KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

YANGA ILISAHAU BIASHARA ASUBUHI, JIONI MAHESABU

JERRY Tegete wa Yanga (kulia) akibadilishana jezi na Ulimboka Mwakingwe wa Simba
BEKI Shadrack Nsajigwa wa Yanga akiangushwa na beki mwenzake, Juma Jabu wa Simba katika mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Jumapili iliyopita.

MUSSA Hassan 'Mgosi' (kulia) wa Simba akichuana na Athumani Iddi 'Chuji' wa Yanga timu hizo zilipokutana katika mechi ya marudiano ya ligi kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba ilishinda mabao 4-3.

KABLA ya kuanza kwa michuano ya soka ya ligi kuu ya Vodacom msimu huu, mashabiki wengi wa klabu ya Yanga walikuwa na matumaini makubwa ya kuiona timu hiyo ikitwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.
Walikuwa na matumaini hayo kutokana na usajili mzuri na wa gharama kubwa uliofanywa na mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji kwa wachezaji 10 wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali.
Wachezaji hao, nchi wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Obren Curkovic (Serbia), Yaw Berko (Ghana), Robert Jama Mba (Cameroon), Wisdom Ndhlovu (Malawi), George Owino, Moses Odhiambo, Boniface Ambani, John Njoroge (Kenya) na Steven Bengo (Uganda).
Matumaini mengine kwa wana-Yanga yalitokana na ukweli kwamba, tmu hiyo ilikuwa ikiendelea kufundishwa na Kocha Dusan Kondic kutoka Serbia, aliyeiwezesha kutwaa ubingwa kwa misimu miwili mfululizo.
Hata hivyo, wakati Yanga ikijiandaa kwa ligi hiyo, kulizuka mvutano kati ya Kocha Kondic na uongozi kuhusu mahali, ambako timu hiyo ingeweka kambi.
Kondic alikuwa akitaka timu hiyo iende kuweka kambi nchini Afrika Kusini kama ilivyofanya msimu uliopita, lakini Mwenyekiti wa klabu hiyo, Iman Madega alitaka kambi iwe Mwanza.
Kwa bahati mbaya, Kondic na Madega walikwaa kisiki baada ya Manji kuamuru timu ikaweke kambi makao makuu ya klabu hiyo, yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Mbali ya kutaka timu ikaweke kambi Jangwani, Manji aliamua kumuhamisha Kondic kutoka kwenye hoteli ya New Africa, iliyopo katikati ya Jiji hadi Valley View iliyopo Jangwani, Dar es Salaam.
Kadhalika ulizuka mvutano miongoni mwa wachezaji kuhusu timu kuhamishia kambi Jangwani. Baadhi ya wachezaji walikubali kwenda kuishi klabuni, lakini wengine walipinga kwa madai kuwa, vyumba vyake ni vya hadhi ya chini.
Yanga ilianza ligi hiyo kwa kusuasua. Katika mechi yake ya kwanza, ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kuinyuka Manyema mabao 3-0 kwenye uwanja huo.
Hata hivyo, Yanga ilikwaa kisiki katika mechi yake ya tatu baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Majimaji mjini Songea, ikalazimishwa sare ya mabao 2-2 na JKT Ruvu kabla ya kuzinduka na kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1.
Yanga iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1, lakini ikalazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Azam, ikaichapa Moro United bao 1-0 kabla ya kucharazwa bao 1-0 na watani wao wa jadi Simba na kuhitimisha mzunguko wa kwanza kwa kuicharaza Prisons mabao 4-2.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, Yanga ilijikuta ikiwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi tano. Pia kocha wake, Kondic aliondolewa na nafasi yake ikachukuliwa na kocha wa sasa, Kostadin Papic.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kwani kiwango chake kisoka kiliongezeka na iliweza kushinda mechi nyingi za mzunguko wa pili, lakini ilishachelewa na kukosea mahesabu. Waswahili wanasema walikumbuka shuka, wakati kumekucha.
Ni katika mechi hizo za mzunguko wa pili, Papic aliweza kugundua kuwa, baadhi ya wanasoka wa kigeni waliosajiliwa na timu hiyo walikuwa bomu na hawakuwa na msaada wowote kwenye kikosi chake.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Jama Mba, ambaye alisajiliwa kwa fedha nyingi kuliko wachezaji wote, Kabongo, Owino, Bengo, Odhiambo na Njoroge. Tayari kocha huyo ameshasema kuwa, hatarajii kuwasajili wachezaji hao katika msimu ujao wa ligi.
Pamoja na wachezaji hao kuonekana kuwa mzigo kwa klabu, Yanga iliweza kuifunga African Lyon mabao 2-0, ikaicharaza Manyema mabao 3-1, iliichapa Majimaji mabao 3-0, iliibwaga JKT Ruvu kwa bao 1-0 kabla ya kuipiga Mtibwa Sugar mabao 3-1.
Katika mechi zingine za mzunguko wa pili, Yanga iliichapa Kagera Sugar mabao 2-1, iliitandika Toto African mabao 6-0, ikaichapa Azam mabao 2-1, iliibamiza Moro United 3-0 kabla ya kukubali kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa watani wao wa jadi Simba.
Kipigo kutoka kwa Simba kimeshaanza kuwagawa viongozi na wanachama wa klabu hiyo, huku kukiwepo na tuhuma kwamba abadhi ya wachezaji walicheza chini ya kiwango kwa lengo la kuihujumu timu.
Yanga ilitarajiwa kuhitimisha ligi hiyo jana kwa kumenyana na Prisons mjini Mbeya huku mshambuliaji wake, Mrisho Ngassa akiwa na matumaini ya kuwapiku Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba na John Boko wa Azam katika kuwania tuzo ya mfungaji bora.
Kabla ya mechi za jana, Mgosi alikuwa akiongoza kwa kufunga mabao 16, akifuatiwa na Boko na Ngassa waliofunga mabao 14 kila mmoja.




No comments:

Post a Comment