KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Simba yapania kuwang'oa Wamisri

KLABU ya Simba imetamba kuwa, inao uwezo wa kuing’oa Haras El-Hadood ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kocha Msaidizi wa Simba, Amri Said alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, ushindi walioupata katika mechi ya awali, ni kichocheo kikubwa kwao kusonga mbele.
Katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba iliichapa El-Hadood mabao 2-1.
Kufuatia ushindi huo, ili isonge mbele katika michuano hiyo, Simba sasa itahitaji sare ya aina yoyote wakati timu hizo zitakaporudiana wiki mbili baadaye mjini Alexandria.
Amri, ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Jaap Stam’ alisema, kikosi chake kimepania kuweka rekodi ya kuzitoa klabu za Misri katika michuano ya Afrika kwa mara ya pili.
Simba iliweka rekodi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2003 wakati ilipoishinda Zamalek kwa penalti 3-2 mjini Cairo baada ya matokeo ya jumla kati ya timu hizo kuwa sare ya bao 1-1.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara pia wanajivunia rekodi ya kuwa timu pekee nchini kuzishinda timu za Misri katika michuano hiyo. Iliwahi kuifunga Al Ahly mabao 2-1 mjini Mwanza mwaka 1984 kabla ya kuzifunga Ismailia bao 1-0 na Arab Contractors mabao 3-1 mjini Dar es Salaam.
Amri alisema Kocha Patrick Phiri amepanga kutumia muda wa siku 10 kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika mechi ya awali. Timu hiyo ilitarajiwa kuondoka nchini jana kwenda Oman kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.
"Tulichokigundua ni kwamba, wapinzani wetu wanatumia mchezo wa pasi fupi na kupiga mipira ya kushtukiza, kwa hiyo tutahakikisha tunawapa mafunzo maalumu wachezaji wetu ili kuwadhibiti,”alisema.
Katika mechi ya awali, Simba iliwakosa viungo wake mahiri, Hillary Echessa, aliyekuwa na kadi mbili za njano na Mohamed Banka, ambaye alikuwa mgonjwa.
Kwa mujibu wa Amri, wachezaji hao wataichezea Simba kwenye mechi ya marudiano na hivyo kuiongezea nguvu kwa vile wapinzani wao hawawafahamu vyema.

No comments:

Post a Comment