KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

AY, Ali Kiba waongoza tuzo za Museke


KWAMBA muziki wa kizazi kipya nchini unazidi kuchukua chati kimataifa, hilo halina ubishi. Hii imetokana na wasanii wengi wa muziki za Bongo Fleva nchini kuteuliwa kuwania tuzo za muziki za Museke.
Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo wiki hii imeonyesha kuwa, katika kila tuzo, yupo msanii mmoja ama wawili wa Tanzania walioteuliwa kuziwania.
Katika tuzo ya mwanamuziki bora wa mwaka, yupo msanii Ambwene Yesaya, maarufu kwa jina la AY. Ameteuliwa kuwania tuzo hiyo na Barbara Kanam na Fally Ipupa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Darey na Wande Coal wa Nigeria, HHP wa Afrika Kusini na Lizha James wa Msumbini.
AY pia ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanamuziki bora wa kiume wa mwaka akiwa na Ali Kiba. Wasanii wengine walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ni Sarey, Ipupa, HHP, Wande na Ralph Anselmo wa Angola.
Kiba pia ameteuliwa kuwania tuzo ya albamu bora kupitia albamu yake ya Ali K 4 Real, sanjari na Blu3 wa Uganda, Samini wa Ghana, Sauti Sol wa Kenya, Anselmo na Wande Coal.
Mtayarishaji nyota wa muziki, Hermy B ameteuliwa kuwania tuzo ya mtengenezaji midundo bora sanjari na Bue d beats wa Angola, Culoe de Song wa Afrika Kusini, Don Jazzy wa Nigeria, Ogopa DJs wa Kenya na Richie wa Uganda.
AY yumo pia kwenye tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop kupitia kibao chake cha Leo. Anawania tuzo hiyo na Sarkodie wa Ghana, Dama do Bling wa Msumbiji, STL wa Kenya, HHP wa Afrika Kusini, Navio wa Uganda na MI wa Nigeria.
Mkali wa nyimbo za Injili nchini, Rose Muhando, ameteuliwa kuwania tuzo ya wimbo bora wa miondoko hiyo, kupitia kibao chake cha Nibebe, sanjari na Noelie wa Togo, Midnight Crew wa Nigeria, Wilson Bugembe wa Uganda, Kefee wa Nigeria, Joyous Celebration wa Afrika Kusini na Makoma wa Congo.
Kiba na Lady JayDee pia wameteuliwa kuwania tuzo ya wimbo bora wa miondoko ya Afro kupitia vibao vyao vya Msiniseme na Natamani kuwa Malaika wakati AY na Marlaw wameteuliwa kuwania tuzo ya wimbo bora wa mwaka wa Afrika Mashariki kupitia vibao vyao vya Leo na Piiii Piiii.

No comments:

Post a Comment