TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes leo itajitupa dimbani kumenyana na Malawi katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika.
Pambano hilo linalotarajiwa kuwa la vuta nikuvute, litapigwa kuanzia saa 9.30 alasiri kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pambano hilo limepangwa kuanza mapema, ili kama matokeo yatakuwa sare, kuwepo na muda wa nyongeza na wa kupigiana penalti tano tano.
Katika pambano la awali, lililochezwa wiki mbili zilizopita mjini Lilongwe, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Ili ifuzu kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo, Ngorongoro italazimika kuifunga Malawi kwa idadi yoyote ya mabao na kutowaruhusu wapinzani wao kupata bao la ugenini.
Malawi ilitarajiwa kuwasili nchini jana mchana, ikiwa na msafara wa wachezaji 20 na viongozi watano.
Kwa mujibu wa Kaijage, baadhi ya mashabiki watakaohudhuria pambano hilo na kukaa kwenye eneo la mzunguko, hawatatozwa kiingilio. Eneo hilo ndilo linalochukua mashabiki wengi ikilinganishwa na kwenye majukwaa.
Kaijage alisema ofa ya kuruhusu mashabiki waingie uwanjani bure, itatoa hamasa kwao kuishangilia Ngorongoro muda wote wa mchezo na hivyo kuwapa ari wachezaji ya kushinda pambano hilo.
Ofisa huyo wa TFF alisema, mashabiki wengine watakaokaa jukwaa kubwa na la kijani watalipa kiingilio. Alivitaja viingilio hivyo kuwa ni sh. 10,000 kwa VIP, sh. 5,000 kwa jukwaa kubwa na sh. 3,000 kwa jukwaa la kijani.
Alisema mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Eritrea. Aliwataja waamuzi hao kuwa ni Gebremichael Luelsged, Mohamed Berhane na Tesfagiorghis O’Michael wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Ibada Ramadhani wa Tanzania.
Iwapo Ngorongoro itaitoa Malawi, itakutana na Ivory Coast katika raundi ya pili. Fainali za michuano hiyo zimepangwa kufanyika mwaka 2011 nchini Libya.
No comments:
Post a Comment