KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

TFF: Ligi Kuu Bara imetufundisha mengi


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wake, Fredrick Mwakalebela.

Na Athanas Kazige
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema michuano ya ligi kuu ya Vodacom msimu huu ilikuwa mizuri na yenye ushindani, ikilinganishwa na ligi za miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema ligi hiyo imetoa mafunzo mengi kwa shirikisho lake kuhusu namna ya kuiboresha zaidi.
"Hii ligi ilikuwa nzuri na timu nyingi zilipania kufanya vizuri na tumejifunza mambo mengi, ikiwemo kubaini kasoro mbalimbali na tutahakikisha tunawabana waamuzi ili waweze kutenda haki katika michuano ya msimu ujao," alisema Mwakalebela.
Katibu Mkuu huyo wa TFF alisema moja ya kasoro kubwa zilizojitokeza katika ligi hiyo msimu huu ni kushindwa kwa waamuzi kuzitafsiri vyema sheria 17 za soka.
Alisema waamuzi wa aina hiyo wamekuwa kikwazo kwa maendeleo ya soka nchini kutokana na kuchezesha mechi kwa upendeleo au kwa kutojua sheria za mchezo huo.
“Ni kweli wapo baadhi ya waamuzi ambao kwa makusudi wamekuwa wakichezesha mechi kwa upendeleo na wengine wanashindwa kuzitafsiri vyema sheria za soka. Hili ni jambo baya katika soka na tutakuwa makini sana msimu ujao,”alisema.
Mwakalebela alisema katika kupambana na tatizo hilo, shirikisho lake limeamua kuanzisha kitengo maalumu cha kufuatilia nyendo za waamuzi pamoja na uchezeshaji wao ili kuwabaini wenye tabia hiyo chafu.
“Hatuwezi kukaa tu na kulalamikia uchezeshaji mbovu wa waamuzi wetu. Tumeamua kuchukua hatua na kwanza kuanzia, tumeanzisha kitengo hiki kwa ajili ya kudhibiti tabia hiyo,”alisema.
Alisema kitengo hicho kinaundwa na baadhi ya maofisa wa TFF, ambao watakuwa wakienda mikoani kutazama mechi za ligi bila kufahamika na waamuzi, makamisaa na klabu husika.
Mbali na kuunda kitengo hicho, Mwakalebela alisema wamekuwa wakizifanyia kazi kwa umakini ripoti za makamisaa kuhusu mechi mbalimbali na kuwachukulia hatua wahusika pale inapobainika kwamba hawakutenda haki.
Hata hivyo, Mwakalebela alikiri kuwa utekezaji wa kazi hizo ulikuwa mgumu msimu huu kutokana na baadhi ya watendaji kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Alisema ana imani kutakuwa na mabadiliko makubwa msimu ujao.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa, kazi ya kuwabaini waamuzi wabovu inafanyika bila kikwazo ili ligi iweze kuendeshwa kwa haki na washindi wapatikane kutokana na uwezo wao,”alisema.
Mwakalebela alisema umakini wa baadhi ya watendaji wao uliiwezesha TFF kuwafungia waamuzi kadhaa kwa makosa ya kupokea rushwa na kukiuka sheria za mchezo huo.
“Kama utakumbuka, tuliwafungia waamuzi wengi kwa makosa hayo na wengine waliondolewa kabisa kwenye ligi na hilo litaendelea hadi tutakapobaki na waamuzi wanaoheshimu na kufuata sheria,”alisema.
Mwakalebela alisema pia kuwa, shirikisho lake bado linaendelea na jitihada za kuzitafutia wadhamini timu zote zinazoshiriki kwenye ligi kuu ili ziweze kujiendesha bila matatizo.
Alisema kwa sasa, zipo baadhi ya timu, ambazo zinashiriki ligi hiyo katika mazingira magumu kutokana na kukabiliwa na ukata kwa vile fedha za udhamini zinazotolewa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, hazitoshi.
Timu pekee zenye udhamini katika ligi hiyo ni Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo imekuwa ikiwalipa mishahara wachezaji, makocha na watendaji wakuu.
Zingine ni Azam FC, inayodhaminiwa na Kampuni ya SSB na African Lyon, inayodhaminiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited.
"Lengo letu ni kuhakikisha tunashirikiana vyema na viongozi wa klabu za ligi kuu kusaka wadhamini ili waweze kuwalipa mishahara wachezaji na makocha na kupunguza gharama. Tunafahamu timu nyingi zina hali mbaya kifedha,"alisema kiongozi huyo.
Amewataka viongozi wa klabu za ligi kuu wasibweteke na kuitegemea TFF ifanye kazi hiyo, badala yake, wajitahidi kuzishawishi kampuni mbalimbali zizidhamini timu zao ili zipate nafasi ya kujitangaza kibiashara.
Hata hivyo, Mwakalebela amewaonya viongozi wa klabu hizo kuwa, wawe makini na udhamini watakaoupata na waweke wazi ripoti za mapato na matumizi ya klabu kila mwaka.
"Unajua hakuna mtu ambaye anapenda kutoa pesa yake bila ya kunufaika, lakini hapa jambo la msingi ni kwamba inabidi viongozi wa klabu waweke mazingira ya uwazi ili kuwavutia wafadhili,"alisema Katibu huyo ambaye anakaribia kumaliza mkataba wake ndani ya TFF.
Alisema kuwa viongozi wa klabu za ligi kuu wamekuwa wakipatwa na wakati mgumu kutokana na baadhi ya pesa wanazopewa na Vodacom kutokidhi mahitaji yao.
"Baadhi ya timu zina madeni mengi, hiyo yote ni kutokana na pesa zinazotolewa na Vodacom kushindwa kutosheleza mahitaji ya klabu kwa vile kuna gharama za usafiri na posho, hivyo tutajaribu kuwaomba wadhamini wafikirie jambo hilo,"alisema.
Kiongozi huyo wa TFF alisema pia kuwa, wamewaomba makocha wa timu za ligi kuu kuwatumia zaidi wachezaji wazalendo badala ya kusajili idadi kubwa ya wanasoka wa kigeni.
Alisema tabia ya baadhi ya timu kubwa kusajili wageni wengi, inawachukiza wanasoka wazalendo kwa sababu idadi kubwa ya wageni hao ni ‘bomu’ kutokana na uwezo wao kisoka kuwa mdogo.
Mwakalebela alisema Tanzania ina hazina kubwa ya wanasoka chipukizi wenye vipaji, lakini wanakosa nafasi ya kuonyesha uwezo wao kutokana na kutokuwepo utaratibu wa kusaka na kuibua vipaji vipya.
"Tunawaomba makocha wa ligi kuu, wajaribu kutumia mfumo wa zamani wa kusaka wachezaji kwenye michezo ya mitaani, wilayani na mikoani. Huko kuna wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo,"alisisitiza.
Alisema binafsi amefurahishwa kuona kuwa, wanasoka wa Tanzania ndio wanaoongoza katika kuwania tuzo ya mfungaji bora wa ligi kuu msimu huu, tofauti na misimu miwili iliyopita.
Wachezaji wanaowania tuzo hiyo ni Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba, anayeongoza kwa kufunga mabao 16, akifuatiwa na Mrisho Ngasa wa Yanga na John Boko wa Azam waliofunga mabao 14 kila mmoja.
Amezipongeza timu za Ruvu Shooting, Polisi Dodoma na AFC Arusha kwa kufuzu kucheza ligi kuu msimu ujao na kuzitaka zifanye usajili mzuri zaidi ili ziweze kutoa ushindani.
Alisema ana imani kubwa kwamba ligi ya msimu ujao itakuwa na msisimko na ushindani mkali kwa vile kila timu imejifunza mengi kutokana na ligi ya msimu huu.
Mwakalebela alisema hawatarajii iwapo mechi za ligi ya msimu ujao zitakuwa zikipanguliwa mara kwa mara kutokana na kuingiliana na michuano ya kimataifa. Alisema watahakikisha wanapanga ratiba kulingana na michuano hiyo ili kuepuka malalamiko.
000000

No comments:

Post a Comment