TIMU ya soka ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars mwishoni mwa wiki iliyopita ilifuzu kucheza raundi ya pili ya michuano ya Afrika baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ethiopia. Licha ya kusonga mbele katika michuano hiyo, Twiga Stars ilionyesha mapungufu mengi kwenye kikosi chake. Makala hii ya Rashid Zahor Wetu inafafanua zaidi kuhusu mapungufu hayo.
Twiga Stars imesonga mbele katika michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, kufuatia ushindi wa mabao 3-1 ilioupata katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Twiga Stars sasa itacheza raundi ya pili kwa kupambana na Eritrea, ambayo imesonga mbele baada ya Kenya kujitoa.
Licha ya kusonga mbele katika michuano hiyo, Twiga Stars ilionyesha udhaifu mkubwa kiuchezaji, ikiwa ni pamoja na wachezaji wake kukosa stamina na kushindwa kumiliki vyema mipira.Uchezaji uliionyeshwa na Twiga Stars katika mechi hiyo ulionyesha dhahiri kwamba hawakupata mafunzo mazuri na ya kitaalam ya kucheza soka na haikueleweka ni mfumo upi waliokuwa wakiutumia.
Wapinzani wao Ethiopia walicheza mpira wa kufundishwa. Walijaza viungo wengi katikati na hivyo kutawala vyema idara hiyo. Walikuwa wakifanya mashambulizi na kuzuia kwa pamoja.
Kutokana na uchezaji wao huo, mashabiki wengi waliohudhuria mechi hiyo walihoji Twiga Starsiliwezaje kuifunga Ethiopia nyumbani. Wengi hawakuamini kile walichokuwa wakikiona uwanjani.Washambuliaji wa Twiga Stars walishindwa kufanya mashambulizi kimpangilio kwenye lango la Ethiopia.
Walishindwa kuingia mara kwa mara ndani ya mita 18 na mashuti yao yalikuwa dhaifu.Kwa ujumla timu ya Twiga Stars ilishindwa kucheza kwa mfumo unaoeleweka. Uwezo wa wachezajiulionekana mdogo na hawakuwa makini.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wachezaji wa Twiga Stars walishindwa kugongeana pasi tano kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Ethiopia. Kila mchezaji alicheza kwa kutumia kipaji chake binafsi.
Cha kushangaza, hata pale wachezaji walipoonekana kuchoka, makocha Charles Boniface naMohammed Rishard walishindwa kufanya mabadiliko, hali iliyoonyesha dhahiri kwamba hakukuwa na mbadala wao.
Pengine kinachoifanya Twiga Stars isiwe tishio sana katika michuano hiyo ni timu kubadilika mara kwa mara. Katika kikosi cha mwaka huu, wapo wachezaji wanne pekee walioichezea mwaka juzi ilipomenyana na Cameroon.
Pamoja na kuwepo kwa mapungufu hayo, baadhi ya wachezaji kama vile kipa Fatuma Omary, mabeki Pulkeria Charaji, Helen Peter na washambuliaji Mwanahamisi Omary, Asha Rashid na Etoo Mlenzi wameonyesha uwezo wa juu kiuchezaji, lakini wanakosa mafunzo ya kuwaonganisha vyema na wenzao.Akizungumza baada ya pambano hilo, Rishard, maarufu kwa jina la Adolph alikiri kuwa, wachezaji wa Twiga Stars hawana uzoefu wa michuano ya kimataifa na wana matatizo katika ukabaji.
“Hadi sasa hawaelewi maana ya kukaba, ndiyo sababu walikuwa wakiwaachia wachezaji wa Ethiopia wakitamba na mipira. Tutaendelea kuwaelimisha kuhusu jambo hilo,”alisema.
Adolph alikiri kwamba, kiwango cha Ethiopia kipo juu kwa vile soka ya wanawake ilianza nchini humo tangu miaka ya 1970, tofauti na Tanzania, ambayo soka hiyo ilianza kuchezwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.
“Sisi hapa wachezaji wetu wengi wanatoka Dar es Salaam na hatuna ligi ya taifa ya wanawake. Tatizo hili litaendelea kutusumbua kwa muda mrefu kama hakutakuwa na mabadiliko katika uendeshaji wa soka ya wanawake,”alisema.
Kwa upande wake, Boniface alisema Ethiopia ilicheza vizuri zaidi ikilinganishwa na Twiga Stars, lakini tatizo lao kubwa lilikuwa katika umaliziaji.
“Kwa kweli Waethiopia walikuwa na uwezo mkubwa wa kututoa, lakini walishindwa kumalizia vyema mashambulizi yao,”alisema.
“Tunashukuru kwamba tumeshinda na kusonga mbele, lakini tunahitaji maandalizi kabambe kabla ya kupambana na Eritrea,”aliongeza.
Boniface alisema taarifa alizonazo ni kwamba kwa sasa Eritrea ipo nchini Ujerumani, ilikokwenda kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo, hivyo wanapaswa kuwa makini kabla ya kupambana nayo.
Aliishukuru serikali kwa kuamua kuisaidia timu hiyo kuanzia raundi ya pili na kuongeza kuwa, jambo hilo linaweza kuwaongezea ari zaidi wachezaji ya kufanya vizuri.
Japokuwa Twiga Stars imeshawahi kucheza na Eritrea mara mbili katika michuano hiyo na kuitoa, lakini kikosi chake cha sasa si imara kama kile cha miaka ya nyuma, hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ili kukiimarisha.
Baadhi ya mbinu zinazoweza kutumiwa kukiimarisha kikosi hicho ni pamoja na kuwapa mazoezi ya kuwaongezea stamina wachezaji na kuwafundisha mfumo unaoeleweka wa kucheza soka.
Makocha Boniface na Adolph pia wanapaswa kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo umuhimu wakuwakaba wachezaji wa timu pinzani ili kutowapa mwanya wa kutawala na mipira uwanjani.Ieleweke kuwa, iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Eritrea, itafuzu moja kwa moja kucheza fainali za michuano hiyo zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini. Hivyo timu isipopewa maandalizi ya kitaalam, tunaweza kwenda kutia aibu katika fainali hizo.
No comments:
Post a Comment