KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

Omotola akana kuwa na uhusiano na Jim Iyke



LAGOS, Nigeria

OMOTOLA Jalade ni mmoja wa waigizaji nyota na maarufu wa filamu nchini Nigeria. Baada ya kuwemo kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 13, bado nyota yake inang’ara, kama ambavyo sura yake imekuwa kivutia kikubwa kwa mashabiki wa fani hiyo.

Kila anaposhiriki kuigiza filamu yoyote, lazima iwe na mvuto. Uigizaji wake, umbile lake, sura yake ya kitoto na miondoko yake ni baadhi ya vitu vilivyomfanya awe kivutio kikubwa kwa mashabiki wa fani hiyo.

Omotola pia ni mwanamuziki. Kibao chake cha ‘Gba’, alichokirekodi miaka mitatu iliyopita kilishika chati za juu kwenye vituo vya radio na televisheni nchini Nigeria, kama ilivyokuwa kwa albamu yake ya kwanza, ambayo iliuzwa nakala nyingi kuliko za wanamuziki nyota wa nchi hiyo.

Mwigizaji huyo pia amekuwa akijihusisha na kazi mbalimbali za kujitolea. Pia ni balozi wa Umoja wa Mataifa katika masuala yanayohusu wakimbizi.

Akihojiwa na waandishi wa habari mjini Lagos hivi karibuni, Omotola alisema uamuzi wake wa kujitosa katika fani ya muziki hauna maana kwamba fani ya filamu hailipi.

“Sifanyikazi zangu kutokana na shinikizo la watu. Si kwa sababu watu wengine wanapiga muziki kama ninavyofanya mimi. Watu walio karibu na mimi watakueleza kwamba, sifanyi vitu kwa sababu watu wengine wanavifanya. Nilichogundua ni kwamba, baadhi ya watu wamekuwa wakipenda kufanya vitu vinavyofanana na nilivyovifanya. Inawezekana ni kwa sababu watu wamekuwa wakiniunga mkono,”alisema.

Omotola alisema muziki si kitu ambacho mtu anaweza kuamka na kusema anataka kukifanya. Alisema anapiga muziki kwa lengo la kueleza hisia zake. Alisema anafurahia kupiga muziki.

Hata hivyo, Omotola alisema anazipenda fani zote mbili kwa vile zinamwezesha kuwasilisha hisia zake kwa jamii. Alisema katika filamu, anaigiza kutokana na maelezo ya hadithi, lakini hadithi si yake. Lakini katika muziki, ni kitu anachopenda kukifanya, ni hadithi yake na anaandika nyimbo zake.

“Katika albamu yangu ijayo, nimeandika asilimia 50 ya nyimbo zilizomo ndani yake. Zingine,
nilihakikisha ni nyimbo ninazoweza kuelezea hadithi yangu, zikielezea hisia zangu,”alisema.

Omotola alisema ameamua kupiga zaidi muziki wa miondoko ya rock kwa sababu ni rahisi kuelezea hisia zake kuliko muziki wa miondoko ya R&B ambao ni wa taratibu zaidi.

“Nahisi kama hatua ifuatayo ya maisha yangu imeshaanza. Najiamini sasa. Siku zote nimekuwa
nikijiamini, lakini najiamini zaidi kwa sasa,”alisema.

“Kuna vitu ambavyo ningependa kuvizungumzia, lakini inaniwia vigumu kuelezea hisia zangu katika miondoko ya R&B,”aliongeza mwanadada huyo, ambaye ni mama wa watoto wane.

Omotola alisema haikuwa vigumu kwake kujitosa kwenye fani ya uigizaji filamu kwa sababu siku ya kwanza aliyofanyiwa majaribio, alifuzu na kupewa nafasi ya kuigiza.Alisema siku hiyo, alimsindikiza rafiki yake kwenda kufanya majaribio, lakini hakufaulu. Alisema wakati
wakitaka kuondoka, rafiki yake huyo alimtaka ajaribu bahati hiyo na kujikuta akifanikiwa.

Pamoja na kufaulu kwake, Omotola alisema familia yake haikuvutiwa na fani hiyo kutokana na
kuheshimika kanisani. Alisema mama yake hakumruhusu kirahisi kujitosa kwenye fani hiyo. Wakati huo, Omotola alikuwa na umri wa miaka 16.

“Mmoja wa majirani zetu ndiye aliyekwenda kwa mama na kumshawishi aniruhusu nijitose kwenye fani hiyo na kumuahidi atahakikisha hakuna kibaya kitakachonitokea,”alisema.

Omotola alisema msimamo wake kwa sasa ni kutocheza filamu holela kwa sababu inapotokea kuwa mbaya, mashabiki hawamtazami mtayarishaji, mhariri au muongozaji. Macho yao huwa kwa waigizaji.

Alisema hali hiyo ndiyo iliyomfanya awe mwangalifu na watayarishaji wa filamu na kujaribu kucheza zile ambazo kiwango chake ni cha juu. Alisema kama nzuri, hayuko tayari kuicheza.

“Wapo baadhi ya waigizaji wenzangu waliochukua uamuzi huo pia na naona fahari juu yao. Ni vigumu, lakini tunapaswa kufanya hivyo, kuongeza kiwango cha filamu zetu,”alisema.

Mwanadada huyo amekanusha madai kuwa, ana uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji Jim Iyke na kwamba wamekuwa wakisafiri mara kwa mara nje ya nchi. Alisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote.

Alisema binafsi hazipi uzito tuhuma za aina hiyo kwa sababu zimelenga kumwangusha kiusanii.
Alisema haelewi ni faida zipi wanazozipata watu wa aina hiyo.Lakini alikiri kuwa, tuhuma za ana hiyo zinawachafua kwa vile baadhi ya mashabiki huziamini.

Alisema inauma kuona mtu anafanyakazi kwa bidii, lakini mtu mwingine anatokea kusikojulikana na kutaka kumwangusha.

Omotola alikiri pia kuwa, ni kawaida ya wanaume kumtongoza kutokana na mwonekano wake, lakini mara wanapogundua yeye ni mtu wa aina gani, hushindwa kuendelea kufanya hivyo.

Mwigizaji huyo alisema kutingwa kwake na kazi hakumkoseshi nafasi ya kuwa pamoja na familia yake. Alisema yeye na mumewe wameifanya siku ya Jumapili kuwa maalumu kwa familia na kila mwaka wametenga siku maalumu za mapumziko, ambapo huzima simu zao na kutumia muda mwingi kuwa na watoto wao.

Alikiri pia kuwa, mafanikio yake kiusanii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wake wa kuolewa mapema. Alisema kwa wengine, ndoa ni kikwazo kikubwa kwao, lakini kwake ndoa ni uhuru.

“Mama yangu ananiunga mkono kwa kila ninachokifanya. Nina uhuru wa kufanya chochote
ninachochagua,”alisema.

Omotola ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu. Alizaliwa Lagos. Baba yake anatoka katika Jimbo la Ondo wakati mama yake anatoka Abeokuta Jimbo la Ogun.Baba yake alikuwa meneja wa klabu ya Country Ikeja ya mjini Lagos wakati mama yake alikuwa
mfanyabiashara. Baba yake alifariki mwaka 1999 wakati Omotola alipokuwa akisoma shule ya
sekondari. Mama yake alifariki mwaka 2001.

No comments:

Post a Comment