KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

Papic amwaga cheche Yanga


KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema ni vigumu kuwafundisha nidhamu wachezaji wa timu hiyo kwa sababu wameshakomaa.
Akizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Papic alisema wachezaji wakishakuwa na umri mkubwa, haiwezekani kuwafundisha nidhamu.
Papic alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Yanga kuchapwa mabao 4-3 na Simba katika mechi ya ligi kuu ya Vodacom, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Papic alisema nidhamu inaanza utotoni na kazi anayoifanya Yanga ni kufundisha kucheza soka kwa kutumia mbinu mbalimbali.
“Haiwezekani kufundisha nidhamu kwa watu wakubwa,” alisema kocha huyo baada ya kuulizwa ana maoni gani kuhusu vitendo vya wachezaji wake, baada ya Amir Maftah na Wisdom Ndhlovu kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi hiyo ya watani wa jadi nchini.
Papic alikataa kumtupia lawama mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akram kwa kutoa kadi hizo na kusisitiza kuwa, anachoangalia ni matokeo.
“Nakubali nimebugizwa mabao manne na huu ndiyo mchezo wa soka,” alisema.
Kocha huyo alitoa onyo kali kwa wachezaji wa timu hiyo wenye tabia ya utovu wa nidhamu na kusema hawezi kuwavumilia kwa vile wanachangia kushuka kwa maendeleo ya timu hiyo.
Papic alisema hakufurahishwa na vitendo vilivyoonyeshwa na wachezaji hao na wengine katika mechi hiyo, hivyo hawezi kuvifumbia macho.
Alisema angependa kuona kila mchezaji anaonyesha juhudi uwanjani, ikiwa ni pamoja na kuepuka makosa ya utovu wa nidhamu yasiyokuwa na maana.
Alisema kwa kipindi cha miezi mitano alichokuwepo Yanga, amegundua kuwa baadhi ya wachezaji wana kiburi na dharau kutokana na kujiona wao ni bora kuliko wenzao.
“Huu ndio msimamo wangu, siwezi kuendelea kuwa na wachezaji wa aina hii na wanaoshindwa kutimiza majukumu yao. Yanga ni timu ya ushindi, wachezaji wanapaswa kutambua hilo,”alisema.

No comments:

Post a Comment