KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 19, 2010

MONALISA: Ndoto yangu ni kutengeneza filamu zangu



MWIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Yvonne Cherry amesema moja ya matarajio yake makubwa ya baadaye ni kutengeneza filamu zake mwenyewe.
Yvonne, maarufu kwa jina la Monalisa alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, anapenda
kutayarisha na kutengeneza filamu zake mwenyewe kwa lengo la kupiga hatua za juu zaidi katika fani hiyo.
Mwigizaji huyo, ambaye ni mama wa watoto wawili alisema, kwa sasa ana mkataba na Kampuni ya Escape, inayojihusisha na utengenezaji wa filamu na tamthilia, hivyo anashindwa kufanyakazi zake binafsi.
“Lakini mara mkataba wangu utakapomalizika, nimepanga kufanyakazi zangu binafsi
nilizokwishazianza. Siku zote ndoto zanguni kufanyakazi zangu mwenyewe,”alisema.
Monalisa alisema alishaanza kutengeneza filamu zinazojulikana kwa majina ya ‘Kaburi Moja’ na ‘Binti Mussa’, lakini alishindwa kuzimalizia kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine.
Alisema mbali na kutengeneza filamu zake mwenyewe, pia atakuwa akishiriki kucheza filamu za watu wengine kwa makubaliano maalumu.
Hata hivyo, Monalisa alikiri kuwa, kazi ya utengenezaji filamu kwa wanawake ni ngumu kwa sababu wamekuwa wakidharauliwa na wafadhili wa fani hiyo.
“Ukiwa mtayarishaji filamu mwanamke unadharauliwa sana. Wafadhili wengi wanapenda kuwathamini watayarishaji filamu wanaume,”alisema.
Mwigizaji huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, tangu alipoanza kujihusisha na fani hiyo miaka 12 iliyopita, hajawahi kukumbana na misukusuko mikubwa.
Alisema kutokumbana kwake na misukosuko huenda kulitokana na kuolewa kwake mapema na mmoja wa waongozaji filamu nyota nchini, George Tyson. Mumewe huyo ni raia wa Kenya.
Aliitaja filamu ya ‘Sabrina’ kuwa ndiyo pekee anayovutiwa nayo zaidi kati ya filamu alizozicheza na kwamba iliweza kumtambulisha na kumtangaza vyema katika soko la fani hiyo.
“Hii ni moja ya kazi nzuri zaidi nilizowahi kuzifanya. Lakini zipo filamu nyingine nilizozicheza vizuri kama vile ‘She is my Sister’ na ‘Binti Mussa’,” alisema.
Monalisa alianza kujihusisha na fani ya uigizaji tangu akiwa shule ya msingi, lakini alijitosa rasmi
kwenye fani hiyo wakati akiwa shule ya sekondari.
Alisema alivutiwa na fani hiyo kutokana na kuvutiwa na ushiriki wa mama yake, Natasha katika maigizo ya kwenye radio.
Ni wakati mama yake alipoitwa kwenye kikundi cha Mambo Hayo, kilichokuwa kikifanya maonyesho ya tamthilia kwenye kituo cha ITV, ndipo nyota ilipoanza kumuwakia.
“Wamiliki wa kikundi hicho walikuwa wanatafuta mwigizaji mwanamke na binti mwingine mdogo
mwenye kipaji. Niliitwa na kufanyiwa usaili, nikaonekana nafaa,”alisema.
Mara baada ya kujiunga na kikundi hicho, alikutana na waigizaji wengine nyota kama vile Richie,
Bishanga, Waridi na Aisha na tamthilia yake ya kwanza ilikuwa Nyota.
Hata hivyo, kundi hilo halikudumu kwa muda mrefu. Lilivunjika mwaka mmoja baadaye na kuzaliwa kwa makundi ya Nyota Ensemble na Nyota Academia.
Filamu ya kwanza ya Monalisa inajulikana kwa jina la ‘Girlfriende’, ambayo aliicheza akiwa muigizaji mkuu. Anakiri kuwa, filamu hiyo ndiyo iliyoleta mapinduzi makubwa katika fani hiyo nchini. Baadaye alicheza filamu za ‘Dilema’ na ‘Sabrina’, ambazo anakiri kwamba zilizidi kuwavutia vijana wengi kujitosa kwenye fani hiyo, ambayo baadhi yao imewaletea mafanikio makubwa kimaisha.
Monalisa anakiri kwamba fani ya filamu inalipa ikitumiwa vizuri na kwamba imemwezesha kuishi vyema, kupata vitu vizuri na kuwatunza watoto wake. Alisema anaichukulia fani hiyo kuwa ndiyo kazi yake inayomwendeshea maisha yake.
Anamshukuru mama yake mzazi, Natasha kuwa ndiye aliyechangia sehemu kubwa ya mafanikio yake kutokana na ushauri, ambao amekuwa akimpatia mara kwa mara.
“Kwa kweli nampenda sana mama yangu kiasi kwamba wakati mwingine huwa najisahau na
kumchukulia kama vile rafiki yangu,”alisema.
Vilevile anamshukuru mumewe, Tyson kwamba naye alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yake kutokana na kuwa muongozaji katika fani hiyo. Pia aliwashukuru wasanii wenzake kwa kumpa ushirikiano wa hali na mali.
Kwa sasa, Monalisa anaishi kwa kujitegemea baada ya kutengana na mumewe. Burudani zake kubwa ni kulala kwa muda mrefu, kutazama vipindi vya ndani na nje vya televisheni na kupika.

No comments:

Post a Comment