TIMU za soka na netiboli za Uhuru zimeamua kujitoa katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la NSSF, inaotarajiwa kuanza Jumamosi kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Uhuru SC, Rashid Zahor alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamefikia uamuzi huo kutokana na mizengwe waliyofanyiwa na kamati ya mashindano hayo.Zahor alisema wameshangazwa na uamuzi wa kamati hiyo kuwazuia wachezaji wake tisa wa soka na sita wa netiboli kucheza michuano hiyo kwa madai kuwa sio waajiriwa.
Aliwataja wachezaji wa soka waliotiliwa shaka kuwa ni Tuzo Jackson, Ally Mohamed, Moni Lyambiko, Hamidu Shomari, Anthony Cyprian, Nassibu Hussein, Rashid Kazumba, Emmanuel Mushi na Brenda Damian.
Kwa upande wa netiboli, wachezaji waliotiliwa shaka ni Mariam Mkali, Sophia Ally, Salome Lazaro, Stella Charles, Sharifa Seif na Happy Aggrey.Alisema ni jambo la kushangaza kuona kuwa, kamati ndogo ya uhakiki imewaita wachezaji hao kuwa si waajiriwa wakati ilionyeshwa vielelezo vyote vya kuthibitisha ajira zao.“Ukimuondoa Mariam Mkali, ambaye ni mfanyakazi mpya aliyeajiriwa mwaka jana idara ya matangazo, wachezaji wengine wote wamekuwa wakiichezea Uhuru kwa miaka mitano sasa kwenye mashindano hayo, sasa iweje kamati iseme si waajiriwa,”alihoji..
“Hii ni mizengwe iliyoandaliwa mapema na wajumbe wa kamati ya mashindano kwa lengo la kuidhoofisha Uhuru ili isifanye vizuri, hasa baada ya kuwa imetwaa ubingwa mara mbili mfululizo,”alisema.“Vyombo vingi vya habari havifurahii mafanikio ya Uhuru, vinaiogopa, vilikuwa na hakika kwamba itatwaa tena ubingwa mwaka huu, ndiyo sababu viliandaa mizengwe mapema,”aliongeza.
Zahor alisema kuondolewa kwake kwenye nafasi ya katibu wa kamati hakukumshangaza kwa sababu ni zengwe lililoandaliwa mapema na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Masoud Saanani kwa kuonekana angekuwa kikwazo kwa timu yake ya Business Times kutwaa ubingwa.Alisema mapendekezo ya kamati ya uhakiki kwamba aondolewe kwenye nafasi hiyo kutokana na kushindwa kusimamia vyema usajili wa timu yake hayana msingi kwa sababu yeye hayumo kwenye kamati ya usajili.
“Usajili wa wachezaji wa Uhuru kwa ajili ya mashindano mbalimbali umekuwa ukisimamiwa na manahodha wa timu zote mbili pamoja na wasaidizi wao. Mimi nahusika na masuala ya kiutawala ya timu, hivyo wamenitwisha tuhuma ambazo hazinihusu,”alisema.
Katibu huyo wa Uhuru alisema kazi ya ukatibu wa kamati alikuwa akiifanya kwa kujitolea zaidi na kwamba ilikuwa ikimbebesha lawama nyingi kila timu zilipoondolewa kwa makosa mbalimbali kwa kuonekana yeye ndiye aliyepitisha maamuzi hayo.
“Wakati mwingine kazi za kamati zilikuwa nyingi kiasi cha kunikosesha muda wa kufanyakazi za kampuni iliyoniajiri ilhali posho niliyokuwa nikilipwa ilikuwa ni sawa na za wajumbe wengine, ndiyo sababu nimesema ilikuwa kazi ya kujitolea zaidi,”alisema.
Zahor alisema wameandika barua rasmi kwa uongozi wa NSSF kwa ajili ya kulalamikia mizengwe waliyofanyiwa na pia kuomba warejeshewe sh. 100,000 walizolipa kwa ajili ya ada ya kiingilio.
No comments:
Post a Comment