo.


Kwa sasa ina pointi 24 ambazo zimewahakikishia kutoshuka daraja na kama Mkwasa atabaki au ataondoka kama mwenyewe alivyowahi kunukuliwa kuwa alisaini mkataba wa muda mfupi ambao utafika tamati baada ya ligi kumalizika, msimu ujao timu hiyo inatakiwa kufanya marekebisho kikosini.


Japokuwa uwepo wa kipa Ivo Mapunda aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo na kuwepo Vicent Barnabas, Meshack Abel na Anthony Matangalu waliotua kwa mkopo kutoka Simba na Yanga, kumeipa timu hiyo uhai katika mzunguko wa pili, suala la kupatikana kocha bora linapaswa kutazamwa kwa umakini.
MRAGE KABANGE


Sifa zake hazipishani na Mkwasa baada ya kukabidhiwa timu ya Kagera Sugar ikiwa taabani katika raundi ya kwanza, lakini alitumia ujuzi wake wote kuipa pointi na hatimaye kuiokoa kushuka daraja.


Wapenda soka wengi walitarajia Kagera ingeshuka kutokana na kupoteza mechi nyingi katika mzunguko wa kwanza na ilizinduka katika michezo ya raundi ya pili baada ya kufukuzwa kocha George Semogerere raia wa Uganda na jahazi lote kukabidhiwa Kabange.


Akizungumzia sababu ya kufukuzwa baadhi ya makocha katika timu hiyo, Kabange anasema si suala la kushangaza kwa kuwa kipimo cha mwalimu wa timu ya mpira wa miguu ni timu kufanya vizuri.Amesema hata yeye haitakuwa ajabu kuondolewa Kagera aliyopewa ubosi baada ya kupigwa chini Semogerere aliyewahi kucheza soka kwa mafanikio katika timu ya Sports Club Villa na timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.


Kocha huyo ameonyesha ana uwezo wa kuiongoza tena timu hiyo kwa msimu ujao kama atafanya usajili wa kurekebisha baadhi ya mapengo katika kikosi hicho na kwa kuibakisha ligi kuu anastahili sifa.
JUMA MWAMBUSI


Ujiko aliojipatia wakati alipokuwa Prisons ya Mbeya msimu wa 2007/2008 umepotea akiwa katika Moro United kutokana na timu hiyo kushuka daraja.Kocha huyo alishuhudia jahazi hilo likishuka daraja kwa kufungwa katika mechi nyingi na chache kuambulia sare. Ingawa, inasemekana aliondoka wakati timu hiyo ikibakiwa na michezo michache, hakwepi matokeo mabaya yaliyoikumba Moro United.Japokuwa kushuka kwa Moro kunaweza kusichafue sifa yake moja kwa moja, katika historia yake kamwe hatasahau kama kuna timu ilishuka ikiwa mikononi mwake na baadaye ataweza kufanya vizuri akiwa na timu hiyo au nyingine.
MAKOCHA WALIOFUKUZWA
EDUARDO ALMEIDA


Baada ya kuahidi kufanya mambo makubwa katika timu hiyo alipozungumza na waandishi wa habari pembeni yake akiwepo mmiliki wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, kocha huyo alifukuzwa baada ya mechi tano tu za raundi ya kwanza kutokana na ‘kuijaza maji’ boti ya Lyon.Kabla ya kufukuzwa Mreno huyo alishushwa cheo kwa kuwa kocha msaidizi wa mzawa Jumanne Chale, ambaye naye alitupiwa virago na kazi hiyo kupewa Mkwasa na Matola.Pamoja na Almeida kutoswa kabla meli haijazama, Lyon ilikosa mafanikio katika ligi na kujikuta ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi saba katika mechi 11 ilizocheza.
AHMED MUMBA/ DAVID MWAMAJA


