KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Dully Sykes ajitoa tuzo za Kili


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Dully Sykes ametangaza kujitoa katika shindano la mwaka huu la kuwania tuzo za muziki za Kilimanjaro.
Dully, maarufu kwa jina la Mr. Misifa alitangaza uamuzi wake huo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai kuwa, haoni faida ya tuzo hizo.
“Nilishasema sitaki kuwekwa kwenye katagori yoyote ile ya Kili Music Award, sioni faida ya tuzo hizo,”alisema Dully, ambaye kwa sasa anatamba kwa kibao chake cha ‘Shekidee’.
“Sijawahi kupata tuzo hizo tangu nianze muziki. Nimetoa singo 36 mpaka sasa kama vile Salome, Hunifahamu na nyinginezo kibao, lakini ajabu ni kwamba hakuna hata moja iliyopata tuzo,”alisema.
Msanii huyo machachari na mwenye mvuto kwa mabinti wa kike alisema, ni bora aendelee kurekodi singo kwa vile zinalipa kuliko kurekodi albamu nzima.
Dully amekuwa msanii wa pili kujitoa kwenye tuzo za mwaka huu. Wa kwanza alikuwa Khaleed Mohamed, maarufu kwa jina la TID, aliyetangaza kujitoa wiki mbili zilizopita.
TID alifikia uamuzi huo kwa madai ya kutoridhishwa na uteuzi uliofanywa na majaji wa shindano hilo kuhusu nyimbo zake na tuzo alizoingizwa kuziwania.
Kiongozi huyo wa bendi ya Top alisema, amekuwa akitengeneza nyimbo nyingi zinazopendwa na kukubalika na mashabiki, lakini hajawahi kupewa tuzo, hivyo haoni sababu ya kuendelea kushindanishwa katika kuziwania.
Sababu nyingine iliyotajwa na TID ni kushindanishwa kuwania tuzo hizo na wasanii wasiokuwa na sifa, hivyo anaona ni bora aendelee kutumia muda wake mwingi kufanyakazi zake binafsi.

No comments:

Post a Comment