KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, April 30, 2010

Wambura, Kaduguda watemwa kugombea Simba


YAMETIMIA. Hatimaye wanachama wawili mashuhuri katika klabu ya Simba, Michael Wambura na Mwina Kaduguda, wametupwa nje ya kinyang'anyiro cha kugombea uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Kuenguliwa kwa wagombea hao pamoja na wengine wawili, kulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Deogratias Lyatto.
Wambura alikuwa akigombea uenyekiti wa klabu hiyo, wakati Kaduguda alikuwa akiwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Kuenguliwa kwa Wambura kunaifanya nafasi ya mwenyekiti sasa kugombewa na watu watatu, Aden Rage ambaye pia aliwekewa pingamizi lakini ameshinda, Hassan Othman 'Hassanoo' na Andrew Tupa, wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti inabaki na mgombea mmoja tu, Geoffrey Nyange 'Kaburu'.
Mgombea mwingine wa nafasi ya mwenyekiti ambaye ameondolewa na kamati ya Lyatto, ni Zacharia Hanspope, na Chano Almasi aliyekuwa akitaka kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Uchaguzi wa klabu ya Simba utafanyika Mei 9 mwaka huu, katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay.
Akifafanua kuondolewa kwa Wambura, Lyatto alisema kamati yake ilikubaliana na uamuzi uliyotolewa na kamati za uchaguzi na rufani za TFF wa mwaka 2008,ambao ulionyesha mgombea huyo hakukidhi matakwa ya ibara ya 29 (7) ya katiba ya TFF na ibara ya 9 ya kanuni za uchaguzi wa wanachama wa shirikisho hilo, wakati alipowania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF.
"Hivyo kulingana na uamuzi uliotolewa na kamati hizo za rufani na uchaguzi za TFF, kamati yangu imemwondoa mgombea huyo," alisema.
Wakati huo Wambura aliondolewa kwa kigezo cha kutokidhi kipengele kinachohusiana na uaminifu.
Akimzungumzia Kaduguda, aliyewekewa pingamizi na mwanachama Asha Kigundula, alisema kamati imebaini hakutimiza wajibu kulingana na katiba ya Simba, ibara ya 19, kifungu namba 3,4,5,6,7,8 na ibara ya 21 kifungu f,g,h,i na ibara ya 38 kifungu namba 4,5,6 na 7.
"Baada ya kupitia pingamizi hiyo ya Asha, kamati imeridhika kuwa Kaduguda ameshindwa kukidhi matakwa ya kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF, ibara ya 9. Hivyo kamati imemwondoa mgombea kwenye mchakato," alisema.
Lyatto alisema Chano Almasi ambaye pia aliwekewa pingamizi na Asha, kamati yake imebaini na kuridhika kuwa mgombea huyo hakutimiza wajibu wake kulingana na katiba ya Simba ibara ya 19 kifungu namba 3,4,6,7 na 8 na ibara ya 21 kifungu g na i.
Alisema kamati pia imebaini mkanganyiko wa majina ya mwombaji huyo katika vyeti vyake vya elimu na hati zingine, na alitoa mfano kuwa katika maelezo yake binafsi ametumia jina la Karaha Hassani Almasi Chano, wakati kwenye kadi ya uanachama wa Simba imeandikwa Chano K.H. Almasi.
"Hivyo kwa kutotimiza wajibu wake kulingana na matakwa ya katiba ya Simba na mkanganyiko huo wa majina, hakika umeitia dosari fomu ya mgombea na amekosa sifa ya kuwa mmoja wa wagombea," alisema.
Lyatto alisema kuenguliwa kwa Hanspope, ambaye alikuwa amewekewa pingamizi na Issa Ruchaki, baada ya kubaini kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF ibara ya 25(2).
Alisema kamati yake imebaini kamati ya uchaguzi ya Simba ilifanya makosa kutumia ibara ya 45 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila ya kuzingatia katiba ya klabu hiyo ibara ya 26(5) kwa kumpitisha mwombaji asiyekidhi matakwa ya kifungu hicho.
Lyatto alisema uamuzi huo umefanywa baada ya kuridhika kuwa wagombea hao wana upungufu unaowanyima nafasi ya kuwania uongozi, na si kwa lengo la kumuharibia yeyote ila kwa kuzingatia kanuni na taratibu kuhusiana na pingamizi zilizowekwa.
"Huo ni uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ambayo kulingana na katiba ya shirikisho, bado wagombea wana haki ya kupinga uamuzi huo kwa Kamati ya Rufani ya TFF, endapo aliyeenguliwa haridhiki na uamuzi uliotolewa," alisema.
Hata hivyo, imedaiwa kuwa kitendo cha kuenguliwa wagombea hao kimezua minong'ono kwa baadhi ya walioenguliwa, na wanachama, na kuzusha tetesi kuwa kuna uwezekano wa wanachama au waliongeliwa wakalipeleka suala hilo mahakakamani.

No comments:

Post a Comment