KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

Kipa wa Tottenham anusurika kufa



LONDON, England
KIPA wa Tottenham Hotspur, Carlo Cudicini amekumbana na ajali, ambayo almanusura iangamize roho yake.
Pikipiki aliyokuwa anaendesha iligongwa na gari aina ya Ford Fiesta na kusababisha aumie. Alipodondoka kichwa chake chupu chupu kikanyagwe na gari na cha kushukuru hakufa katika ajali hiyo ya kutisha.
Baada ya kugongwa, alianguka kwenye barabara iliyokuwa imesambaa barafu, na kuugulia maumivu yaliyomtia wasiwasi wa kupooza.
Ghafla alijikuta anakuwa kama mwehu na kujiuliza maswali mengi kama shingo yake inacheza, vidole gumba vinafanya kazi, wapi alipoumia na kama huo ulikuwa mwisho wake wa kucheza soka?
“Ni kitu kilichotokea ghafla,” anasema kipa huyo wa Tottenham alipozungumza hadharani kwa mara ya kwanza kuhusu ajali iliyotokea barabara ya Forest mjini Walthamstow miezi miwili iliyopita.
Cudicini anasema polisi wanachunguza chanzo cha ajali hiyo.
“Kama dakika moja hivi nilikuwa njiani kwenda mazoezini na hatua iliyofuata, nilipakiwa katika gari la wagonjwa (ambulance) na kupelekwa hospitali. Lakini nakumbuka kila hatua hadi kutokea ajali hiyo. Nakumbuka kitu kilichotokea.
"Ilitokea kwa sekunde, lakini nakumbuka ajali ilivyokuwa inatishia uhai, hakika nakumbuka nilivyolala uwanjani. Sikupoteza fahamu.
“Kitu cha kwanza nilichofanya ni kuchunguza mwili kujua kama niliumia mgongo, miguu, nimepooza na kila kitu.
“Nilihisi maumivu kwenye viganja na mbavu zangu. Lakini presha kubwa ilikuwa kama nimeumia kiasi gani. Kama umeteguka mguu, unaweza kubaini. Hata hivyo, si kwa maumivu ya ndani. Nilisubiri hadi nilipofika hospitali.”
Amesema kuwa, alipakizwa katika gari hilo la wagonjwa akiwa amekaa nyuma na mtu mmoja.
“Ndani ya sekunde kadhaa alikuwa pamoja nami, amenishika mkono na kunituliza,” anasema Cudicini. “Hakunijua kwa kingine zaidi. Kichwani bado nilikuwa na helmeti.
“Lakini wakati jamaa wanafika na gari la wagonjwa na maofisa wa polisi, walinivua helmeti na niliwaambia mimi ni mwanasoka wa kulipwa na wampigie simu daktari wa klabu.”
Mtumishi wa gari la wagonjwa la London, amesema kipa huyo alikuwa ameumia sana.
Cudicini alipatwa na maumivu makali kabla ya kuanza kuwaza nini kitajiri. Alijiuliza kama ameumia sana na kugundua kuwa, hawezi kufa isipokuwa alijiuliza juu ya hatima yake ya soka.
Hakuwa na jibu. Alitishwa na upasuaji aliofanyiwa wa kutolewa nati zilizonasa mgongoni mwake. Alibaki na wasiwasi kuwa hataweza kurejea katika hali yake ya kawaida hasa alipotazama kiganja chake cha kulia, ambapo alikamilisha tiba kwa kufungwa sahani ya bati.
Katika siku za karibuni, amekuwa anaendelea vizuri na ana matumaini atapona, na kueleza jinsi upasuaji huo ulivyofanyika kwa mafanikio.Amesema tatizo kubwa, ambalo lilimsumbua ni wasiwasi na si kitu kingine.
“Sikudhani kama walikuwa na presha kuhusu kupona kwangu, lakini kwa sababu ni kipa, kiganja changu kiliumia sana na hapo ndipo ilipokuwepo hofu, kwa kuzingatia nilihitaji kupona kwa vile nilikitegemea kwa kazi yangu,"alisema.
Gudicini anasema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na kila anayekwenda kumjulia hali, anaridhika naye, ingawa kiganja cha kulia bado kinamuuma, lakini ana matumaini kitapona muda si mrefu.
“Dhumuni langu haswa ni kupona na kucheza tena mpira, tegemeo langu lote lipo hapo, nitajaribu kufanya vizuri na kurudi katika kiwango nilichokuwa nacho,” alisema.
Kipa huyo amesema hataki kujadili hatima yake kisheria na anamshukuru Mungu kwa kuwa hai.
Amevutiwa na salamu alizotumiwa na familia, marafiki na jamaa zake kwa njia ya barua pepe na barua za kawaida, ambapo anasema zimempa moyo naye amewataka wasikate tamaa.
Watu wanaomuhudumia ni mama yake, ambaye ametoka Milan, Italia na kukaa naye hospitalini mwezi mmoja, golikipa nambari moja wa Chelsea, Petr Cech na kocha wake, Harry Redknapp.
“Hii ni changamoto, ambayo sijawahi kukutana nayo maishani mwangu,” anasema Cudicini.
“Ni kitu kinachotisha, ambacho hakijawahi kunitokea, najua nakabiliana na hali ngumu.
"Majeraha siku zote ni kitu kibaya. Inabidi kufanya mazoezi kila siku, kujiweka fiti kwa mechi ni ngumu kidogo," alisema.
Madaktari wamemweleza Gudicini kuwa, atapona baada ya miezi minne badala ya miwili na mguu wake wa kulia umeanza kupata nafuu kwa asilimia 70 kwa kuhimili uzito wa mwili wake.
Kipa huyo alipata ajali Novemba 12 mwaka jana huko Walthamstow, kaskazini mwa London.
Pikipiki yake aina ya BMW ililigonga gari lililokuwa linaendeshwa na mwanamke, aliyekuwa amempakia mtoto wake na licha ya mchezaji huyo kuumia, gari nalo liliharibika zaidi.
Mwanamke huyo alipelekwa hospitali na aliruhusiwa kuondoka siku hiyo hiyo baada ya kuchunguzwa na kukutwa hawajaumia.

No comments:

Post a Comment