KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

Nigeria vinara wa kughushi umri wa wachezaji



LAGOS, NigeriaUMRI wa mchezaji Nwankwo Kanu wa Nigeria kwa sasa ni miaka 42 na ule wa Taribo West, ambaye alistaafu soka miaka miwili iliyopita, ni miaka 50.
Hayo ni baadhi tu ya maelezo yaliyotolewa na wamiliki mbalimbali wa mitandao ya kompyuta, maarufu kwa jina la ‘blogs’ nchini Nigeria.Baadhi ya mitandao hiyo imeeleza kuwa, umri unaotajwa kuwa ni wa Kanu ni miaka 33, lakini umri wake halisi ni miaka 42.Naye Obafemi Martins anatajwa kuwa na umri wa miaka 25, lakini umri wake halisi ni miaka 32 wakati
Jay-Jay Okocha alikuwa na miaka 10 zaidi ya umri uliokuwa ukitajwa kwenye hati yake ya kusafiria.

Ni nani anayetoa kauli hizo? Wananchi kadhaa wa Nigeria wametoa maelezo hayo kupitia kwenye ‘blogs’ maarufu nchini humo, walipokuwa wakielezea sababu za
kutolewa mapema kwa timu ya taifa ya nchi hiyo, ‘Super Eagles’, katika fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika mwezi uliopita nchini Angola.Kushindwa kwa Nigeria kutwaa kombe hilo, siku zote kumekuwa kukichukuliwa kama tukio lisilo la
kawaida, lakini safari hii kumechukua sura mpya.Kocha wa zamani wa moja ya klabu kubwa za Nigeria, alilieleza gazeti la Guardian: “Kile kilichotokea Angola ni uthibitisho wa kile, ambacho kimekuwa kikitokea katika miaka ya hivi karibuni, ambapo wachezaji wengi wamekuwa wakidanganya umri wao wakati wa michuano hiyo. Wachezaji wengi umri wao huwa ni zaidi ya ule wanaoutaja na hii inasababisha iwe vigumu kwao kuhimili vishindo vya timu kama Zambia na Benin.”

Kutolewa mapema kwa Nigeria katika michuano hiyo pia kumezua mijadala mingi nchini humo, hasa ikizingatiwa kuwa imesalia miezi mitatu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, zitakazofanyika nchini Afrika Kusini.

“Vijana wetu ni wakubwa kiumri, hivyo tunalipa gharama za kudanganya umri wao,”alisema Ken Anugweje, daktari wa zamani wa Super Eagles na mjumbe wa bodi ya Chama cha Soka cha Nigeria (NFA).Tatizo la umri halisi kwa baadhi ya wachezaji wa Nigeria lilianza miaka 20 iliyopita. Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) liliifungia nchi hiyo kushiriki michuano yote ya kimataifa kwa miaka miwili baada ya kugundulika kuwa, tarehe za kuzaliwa za wachezaji wake watatu walioshiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 1988, zilikuwa tofauti na zile zilizotumiwa na wachezaji hao katika michezo iliyopita.Mwaka uliofuata, mwanasoka nyota wa zamani wa dunia, Pele alibashiri kwamba, timu moja ya Afrika itaweza kutwaa Kombe la Dunia ndani ya kipindi cha miaka 15, baada ya kuiona timu ya Nigeria ya vijana wa chini ya miaka 17, ikitwaa kombe la dunia na na ile ya vijana wa chini ya miaka 20 kufuzu kucheza fainali za kombe hilo.

Lakini ukweli ni kwamba, timu ya vijana wa chini ya miaka 20 ya mwaka 1989, haikuwa na wachezaji wenye umri huo. Wengi walikuwa na umri mkubwa, akiwemo mchezaji aliyetumia jina la George Onmonya.

Kwa mujibu wa tovuti ya ‘nigeriavillagesquad.com’, wachezaji wengi walioichezea Nigeria katika mwaka huo hivi sasa wamestaafu na wengine wanaitwa babu.Nigeria ina hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji, ambao baadhi yao walishindwa kutimiza ndoto zao. Mfano wa wachezaji hao ni Phillip Osondu, ambaye alikuwa mchezaji bora katika fainali za kombe la dunia za vijana wa chini ya miaka 17 za mwaka 1987.

Lakini mara baada ya kunyakuliwa na klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji, alijikuta akishindwa kutimiza ndoto zake na kuamua kufanya shughuli nyingine badala ya kucheza soka baada ya kutokea utata kuhusu umri wake halisi.Nyota huyo wa Nigeria katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2001 kwa vijana wa chini ya miaka 17, pia aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo kucheza fainali za wakubwa za kombe hilo wakati Nigeria ilipomenyana na England na kutoka nayo suluhu mwaka 2002.

“Rafiki yangu mmoja, ambaye aliwahi kucheza katika ligi ya Nigeria alinieleza kwamba, umri wake halisi wakati huo ulikuwa miaka 34, lakini kisoka alikuwa akijulikana ana umri wa miaka 21,” ameandika mchangiaji mmoja kwenye moja ya ‘blogs’ hizo.

“Leo hii unaweza kwenda kwenye ofisi yoyote ya Idara ya Uhamiaji Nigeria na kughushi fomu za
maombi ya hati ya kusafiria, ukabadili jina, mahali pa kuzaliwa, tarehe ya kuzaliwa na kulipa naira 7,000 au 10,000 badala ya kulipa naira 5,500 kwa hati ya kusafiria ya kimataifa na baada ya saa chache unakuwa umekamilisha taratibu zote,”aliongeza.

“Hii inamaanisha kwamba, unakuwa na hati mpya ya kusafiria, unakuwa mtu mpya, na kama ni
mwanasoka, unakuwa na umri mdogo kuliko umri wako halisi,”alisema.

Mfanyakazi wa zamani wa ubalozi wa Uingereza nchini Nigeria alilieleza gazeti la Observer kwamba, watu walipokuwa wakienda ubalozini na kumlalamikia kuhusu maombi yao kukataliwa, alikuwa akiwajibu: “Usizungumze na mimi kuhusu hilo, nimeshakufa.”

Alipoona majibu yake yanawashangaza watu hao, aliwaonyesha kwa kidole kwenye ukuta wa nyuma ya kiti chake, ambako alibandika cheti chake cha kifo, kilichoghushiwa na kununuliwa kwa bei nafuu kutoka kwa mfanyabiashara mmoja nchini humo.

Tayari FIFA imeshatangaza kuwa, imepata chombo maalumu kwa ajili ya kupima umri wa wachezaji. Kabla ya fainali za kombe la dunia za vijana wa chini ya miaka 17 zilizofanyika mwaka jana nchini Nigeria, shirikisho hilo lilitangaza kuwa, wachezaji watafanyiwa vipimo hivyo ili kubaini umri wao alisi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Hatua hiyo ya FIFA ilizifanya nchi nyingi nazo kuamua kuwapima wachezaji wake kabla ya kushiriki kwenye michuano inayozingatia umri. Lakini matokeo ya vipimo hivyo hayajatangazwa.Kabla ya kuanza kwa fainali hizo, Nigeria iliwaengua wachezaji wake 15 wakati Ghana iliwaengua wachezaji 11 kati ya 18 walioiwezesha kutwaa ubingwa wa Afrika miezi michache iliyopita.Ripoti zimeeleza kuwa, uchunguzi uliofanywa katika fainali tatu za kombe la dunia za vijana wa chini ya miaka 17, umeonyesha kuwa, zaidi ya theluthi moja ya wachezaji walikuwa na umri mkubwa.

No comments:

Post a Comment