NAIROBI, Kenya
WAZIRI Mkuu wa Kenya Raila Odinga amesisitiza kuwa, alifanya kila aliloweza kuhakikisha mwanasoka wa kimataifa wan chi hiyo, McDonald Mariga anapata kibali cha kufanyakazi nchini Uingereza.
Katika juhudi zake hizo, Odinga alisema alimpigia simu Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown mara kadhaa ili kumshawishi mchezaji huyo apatiwe kibali hicho.
Mariga alikuwa akiwaniwa kwa udi na uvumba na klabu ya Manchester City, lakini ilishindwa kumsajili kutokana na kukosa kibali hicho.
Mchezaji huyo alikamilisha taratibu za kujiunga na Inter Milan ya Italia wiki iliyopita akitokea klabu ya Parma. Ametia saini mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka minne.
“Ningependa kuwahakikishia mashabiki wa soka na Wakenya wote kwamba, kwa kushirikiana na balozi wetu nchini Uingereza, nilifanya kila nililoweza kumwezesha Mariga kujiunga na Manchester City,”alisema Odinga.
“Nilitumia karibu saa tatu kuzungumza kwa simu na ofisi ya Gordon Brown, ofisi ya utamaduni na michezo, wizara ya mambo ya ndani, rais wa FA, Lord Treisman na Mariga mwenyewe,”aliongeza.
Odinga alisema Mariga (22) aliweza kupata kibali hicho, lakini tayari msimu wa usajili wa dirisha dogo ulikuwa umeshafungwa.
Hii inamaanisha kwamba, Mariga anaweza kujiunga na klabu yoyote ya ligi kuu ya England katika msimu ujao wa usajili, unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu.
Iwapo angesajiliwa na Manchester City, angekuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika
Mashariki kucheza soka ya kulipwa England.
No comments:
Post a Comment