KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Kutana na Preta wa Shades of Sin


KWA mashabiki wa tamthilia hapa nchini, jina la Preta de Souza si geni kwao. Ni mmoja wa waigizaji wenye mvuto na walioipamba vyema tamthilia ya Shades of Sin, inayoendelea kuonyeshwa kupitia kituo cha televisheni cha ITV.
Ni msichana mwenye sura na umbo lenye mvuto, aliyezaliwa Maranhao. Ni msichana mwenye tabia nzuri, anayejiamini na mwenye msimamo wa aina wa pekee katika maisha yake.
Preta, ambaye jina lake halisi ni Taís Bianca Gama de Araújo, alizaliwa na kulelewa na mama yake, Dona Lita. Kamwe hakuwahi kukutana na baba yake.
Licha ya kumbukumbu ya maisha duni, aliyoishi na mama yake, siku zote amekuwa ni mtu mwenye njozi njema katika maisha yake na amekuwa akifanyakazi kwa bidii kwa lengo la kufanikisha azma yake.
Tangu akiwa mdodo, Preta amekuwa akimsaidia mama yake kuuza dawa mbalimbali zitokanazo na mitishamba katika mji mdogo wa Sao Luis uliopo Maranhao.
Kila alipokuwa hana kazi ya kufanya, Preta alipendelea sana kucheza muziki wa dansi wa miondoko ya tambor de crioula, ambao asili yake ni nchini Brazil, akiwa na rafiki zake. Wakati mwingine alipendelea kwenda matembezini akiwa na rafiki yake, Helinho.
Kama ilivyokuwa kwa Paco, Preta hakuwahi kujitosa kimapenzi kwa mwanaume yeyote. Alikuwa na urafiki wa kawaida na Dodo, kijana mwenye kipaji cha fani ya muziki.
Wakati Paco alipofika Sao Luis, ndipo Preta alipojihisi na kuwa na uhakika kwamba ndiye mwanaume pekee aliyemuingia moyoni mwake. Alimuona kuwa ndiye mwanaume pekee anayemfaa maishani mwake.
Binti huyo mwenye haiba yenye mvuto, alilazimika kwenda kinyume na usia wa mama yake, ambaye hakuwa akimwamini kijana huyo. Aliamua kuliamini penzi la Paco. Hata hivyo, Preta anahujumiwa na Barbara, mwanamke mwenye tabia chafu na ambaye alikuwa anataka kumtumia Paco ili kuchuma utajiri wa baba yake, Afonso. Barabara anatumia kila njia kumtenganisha Preta na Paco.
Njama hizo za Barbara zinafanikiwa. Na wakati Paco akitengana na Preta, binti huyo alikuwa tayari na uja uzito kabla ya kujifungua mtoto wa kiume, Rai.
Preta anapata taarifa za kifo cha Paco akiwa kwenye gari, anarejea Maranhao kutoka mjini Rio de Janeiro. Anapatwa na huzuni kubwa.
Anaamua kumtunza Rai kwa msaada mkubwa wa mama yake pamoja na swahiba wake mkubwa, Helinho bila kufanya jitihada zozote za kuitafuta familia ya Paco.
Ni pale anapoamua kwenda mjini kuisaka familia ya Paco, ndipo Preta anapokutana na masahibu mazito, yanayomfanya aishi maisha yaliyojaa woga na mashaka mazito.
Barbara, mchumba wa zamani wa Paco, aliyejifanya kuzaa na kijana huyo, ndiye anayeongoza mashambulizi hayo dhidi ya Preta kwa kushirikiana na Tony, mmoja wa wafanyakazi katika kampuni ya Afonso.
Tony na Barbara wanafanikiwa kumfanya Rai aonekane kuwa si mjukuu wa Afonso kwa kubadili vipimo vya DNA. Pia wanamuhusisha Preta na utapeli wa kuuza fomula, inayomilikiwa na Afonso kwa kumtumia mmoja wa wafanyakazi waaminifu wa mzee huyo.
Mbaya zaidi, Afonso anamuasili Rai kwa kutumia nguvu kutokana na kumpenda sana kijana huyo. Siku zote Afonso amekuwa akimlinganisha Rai na Paco alipokuwa mdogo.
Hata hivyo, mbinu hiyo chafu ya kuuza fomula inakuja kubainika baada ya mfanyakazi huyo wa Afonso kukiri kosa hilo mbele ya Preta na kwa mzee huyo. Ni kuanzia wakati huo, Afonso anaanza kurejesha imani kwa Preta. Kujitokeza kwa Paco baada ya kugundua kwamba Rai ni mtoto wake halali, aliyezaa na Preta, ndiko kunakohitimisha tamthilia hii. Paco anagundua kwamba Preta si laghai kama alivyokuwa akimfikiria. Safari hii anajitokeza kama Paco na si Apollo.
Preta alizaliwa Novemba 25, 1978 mjini Rio de Janeiro. Ni mmoja wa waigizaji filamu wenye mvuto nchini Brazil, akiwa Mbrazil wa kwanza mweusi kuigiza tamthilia ya Xica da Silva mwaka 1996. Pia alishiriki kucheza tamthilia ya Da Cor do Pecado mwaka 2004. Binti huyo pia alikuwa mwigizaji mkuu katika tamthilia ya Viver a Vida.
“Nilipokuwa mdogo, sikuwa na kitu chochote kilicholinganishwa na mimi. Sasa msichana mweusi anavyo vitu vingi vya kulinganishwa naye kwenye TV, yakiwemo masuala ya urembo,”alisema Preta alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni cha Brazil.
Mbali na kushiriki kucheza tamthilia na filamu nyingi, mwigizaji huyo wa kike pia ameshinda tuzo nyingi kutokana na uigizaji wake maridhawa.
Baadhi ya filamu alizoshiriki kuzicheza ni pamoja na A Guerra dos Rocha, O Maior Amor do Mundo, Nzinga, As Filhas do Vento, Cida, Garrincha, Caminho dos Sonhos na Drama Urbano.

No comments:

Post a Comment