KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

SIMBA YAFUNGA KAZI; Mgosi awazika Ngasa na Boko; Kaseja kuibuka kipa bora

Na Latifa Ganzel, Morogoro
MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba jana walimaliza michuano ya ligi kuu kwa kishindo baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Matokeo hayo yaliiwezesha Simba kuweka rekodi ya kumaliza ligi hiyo bila kupoteza mchezo, ikiwa imeshinda mechi 20 na kutoka sare mbili. Inazo pointi 61 baada ya kucheza mechi 22.
Mbali na rekodi hiyo, mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ ameibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu msimu huu baada ya kuifungia Simba mabao mawili kati ya manne.
Mgosi amemaliza ligi hiyo akiwa na mabao 18, akifuatiwa na Mrisho Ngasa wa Yanga na John Boko wa Azam waliofunga mabao 14 kila mmoja.
Kipa Juma Kaseja wa Simba huenda akaibuka kuwa kipa bora msimu huu baada ya kudaka mechi 21 kati ya 22 na kuruhusu timu yake kufungwa mabao 12.
Iliwachukua Simba dakika 15 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Mgosi kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka pembeni ya uwanja.
Mohamed Kijuso aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 34 baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mike Baraza aliyeambaa na mpira pembeni ya uwanja na kumimina krosi. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.
Bao la tatu la Simba lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ baada ya gonga safi kati yake, Mgosi na beki Salum Kanoni, aliyepanda na mpira mbele kutoka nyuma ya uwanja.
Simba ilihitimisha karamu ya magoli dakika ya 80 kwa bao lililofungwa na Mgosi baada ya kuunganisha wavuni krosi iliyopigwa na Jabir Azizi.
Mtibwa ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake, Geofrey Magori kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 89 kwa kosa la kumkwatua kwa nyuma Kelvin Yondani akiwa ndani ya eneo la hatari.

No comments:

Post a Comment