KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

NI LIGI ILIYOJAA WANASOKA WENGI WA KIGENI

JOSEPH Owino
HILLARY Echessa

EMMANUEL Okwi

MICHUANO ya soka ya ligi kuu ya Vodacom ilitarajiwa kufikia tamati jana kwa mechi sita zilizotarajiwa kuchezwa kwenye viwanja sita tofauti.
Katika mechi hizo, mabingwa Simba walitarajiwa kumenyana na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, washindi wa pili Yanga walitarajiwa kucheza na Prisons mjini Mbeya wakati African Lyon ilitarajiwa kucheza na JKT Ruvu mjini Dodoma.
Katika mechi zingine, Manyema ilitarajiwa kuvaana na Azam mjini Dar es Salaam, Majimaji ilitarajiwa kucheza na Moro United mjini Songea wakati Toto African ilitarajiwa kukipiga na Kagera Sugar mjini Mwanza.
Kabla ya mechi za jana, Moro United ndiyo timu pekee, iliyokuwa imeshapata tiketi ya kushuka daraja msimu huu na kusubiri kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao. Moro ilikuwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 21.
Timu zingine zilizokuwa hatarini kushuka daraja ni Prisons na Toto African, zilizokuwa na pointi 20 kila moja baada ya kucheza mechi 21 na Manyema iliyokuwa na pointi 22 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Katika ligi ya msimu huu, timu saba kati ya 12 ziliweka maskani yake mjini Dar es Salaam na kucheza mechi zake kwenye Uwanja wa Uhuru. Timu hizo ni mabingwa Simba, Yanga, Azam, African Lyon, Moro United, JKT Ruvu na Manyema.
Timu zilizoshiriki ligi hiyo kutoka mikoani ni Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Majimaji, Prisons na Toto African.
Timu za Simba, Yanga na Azam, ambazo zinafundishwa na makocha wa kigeni, ndizo pekee zilizofanya vizuri na kushika nafasi tatu za kwanza. Simba inanolewa na Patrick Phiri kutoka Zambia, Yanga inanolewa na Kostadin Papic kutoka Serbia wakati Azam inanolewa na Itamar Amorin kutoka Brazil.
Kadhalika, timu zilizokuwa na wachezaji wengi wa kigeni ndizo zilizofanya vizuri katika ligi hiyo msimu huu. Simba iliwatumia Emmanuel Okwi na Joseph Owino kutoka Uganda, Hillary Echessa, Mike Baraza na Jerry Santo kutoka Kenya.
Wachezaji wa kigeni walioichezea Yanga msimu huu ni makipa Obren Curkovic (Serbia), Yaw Berko (Ghana), Robert Jama Mba (Cameroon), Wisdom Ndhlovu (Malawi), George Owino, Boniface Ambani, John Njoroge, Moses Odhiambo (Kenya), Steven Bengo (Uganda) na Honore Kabongo (DRC).
Wageni wengine waliocheza ligi ya msimu huu ni Vladimir Niyonkuru (Burundi), Ben Karama, Danny Wagaruka na Ibrahim Shikanda kutoka Uganda, waliosajiliwa na Azam FC, Mike Katende na Robert Ssentongo kutoka Uganda waliosajiliwa na African Lyon.
Pamoja na kuwepo kwa wanasoka wengi wa kigeni, ni wachache walioweza kuziletea mafanikio timu zao. Hao ni Okwi, Echessa na Owino wa Simba, makipa Curkovic wa Yanga na Niyonkuru wa Azam.
Baadhi ya wachezaji kama vile Robert Mba, Owino, Bengo, Kabongo, Njoroge, Ambani na Ndhlovu, ambao walisajiliwa kwa fedha nyingi na Yanga, walionekana kuwa mzigo kwa klabu hiyo na tayari Kocha Papic ameshatamka wazi kuwa, atawaacha kwenye usajili wa msimu ujao.
Japokuwa ligi ya msimu huu ilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu nyingi kupania kutwaa ubingwa, zilijitokeza dosari kadhaa, ikiwa ni pamoja na uamuzi mbovu.
Katika baadhi ya mechi, waamuzi na wasaidizi wao walishindwa kutafsiri vyema sheria 17 za mchezo huo na wengine walichezesha kwa upendeleo, hatua iliyosababisha wafungiwe na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa ligi hiyo.
Baadhi ya timu zililazimika kutimua makocha wake kutokana na mwenendo mbovu katika ligi. Makocha walioonja adha hiyo ni pamoja na Abdalla Kibadeni wa Manyema, George Ssemogerere wa Kagera Sugar, Kenny Mwaisabula wa Majimaji, Dusan Kondic wa Yanga, Mbwana Makata wa Toto African, Fred Felix Minziro wa Moro United na Eduardo Almeider wa African Lyon.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya ligi hiyo, kanuni za mashindano za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilikuwa zikijikanganya na kusababisha kutofautiana kwa maamuzi kati ya kamati ya mashindano na kamati ya nidhamu.
Kila kamati ya mashindano ilipotoa adhabu kwa timu ama wachezaji walioonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu, kamati ya nidhamu ilitengua maamuzi hayo baada ya kupokea rufani na kuifanya kamati ya mashindano ionekane kama vile haitambui majukumu yake.
Msuguano kati ya kamati hizo mbili ulisababisha Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Nassib Ramadhani, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya mashindano, atoe malalamiko dhidi ya kamati ya nidhamuakidai kwamba maamuzi yake yamekuwa yakiidhalilisha kamati anayoiongoza.
Dosari nyingine iliyojitokeza katika ligi hiyo msimu huu ni kuuzwa kwa wachezaji katikati ya ligi. Hali hii ilisababisha timu nyingi kudhoofika kutokana na wachezaji wake nyota kuuzwa nje.
Kusimama kwa ligi kwa muda mrefu baada ya kumalizika kwa mechi za mzunguko wa kwanza na pia ligi kusimama ili kupisha mechi za timu ya taifa, Taifa Stars nako kulipunguza ushindani na msisimko wa ligi hiyo.
Mzunguko wa kwanza ulimalizika Novemba 15 mwaka jana wakati mzunguko wa pili ulianza Januari 16 mwaka huu. Hali hii ilisababisha baadhi ya wachezaji wajisahau kwamba wapo kwenye mashindano na ushindani kwa timu kupungua, tofauti na mzunguko wa kwanza.
Dosari nyingine iliyojitokeza katika ligi hiyo ni wizi wa mapato ya mechi za ligi. Kutokana na kukithiri kwa wizi huo, tayari baadhi ya watendaji wa TFF na viongozi wa klabu kubwa wameshakamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.

No comments:

Post a Comment