KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

CAPELLO: Enzi za klabu za England kutamba Ulaya zimekwisha

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya England, Fabio capello amezionya klabu kubwa za England kuwa zitashindwa kuendelea kutamba barani Ulaya iwapo zitashindwa kuwekeza kwa kusajili wachezaji nyota.
Onyo hilo la Capello limekuja siku chache baada ya miamba ya soka nchini humo, Chelsea, Manchester United na Arsenal kutolewa mapema katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Kutolewa mapema kwa miamba hiyo ya soka kunamaanisha kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya ligi ya mabingwa wa Ulaya tangu mwaka 2003, mechi za robo fainali zitafanyika bila ya kuwepo wawakilishi wa England.
Capello alizisikitikia Chelsea na Manchester United kwa kufungashwa virago mapema na timu za Inter Milan ya Italia na Bayern Munich ya Ujerumani katika hatua ya robo fainali.
Kocha huyo alisema: “Ikilinganishwa na msimu uliopita, klabu zote za England ziliuza wachezaji wake muhimu. Baadhi walikwenda nje ya nchi, wengine walihamia klabu mpya, ikiwemo Manchester City. Ni wazi kwamba zilidhoofika.”
“Kwa uzoefu wangu, kama klabu ipo juu, inapaswa kununua mchezaji mmoja au wawili wenye kiwango cha juu kila mwaka ili iweze kubaki nafasi za juu, ikizingatiwa kuwa, upinzani unazidi kuwa mkali,” aliongeza.
“Haishangazi kuona kwamba, klabu zilizotumia fedha nyingi kusajili wachezaji wapya msimu huu kama vile, Barcelona, Inter Milan na Bayern ndizo zilizofuzu kucheza nusu fainali msimu huu,”alisema kocha huyo.
Capello alisema ni wazi kwamba mtikisiko wa kiuchumi duniani umeziathiri klabu nyingi barani Ulaya, baada ya kuwa zimetingisha kisoka kwa miaka kadhaa.
Alisema mbali na Manchester City, klabu zilizopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu, zilikuwa Real Madrid na Inter Milan, ambazo zilitumia mamilioni ya pesa kwa ajili ya kujiimarisha.
Kocha huyo alisema, Rais wa Real Madrid, Florentino Perez alifanya kila aliloweza kuirejesha kwenye chati klabu hiyo wakati Inter Milan ilinunua wachezaji wapya sita.
“Uwekezaji ni muhimu, lakini unapaswa kufanywa kwa umakini. Unapaswa kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuelewana na wenzao kwa haraka na kupata mafanikio,”alisema.
“Hata hivyo, jambo hili si la lazima, baadhi ya wachezaji hupata wakati mgumu kufiti kwenye klabu mpya, hata kama ni kutoka klabu ndogo kwenda klabu kubwa,”aliongeza.
Licha ya kuondoka kwa Cristiano Ronaldo na Carlos Tevez katika klabu ya Manchester United na usajili mdogo uliofanywa na Carlo Ancelotti ndani ya Chelsea, Capello alisema timu hizo mbili zilipaswa kuendelea kuwemo kwenye michuano hiyo hadi sasa.
Lakini alikiri kuwa, uamuzi wa Arsenal kuwauza Emmanuel Adebayor na Kolo Toure kwa klabu ya Manchester City, kulichangia kuidhoofisha na kuifanya itolewe na Barcelona.
Kocha huyo alisema, Manchester United haikuwa na bahati kwa sababu ililipa kutokana na makosa iliyoyafanya, kama ilivyoizawadia Bayerm Munich bao la pili mjini Munich na kuiruhusu kupata bao la kwanza baada ya kuwa mbele kwa mabao 3-0 ziliporudiana kwenye uwanja wa Old Trafford.
“Kilichofanya kuwepo na tofauti ni kutolewa kwa kadi nyekundu beki Rafael na kuumia kwa Wayne Rooney. Huwezi kuendelea mbele katika michuano hii ukiwa na matatizo ya aina hii,”alisema.
Capello alisema Chelsea ilicheza vizuri mjini Milan na ingeweza kupata matokeo mazuri na kwamba Inter Milan ingepaswa kucheza mchezo tofauti kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
“Kama ilivyotokea, Inter Milan ilicheza vizuri mechi ya marudiano,”alisema.
Akiizungumzia Arsenal, kocha huyo alisema haikuwa na bahati kutokana na kuwapoteza wachezaji wake nyota watano, ambao ni majeruhi. Wachezaji hao ni Van Persie, Cesc Fabregas, Arshavin, William Galas na Ramsey. Alisema Arsenal iliwahitaji wachezaji hao ili iweze kusonga mbele.
Kocha huyo aliwaeleza Rooney na Lionel Messi wa Barcelona kuwa ni wachezaji tofauti, lakini wenye uweo mkubwa. Alisema ni jambo linalofurahisha kuwazungumzia wachezaji hao pamoja na Ronaldo.
Capello alikataa kumlaumu Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson kwa uamuzi wake wa kumchezesha Rooney katika mechi dhidi ya Bayern ya kupona sawasawa maumivu ya kifundo cha mguu.
Alisema kuumia kwa wachezaji hao na wengineo wa England, huenda kukatia doa mipango yake katika michuano ya mwaka huu ya fainali za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini.
“Naelewa wazi uamuzi wa Sir Alex wa kumchezesha Rooney kwa sababu anaelewa umuhimu wake kwa timu nzima,”alisema Capello. “Sifikirii kama alifanya kosa. Kama Sir Alex alimchezesha Rooney, bila shaka hali yake ilimruhusu kufanya hivyo.”
“Bahati pekee ni kwamba wachezaji wote wa England watapatikana mwanzoni mwa maandalizi yetu nchini Austria. Wakati wachezaji wanaposhinda mataji, wanakuwa na furaha kubwa na naamini hilo litakuwa na mafanikio kwetu,”alisema.
“Kitu muhimu kitakuwa ni kwa wachezaji wote wa England kupona na kuwa kwenye kiwango chao cha kawaida, mambo ambayo yalitusaidia kufanya vizuri katika mechi za kufuzu kombe la dunia,”alisema.
Capello alisema amekuwa akiwafuatilia kwa makini wachezaji wake wote na kwamba, daktari wa England amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na madaktari wa klabu ili kujua maendeleo ya hali zao.
Kocha huyo alisema haitakuwa na maana kwake kuzungumza na madaktari wa klabu au wachezaji kwa vile hawawezi kupata picha kamili. Alisema anazungumza na wachezaji anapokutana nao kwenye mechi, lakini si kwa lengo la kufuatilia hali zao.
00000

No comments:

Post a Comment