KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Simba kuongeza wapiga mabao wawili


KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri amesema anafanya mipango ya kusajili washambuliaji wapya wawili na kiungo mmoja kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Phiri alisema amepanga kusajili wachezaji hao kwa lengo la kukiimarisha zaidi kikosi chake.
Hata hivyo, Phiri hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji hao, lakini kuna habari kuwa, miongoni mwao ni kiungo Abdulrahim Humoud kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Phiri alikiri kuwa, baadhi ya wachezaji walioichezea Simba msimu huu, kiwango chao kimeshuka na hatarajii kuwa nao msimu ujao, ndio sababu ameanza mapema mipango ya kuziba mapengo yao.
Mbali na Humuod, mchezaji mwingine, ambaye ametajwa kuwa huenda akasajiliwa na Simba msimu ujao ni mshambuliaji Mumba Felix Sunzu kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Chanzo cha habari kimelidokeza gazeti hili kuwa, Sunzu anatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, Simba huenda ikakumbana na kizingiti kikubwa cha kumsajili mchezaji huyo baada ya klabu ya FC Lupopo kusema inataka ilipwe sh. milioni 195 kwa ajili ya ada ya uhamisho.
Wachezaji wengine, ambao Simba imepanga kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao wanatarajiwa kutoka katika klabu za Dynamo na Lengthens za Zimbabwe.
“Lengo langu ni kuongeza nguvu sehemu zenye mapungufu na kuimarisha zaidi safu ya ushambuliaji kwani kama unavyojua, timu inakabiliwa na michuano migumu ya Afrika,”alisema.
Wachezaji wa kigeni walioichezea Simba msimu huu ni beki Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda, viungo Hillary Echessa, Jerry Santo na mshambuliaji Mike Baraza kutoka Kenya.

No comments:

Post a Comment