Mumba ndiye alikuwa kocha mkuu wa Majimaji ilipopanda Ligi Kuu msimu huu, lakini baada ya timu hiyo kupigwa mawimbi makali kwa kupoteza baadhi ya mechi mapema, alijikuta katika wakati mgumu.Licha ya kuitoa Yanga machozi kwa kuitandika bao 1-0 katika mechi ya pili ya Ligi Kuu na kupoza machungu ya kulizwa na Simba nyumbani kwao, mashabiki wa timu hiyo mjini Songea walisahau mazuri yake.Walimbeza kuwa hana uwezo kutokana na kufungwa mechi kadhaa nyumbani na ugenini, ambapo kelele hizo zilimnyima raha Mumba na kuahidi kushinda mechi zilizokuwa mbele yake, lakini mwisho wa siku aliwekwa kando katika ukocha na nafasi yake kupewa David Mwamaja.Mwamaja naye ametimuliwa Majimaji katika mzunguko wa pili kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, lakini vipigo kutoka kwa Azam na Yanga huenda vilichangia aonyeshwe mlango wa kutokea na timu kubaki kwa kocha msaidizi Peter Mhina.
HASSANI MLILWO


Ni ofisa wa Jeshi la Magereza aliyepewa ukocha mkuu wa Tanzania Prisons ili kumuongezea nguvu James Nestory.Uwepo wake katika timu hiyo ulishindwa kufua dafu hasa katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyochezwa nchini Sudan mwaka jana na kujikuta wanaaga mapema.Chini ya Mlwilo na Nestory aliyewahi kuichezea Prisons kabla ya kustaafu, Prisons pia imekuwa nyanya katika ligi kuu ya Vodacom.Uongozi wa Prisons ulimtema Mlwilo na kukabidhi kikosi kwa Danny Koroso, lakini naye inadaiwa aling’olewa na timu kubaki kwa Nestory. Ilimaliza ligi jana kwa kucheza na Yanga ushujaa wa ‘kaimu’ huyo utatokana na timu kunusurika kushuka daraja na vinginevyo atakuwa ameshindwa kuonyesha cheche katika kazi ya ukocha kwa vile timu itashuka akishuhudia. Kabla ya kucheza na Yanga Prisons ilikuwa na pointi 20 na iligota kwenye nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi kuu.
MBWANA MAKATA


Alikuwa kocha wa Toto African ya Mwanza, ambayo huenda kushindwa kwa timu hiyo kupiga makasia yao vyema kwenye ligi kuu kulichangia atoweke kabla ya kuambiwa aondoke.Makata alisikika katika vyombo vya habari akisema kuwa alirudi Dar es Salaam kujiuguza kwa kuwa afya yake si nzuri na hakuonekana tena kwenye jiji la Mwanza kuendelea na kazi yake hivyo kuwa amekimbia balaa mapema. Kocha msaidizi Choki Abeid ndiye aliyebaki na Toto.
DUSAN KONDIC


Mserbia huyo alifunga dimba katika orodha ya makocha waliong’olewa katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, lakini katika raundi ya pili alipata wenzake wa kuondoka nao. Kocha huyo licha ya kuipa Yanga ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo, alitupiwa virago baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi ya msimu huu kuanza kwa kusuasua hali iliyosababisha hata ipote taji kabisa ambalo limechukuliwa na Simba.Nafasi ya Kondic ilichukuliwa na Mserbia mwenzake Kostadin Papic.
ABDALLAH KIBADENI


Uongozi wa Manyema Rangers ulimtimua baada ya kushindwa kuipa timu ushindi katika mechi tatu alizokuwa masharti kuwa lazima ashinde ili kuiepusha timu na janga la kushuka daraja.Aliwaongoza vizuri Manyema katika mzunguko wa kwanza na hatua ya pili akajikuta anashindwa kazi na hivyo kuwekwa pembeni kwa kipimo cha mafanikio aliyoshindwa kutimiza kama ilivyokuwa inatarajiwa na uongozi wa klabu hiyo.
GEORGE SEMOGERERE


Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ alifukuzwa baada ya duru la kwanza kumalizika kutokana na kuiweka Kagera Sugar katika kona hatari ya kung’oka ligi kuu msimu huu.Timu hiyo ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 12 tu na ndipo wamiliki wa Kagera wakamwambia akae kando na nafasi hiyo kupewa msaidizi wake Mrage Kabange aliyejitahidi kurejesha uhai wa timu hadi kufanikiwa kubaki ligi kuu ya msimu ujao.

No comments:

Post a Comment