Na Athanas Kazige
WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Haras El-Hodood ya Misri kinatarajiwa kuwasili nchini kesho, benchi la ufundi la klabu ya Simba limefanikiwa kunasa siri kadhaa za timu hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Simba, Kassim Dewji alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, El-Hodood inatarajiwa kuja nchini ikiwa na kikosi cha wachezaji 20 na viongozi watano.
Hata hivyo, Kassim hakueleza timu hiyo itakuja kwa ndege ipi na itafikia hoteli gani. Lakini kwa kawaida, timu za Misri huja nchini kwa ndege za Shirika la Ndege la Misri.
Simba na El-Hodood zinatarajiwa kumenyana Jumapili katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Cairo.
Wakati Wamisri wakitarajiwa kutua kesho, benchi la ufundi la Simba limesema, limeshanasa siri kadhaa za timu hiyo na limejiandaa kuwawezesha mabingwa hao wa soka Tanzania Bara kuibuka na ushindi mnono. Mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Simba, amelieleza Burudani jana kuwa, wamefanikiwa kupata siri hizo kutoka kwa ofisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania nchini Misri.
Kiongozi huyo alisema, mara baada ya kuzinasa siri hizo, walianza kuzifanyiakazi ili kuwawezesha wachezaji wa idara zote tatu kukabiliana vyema na wapinzani wao.
Imeelezwa kuwa, El-Hodood, inayotumia uwanja wa El-Max uliopo mjini Alexandria, imekuwa ikiwategemea zaidi wachezaji wake wane nyota kupata ushindi.
Wakali hao, ambao ni tegemeo kubwa la Kocha Tarek El-Ashry nipamoja na nahodha, Ahmed Eid Abdel Malek, ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Misri.
Wengine ni mshambuliaji Fofo Wisdom, anayetoka Ghana, kiungo Abdoulaye Sidibé anayetoka Mali na kiungo mwingine, Abdelrahman Mohie, rais wa Misri, ambaye ni mahiri kwa kufunga mabao ya mashuti ya mbali.
Kwa upande wa makipa, timu hiyo imewasajili Wael Khalifa, Mohamed Said na Mathurin Kameni kutoka Cameroon, ambao mmojawapo atakuwa na kazi kubwa ya kuzuia mashuti ya Mussa Hassan ‘Mgosi’, Mohamed Banka, Emmanuel Okwi na Uhuru Selemani.
Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema jana kuwa, wameshachukua tahadhari zote kabla ya kukabiliana na timu hiyo ya Misri, ambayo inashika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ya nchi hiyo.
Ndimbo alisema Simba inatarajiwa kuondoka Morogoro leo asubuhi kurudi Dar es Salaam, ambako itapanda boti kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa kukabiliana na wapinzani wao.
Simba ilifuzu kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuichapa Lengthens ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-1. Ilishinda mechi ya awali mjini Zimbabwe kwa mabao 3-0 kabla ya kushinda mechi ya marudiano mjini Dar es Salaam mabao 2-1.
Katika hatua nyingine, wagombea wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, Michael Wambura na Ismail Rage wamekatiwa rufani.
Wambura na Rage wamekuwa wagombea wengine wawili kukatiwa rufani baada ya kupitishwa na kamati ya usajili ya Simba. Mgombea mwingine ni Zacharia Hanspope.
No comments:
Post a Comment