KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

Jokha Kassim aingia mitini Five Stars Modern Taarab



MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Jokha Kassim ameamua kujiengua katika kundi la Five Stars Modern Taarab na kutulia nyumbani.

Jokha, mwimbaji mwenye sauti yenye mvuto, inayostarehesha na kuliwaza, amefikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa, uongozi wa kundi hilo umeshindwa kumlipa madai yake.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha C2C mwishoni mwa wiki iliyopita, Jokha alisema hataendelea kuimba katika kikundi hicho iwapo madai yake hayatalipwa.

“Kwa sasa nimeamua kukaa nyumbani na kutulia, sitajihusisha na muziki wa taarab,”alisema mwimbaji huyo, mke wa zamani wa kiongozi wa kikundi cha Jahazi, Mzee Yusuf.

“Unajua mahali popote panapokuwa na wingi wa watu, hasa wanawake, huwa hapakosi kutokea
matatizo, ndiyo sababu nimeamua kujiweka kando kwa sasa,”aliongeza.

Mwimbaji huyo mwenye sura ya mvuto na tabasamu la kuliwaza alisema, imani yake kwa uongozi wa kundi hilo ndiyo iliyomponza kwa vile aliwaamini viongozi kwamba watatekeleza ahadi walizomuahidi.

“Imani zinatuponza, kutuchongea na kugeuka matatizo,”alisisitiza. “Msanii kama anaonekana
anafanyakazi, alipwe haki zake anazostahili.”

Hata hivyo, Jokha hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha, anachodai kwa uongozi wa kundi hilo kwa madai kuwa hiyo ni siri baina ya pande hizo mbili.

Lakini uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, uamuzi wa Jokha kujiondoa kwenye kundi hilo umekuja baada ya msanii mwenzake nyota, Khadija Yusuf kulipwa fedha alizokuwa anadai kwa uongozi.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Khadija alilipwa pesa zake muda mrefu uliopita, lakini Jokha amekuwa akipewa ahadi za ‘tutakulipa kesho, keshokutwa’.

“Mimi sina tatizo na wasanii wenzangu, tatizo lipo kwa viongozi. Ni aina ya matatizo, ambayo
yamekuwa yakitokea sana kwenye jamii tunazoishi,”alisema.

Mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Zanzibar Stars alisema, iwapo uongozi utamlipa madai yake, atakuwa tayari kurejea na kuendelea kufanya nalo maonyesho.

“Unajua msanii yeyote anayeipenda kazi yake, huifanya kwa mapenzi na moyo wake wote, lakini wakati mwingine utakuta hathaminiwi. Anajitahidi kubuni vitu vizuri, lakini anakatishwa tamaa,”alisema.

Jokha amewataka viongozi wa vikundi vya taarab nchini, kuwathamini wasanii wao na kutekeleza kwa vitendo ahadi wanazowaahidi badala ya kuwaacha ‘kwenye mataa’.

Alisema tabia ya aina hiyo inachangia kuwakatisha tamaa wasanii wa muziki huo na hatimaye
kusababisha vikundi vingi kufifia ama kutoweka kabisa katika ulimwengu wa taarab.

Mmoja wa viongozi wa Five Stars Modern Taarab, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa ni kweli Jokha anadai fedha alizoahidiwa, lakini hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha.

“Ni kweli anaudai uongozi na suala lake linashughulikiwa, hivyo tunatarajia ataendelea na maonyesho ya Five Stars kama kawaida,”alisema.

Jokha alianza kuimba taarab mwaka 2002 katika kundi la Zanzibar Stars Modern Taarab kabla ya kujiunga na East African Melody. Alijiunga na kundi la Five Stars Modern Taarab mwaka jana, akiwa mmoja wa waanzilishi wake.

Aliwahi kuolewa na Mzee Yusuf mwaka 2000 na kuzaa naye mtoto mmoja wa kiume, anayejulikana kwa jina la Yusuf. Kwa sasa, hana mume.

No comments:

Post a Comment