'
Monday, April 19, 2010
DOGO INNO: Muziki utanikomboa
MAISHA ni safari ndefu kwa maana lazima mtu apite katika hatua mbalimbali hadi kufikia malengo aliyojiwekea.
Ni wachache, ambao hawakuvuka mito na kupanda milima au mabonde, lakini asilimia kubwa
wamepitia huko na kamwe hawasiti kusema ukweli, iwe wamefanikiwa au la.
Innocent Magawa a.k.a Dogo Inno ni miongoni mwa waliopita katika adha tofauti za maisha kwa
sababu ameyapigania kwa hali na mali hadi kufikia hatua alinayo sasa ya kukaribia kuzindua albamu yake ya kwanza baada ya kutumbukia katika muziki miaka kadhaa iliyopita.
Japokuwa Dogo Inno hajafanikiwa kuwa msanii mashuhuri katika muziki wa kizazi kipya, kwa hatua aliyofikia ni kubwa ikilinganishwa na alikotokea kama mwenyewe anavyobainisha: “Mimi ni yatima, ambaye sina baba wala mama, wazazi wangu walifariki kwa ugonjwa wa ukimwi mkoani Dodoma na baada ya wao kufa, mimi na wadogo zangu tuliteseka sana,” anasema Dogo Inno aliyezaliwa miaka 25.
Msanii huyo chipukizi alizaliwa kwenye kijiji cha Mundemu kilichopo jirani na wilaya ya Kondoa,
Dodoma, ambako mama yake mzazi alikuwa anafanya kazi ya uuguzi katika zahanati ya kijiji hicho na baadaye alihamishiwa hospitali ya mkoa.
“Darasa la kwanza hadi la saba nilisoma shule ya Mundemu na mwaka 2000 mama alipohamishiwa kikazi Dodoma Mjini, nilijiunga na shule ya Sekondari ya Central Dodoma na nikaishia kidato cha pili baada ya yeye kufariki dunia,” anaeleza Dogo Inno.
Amesema kufariki kwa mama yake kulimpa wakati mgumu yeye na wadogo zake na hivyo bibi yao kwa upande wa mama aliamua kuwachukua na kurudi nao kijijini Mvumi, ambako aliishi hadi mwaka 2004 aliporudi tena shule.
“Wakati tulipokuwa kijijini Mvumi, kuna shule inaitwa DCT ambayo mkuu wake alikuwa mzungu, ambaye alitangaza watoto yatima tukasome pale na mimi ikawa rahisi kuanza tena masomo, lakini kabla ya kufika kidato cha tatu, nikafukuzwa alipokuja mkuu mwingine wa shule,” anasema Dogo Inno.
Amefafanua kwamba, mkuu huyo alipofika shuleni alichunguza na kugundua kuna watoto wengine hawakuwa yatima ndipo akatembeza fagio kwa wanafunzi 20 na kubakisha nusu ya idadi hiyo, ambapo Dogo Inno naye aliondolewa licha ya kujitetea kuwa yeye ni yatima.
“Kweli mimi ni yatima kwani baada ya mama kufariki na baba naye alifuata siku chache na yeye
hakuwa anatulea, mama yangu alikuwa mwanamke wake wa nje na kila tulipokwenda kwa ndugu zake, (baba) walikuwa wanatukataa na kibaya mama alizaliwa peke yake,” anabainisha msanii huyo.
Wahenga wanasema shida kipimo cha akili kwani baada ya kufukuzwa shule, Dogo Inno alianza
kwenda kituo cha mabasi yaendayo mikoani, ambako alikuwa anabeba mizigo na kulipwa ujira mdogo, lakini baadaye aliajiriwa na Kampuni ya CRG inayomilikiwa na Wachina na kuwa anapaka rangi kwenye jengo la Bunge.
Amesema kupitia kazi hiyo, alipata pesa zilizomwezesha kuingia studio na kurekodi nyimbo
mbalimbali, ambapo hakuweza kutamba na hivyo mwaka 2008 akaamua akimbilie Dar es Salaam kwa nia ya kutafuta maisha zaidi.
“Nikiwa Dar es Salaam, niliteseka, sikuwa na pa kulala hadi dereva teksi mmoja akanichukua na
kunipeleka nyumbani kwake Mbezi Beach, ambako naishi hadi sasa,” anaeleza Inno.
Amesema baada ya kufanikiwa kupata ‘hifadhi’ kwa msamaria mwema huyo, aliamua kujikita kwenye muziki kwa kwenda katika matamasha ya wasanii wa bongo fleva na alibahatika kukutana na Rugemalila Mutahaba, ambaye ni miongoni mwa mabosi wa radio Clouds FM na kumuomba amsaidie kukuza kipaji chake.
Msaada aliotoa Ruge kwa Dogo Inno ni kumpeleka katika kundi analoliongoza la Tanzania House of Talents (THT), na hapo msanii huyo akaanza kucheza na kuimba na hadi sasa amefanikiwa kutunga nyimbo nane kwa ajili ya kutoa albamu yake binafsi.
Kwa mujibu wa msanii huyo, albamu hiyo inayoitwa ‘Yatima’ ina mkusanyiko wa nyimbo nane, ambazo 'Ni wewe’,‘Nakuita’,‘Dodoma’,‘Nimeathirika’, ‘Tunapari’, ‘Maisha mapambano’, ‘Vumilia’ na ‘Iko siku’.
Baadhi ya nyimbo hizo amerekodi katika studio za MJ Records, Mass Records na 41 Records, ambapo gharama zote zimelipwa na THT, kundi ambalo msanii huyo amesema ana mkataba nalo wa kufanya kazi na iwapo atafanikiwa, kuna asilimia atakayokatwa ili kufidia pesa hizo.
“Bado kuna vitu vidogo namalizia ndipo nitoe albamu yote, lakini sasa hivi wimbo wa ‘Tunapari’ ambao nimemshirikisha msanii Diamond umeanza kuchezwa katika vituo vya redio na Clouds FM ndiyo ilikuwa ya kwanza kuutambulisha,” anasema Dogo Inno.
Amesema kuwa haogopi ushindani uliopo katika muziki kwa sababu ana vipaji lukuki vya kuhimili vishindo. “Naweza kucheza filamu, kutunga hadithi, kuimba, kucheza na kila kitu,” anatamba Dogo Inno.
Msanii huyo ana imani kuwa atafanikiwa kupitia muziki na dhamira yake kubwa ni kupanga chumba ili aanze kujitegemea na kujiendeleza kimaisha kwa kutegemea sanaa. Alianza kuandaa albamu hiyo mwaka 2008 na sasa imekamilika.
Huyo ndiye Dogo Inno mwenye matarajio kibao ya kuchomoza kwenye fani ya muziki wa R&B na
kuwafunika wakali wanaotamba sasa kwenye bongo fleva.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment