KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

NADIA BUARI: Michael Essien mpenzi wangu



ACCRA, Ghana
MWIGIZAJI nyota wa filamu, raia wa Ghana, Nadia Buari amekiri kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mwanasoka mahiri wa nchi hiyo na klabu ya Chelsea ya England, Michael Essien.
Akijibu swali la mtangazaji Kwame Sefa Kayi wa kipindi cha televisheni cha ‘Velvet Life’ chaneli 3 kuwa ana uhusiano na msukuma ndinga huyo, Nadia alisema Essien ni mpenzi wake, kauli iliyopokewa kwa shangwe kubwa na watazamaji wa kipindi hicho waliokuwa studio kumsikiliza nyota huyo wa filamu.
Essien, aliyeshindwa kung’ara katika fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu baada ya kuumia na kuondolewa mapema kwenye kikosi cha Black Stars na Nadia, kwa muda mrefu walikuwa wagumu kuweka wazi juu ya uhusiano wao wa kimapenzi.
Wawili hao walikuwa wagumu kuthibitisha uhusiano huo licha ya kuwepo uvumi mkubwa kuwa ni wapenzi. Mara kadhaa wamekuwa wakipigwa picha wakiwa pamoja katika matukio mbalimbali kama ya wiki ya mavazi nchini Ghana, matamasha ya muziki na filamu.
Ingawa kutoonekana pamoja katika siku za karibuni kunadhaniwa kumetokana na kufifia kwa uhusiano wao, inaelezwa kukiri kwa Nadia kuwa ni kidosho wa Essien kumechelewa, kufuatia kuibuka uvumi mwingine mbaya juu yao.
Fununu hizo zinadai kuwa, nyota hao wamepigana kibuti ndiyo maana hawajaonekana wakiwa pamoja muda mrefu, lakini wadadisi wa mambo wanadai hali hiyo inatokana na Nadia kutingwa na shughuli ya kucheza filamu huku Essien akiuguza goti, ambalo aliumia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Libya.
Katika siku za karibuni, Essien pamoja na Ashley Cole walikuwa Paris, Ufaransa kutibiwa majeraha yaliyokuwa yanawasumbua, ambapo kuwepo taarifa rasmi kuwa mwanandinga huyo na Nadia ni wapenzi, kumepongezwa na nyota wengi wa Ghana.
Nadia katika kudhihirisha kuwa hajapigana chini na mchezaji huyo, alipiga simu katika ofisi za gazeti la Flex na kukanusha taarifa ya kuachana na mpenzi wake.
Akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hilo alisema: "Uvumi huu umekuwepo kwa muda mrefu sasa, sijui nani ameusambaza, lakini hatujaachana, ukweli huo ni uwongo, bado tuko pamoja na hatuna tatizo lolote.
"Gazeti la Flex limedai kugundua wapenzi hao wameachana baada ya Essien kumpokonya laazizi wake magari saba aliyomnunulia wakati mahaba yao yalipokuwa moto, huku kukiwepo na madai kuwa kiungo huyo anajiandaa kurudiana na mke wake wa zamani, Dela Ackumey.Essien alimuacha Dela baada ya kunasa kwa Nadia na uamuzi wake huo ulimweka katika wakatimgumu baada ya kuburuzwa kizimbani.
Dela alikuwa anadai ni mke halali wa Essien baada ya kufunga naye ndoa ya kimila miaka kadhaa
iliyopita na hivyo haruhusiwi kuoa mwanamke mwingine bila ya kumtaliki kwanza yeye.
“Mimi ni mke halali wa Michael Essien. Kama anawadanganya wanawake wengine, bora wafikirie kwa makini kwa sababu Essien ni mume wangu hadi mwisho,” alisema Dela.
Katika hatua nyingine, licha ya habari za mwigizaji filamu na mcheza soka huyo kutawala kwenye
vyombo vya habari, pia uraia wa Nadia umezua gumzo kubwa nchini humo, ambapo Waghana wengi wanahisi mlimbwende huyo si ‘mwenzao’.
Maswali kuhusu uraia wake yameibuka kutokana na kuwa chotara huku wananchi wengi wa taifa hilo ngozi zao zikiwa rangi nyeusi na hivyo kutambulika kwa urahisi pindi wanapojitambulisha utaifa wao.

Nadia ametumia nafasi hiyo kuweka mambo sawa kwa kueleza sababu ya kuzaliwa chotara wa
kizungu na maisha yake kwa ujumla.
"Mama na baba yangu wote ni Waghana na nimekulia Ghana maisha yangu yote. Mama yangu ngozi yake nyeupe, ambayo mimi ni kielelezo chake."

Akielezea kuhusu utamkaji wake maneno, anasema:
"Ukweli, maishani mwangu nimekulia Marekani na hiyo ndiyo sababu inayonifanya nizungumze kama Mmarekani. Naweza kuzungumza lugha yangu, lakini huu ndio uzungumzaji wangu halisi; Najieleza vyema ninapozungumza kama hivi.
"Nadia ametoka katika familia ya msanii. Huenda hata kipaji alichonacho amerithi kwa baba yake, Sidiku Buari, mwanamuziki maarufu na mwenye mafanikio nchini Ghana, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Kamati ya Wanamuziki wa Afrika. Pia anakaimu uenyekiti wa Chama cha Hakimiliki cha nchi hiyo (COSGA).
Mwigizaji huyo amejitetea kuwa ni raia kamili wa Ghana kwani amesomea nchini humo.Nadia
anasema: "Nilisoma na kuhitimu shahada yangu ya sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Ghana, Legon.Siku zote nilikuwa napenda kuigiza, nakumbuka nilianza shuleni. Nilikuwa nashiriki katika kikundi cha maigizo na kucheza.
"Ilimchukua miaka miwili kujizolea umaarufu katika medani ya filamu ndani na nje ya Ghana, ambapo filamu yake ya kwanza kuiachia sokoni ilikuwa ‘Beyonce’, ambayo aliigiza kwa umaridadi mkubwa.
Baadaye akachomoza katika filamu za ‘Darkness of Sorrows’, ‘Mummy's Daughter’(2),‘The
Return of Beyonce’, ‘In the Eyes of My Husband’, ‘American Boy’, ‘Dangerous Mission’, ‘Slave to Love’ na ‘Stone Face’.
‘A Woman's Honour’ ilimtambulisha rasmi katika soko la filamu nchini Nigeria, maarufu kamaNollywood, ambayo Nadia anaisifu kuwa ni kubwa kuliko ya Ghana.Anasema anapenda kufanya kazi ya filamu nyumbani kwao, lakini amelazimika kutumbukia Nigeria kwa sababu ina watu wengi wanaojihusisha na uigizaji na utengenezaji filamu na wateja ni wengi kupita Ghana, aliyodai watu wake wengi wamewekeza katika biashara ya viwanda zaidi.
Akijibu swali iwapo atapenda Ramsey Nouah awe mumewe halisi kama walivyoigiza katika filamu ya 'Stone Face', alicheka halafu akajibu: "Ukweli Ramsey ni miongoni mwa waigizaji wa kiume wa Nigeria wanaonivutia kufanya naye kazi, lakini hakuna kingine zaidi ya hapo."
"Kama nisingekuwa kwenye uhusiano na mtu yeyote, huenda ningefikiria hivyo, ningependa kuolewa naye, lakini simjui kwa undani. Nilipenda kumfahamu kwa kina, lakini wakati tayari nipo katika uhusiano, ndipo Ramsey ametokea.
"Nadia amesema anajisifia kutokana na kufanya vyema katika uigizaji na malengo yake ya baadaye ni kutengeneza filamu zake mwenyewe. Anavutiwa na mwigizaji wa Marekani, Julia Roberts.

No comments:

Post a Comment