KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

DALILI ZA UBINGWA SIMBA ZILIANZA MAPEMA

NAHODHA wa Simba, Nico Nyagawa (kushoto) na beki Juma Jabu wakifurahia kombe la ubingwa wa ligi kuu ya Bara
WACHEZAJI wa Simba wakishangilia baada ya kuifunga Yanga

TIMU kongwe ya soka nchini, Simba msimu huu imeweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom kabla haijamalizika baada ya kuwa na idadi kubwa ya pointi, ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine.
Simba iliweka rekodi hiyo baada ya kuichapa Azam FC mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Machi 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliiwezesha Simba kufikisha pointi 56, ambazo hakuna timu nyingine inayoweza kuzifikia katika ligi hiyo. Jumla ya timu 12 zinashiriki katika ligi ya msimu huu.
Mbali na kutwaa ubingwa mapema, Simba pia iliweka rekodi ya kutofungwa hata mechi moja katika mechi 21 ilizocheza hadi sasa. Mabingwa hao wa soka Tanzania Bara, walitarajiwa kucheza mechi ya mwisho jana dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Mafanikio ya Simba msimu huu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafunzo mazuri kutoka kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri kutoka Zambia. Phiri pia aliiwezesha Simba kutwaa taji hilo mwaka 2006 na 2007.
Dalili za mafanikio kwa Simba zilianza kujionyesha katika mechi zake za mwanzo, ambapo iliichapa Majimaji mabao 2-0 mjini Songea kabla ya kuilaza Prisons bao 1-0 mjini Mbeya.
Simba iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuichapa Toto African mabao 3-1 mjini Dar es Salaam, iliilaza Kagera Sugar mabao 2-0 mjini Dar es Salaam kabla ya kuishindilia Manyema mabao 2-0 kwenye uwanja huo.
Miamba hiyo ya soka nchini iliendelea kuwapa raha mashabiki wake baada ya kuichapa Moro United mabao 2-1 mjini Dar es Salaam, iliichapa African Lyon bao 1-0 mjini Dar es Salaam kabla ya kuipa kipigo cha mwaka JKT Ruvu kwa kuicharaza mabao 4-1 kwenye uwanja huo.
Simba pia iliichapa Azam FC bao 1-0, ikaichapa Yanga idadi hiyo ya bao kabla ya kuibamiza Mtibwa Sugar mabao 3-1. Mechi hizo zote tatu zilichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuiwezesha Simba kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kushinda mechi zote 11.
Katika mechi za mzunguko wa pili, Simba iliichapa Majimaji mabao 2-0, iliicharaza Prisons mabao 3-1, iliilaza Toto African mabao 2-0 lakini ikakwaa kisiki kwa Kagera Sugar baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1 mjini Bukoba.
Mabingwa hao wa Bara waliichapa Manyema mabao 2-0, waliibamiza Moro United mabao 4-1 lakini wakakwaa kisiki kwa African Lyon baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Simba iliendeleza tena ubabe kwa kuichapa JKT Ruvu mabao 3-1, iliichapa Azam FC mabao 2-0 kabla ya kuwapa kichapo kingine watani wao wa jadi Yanga cha mabao 4-3.
Mbali na mafanikio hayo ya Simba kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mafunzo ya Phiri, pia yametokana na kujituma kwa wachezaji wake na kucheza kwa ushirikiano.
Baadhi ya wachezaji waliochangia mafanikio hayo ni kipa Juma Kaseja, aliyecheza mechi zote 21 na kuruhusu kufungwa mabao 12 na kiungo Mohamed Banka, ambaye alicheza mechi zote 11 za mzunguko wa kwanza.
Wachezaji wengine ni nahodha Nico Nyagawa, ambaye Phiri amekuwa akimpanga mara kwa mara kutokana na uwezo wake wa kukaba wachezaji wa timu pinzani na mabeki Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani na Juma Nyosso.
Kwa upande wa safu ya ushambuliaji, wachezaji waliochangia mafanikio hayo ya Simba ni Mussa Hassan ‘Mgosi’, Uhuru Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Mohamed Kijuso.
Lakini si rahisi kuzungumzia mafanikio hayo ya Simba bila ya kuwataja nyota wake kutoka nje ya nchi. Nyota hao ni beki Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda na kiungo Hillaly Echessa kutoka Kenya.
Kama kuna timu inayoweza kujivunia usajili wake wa wachezaji wa kigeni basi ni Simba. Wachezaji hao wamekuwa wakicheza kwa kujituma na kuthibitisha maana halisi ya soka ya kulipwa, tofauti na wageni waliosajiliwa na timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga aliwahi kutamka bayana baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kumalizika kuwa, kama kuna timu iliyosajili wachezaji halisi wa kulipwa, basi ni Simba.
Tenga alisema kujituma kwa wachezaji hao uwanjani, staili zao za uchezaji na ushirikiano waliouonyesha kwa wachezaji wenzao wa Simba ni baadhi tu ya mambo yaliyoiwezesha timu hiyo kufanya vizuri msimu huu.
Akizungumzia mafanikio ya timu hiyo msimu huu, Phiri alisema yametokana na wachezaji kuyashika vyema mafunzo yake na kuyafanyiakazi wanapokuwa uwanjani.
Phiri alisema amefurahi kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika na pia kuwa timu pekee, ambayo haijapoteza mechi hata moja.

No comments:

Post a Comment