LONDON, England
MSHAMBULIAJI Didier Drogba wa Chelsea amesema kumshinda Wayne Rooney wa Manchester United katika kinyang’anyiro cha ufungaji wa mabao hakutakuwa na maana kama watashindwa kutwaa taji la ligi kuu ya England.
Kauli hiyo ya Drogba imekuja siku chache baada ya kuifungia Chelsea bao la 30 msimu huu, kufuatia kufunga mabao mawili wiki iliyopita wakati Chelsea ilipoinyuka Portsmouth mabao 5-0 katika mechi ya ligi kuu ya England.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast anashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 24 katika ligi kuu ya England, akiwa nyuma ya kinara Rooney kwa tofauti ya mabao mawili.
Ushindi huo wa Chelsea pia uliiwezesha kuitimulia vumbi Manchester United katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa ligi hiyo. Timu mbili hizo zinatofautiana kwa pointi moja.
Manchester United inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 72 baada ya kucheza mechi 32, ikifuatiwa na Chelsea yenye pointi 71. Arsenal ni ya tatu kwa kuwa na pointi 68.
“Unajua nini, kama sintamaliza ligi nikiwa mfungaji bora, siwezi kujali kama tutakuwa tumetwaa
ubingwa,”alisema Drogba.
ubingwa,”alisema Drogba.
“Nilitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu mwaka 2007 na itakuwa furaha kubwa kwangi kama niitwaa tena, lakini kilicho bora hasa kwangu ni ubingwa wa ligi kuu,”aliongeza.
Drogba alisema ni jambo zuri kwa mchezaji kutwaa tuzo binafsi, lakini ni vizuri zaidi kutwaa tuzo ya pamoja na rafiki zake na wachezaji wenzako.
“Msimu huu umekuwa mrefu na mgumu. Utakuwa msimu mbovu kama nitaibuka mfungaji bora, lakini Chelsea haitatwaa ubingwa,”alisema.
Drogba, ambaye alitimiza umri wa miaka 32 mapema mwezi huu, hadi sasa ameifungia Chelsea mabao 124 katika misimu sita aliyokaa Stamford Bridge. Hakuna mchezaji mwingine wa kigeni katika historia ya Chelsea aliyeweza kufikisha rekodi hiyo.
Kwa sasa, Drogba amepania kufikisha mabao 33 kwa msimu ili kuiwezesha timu hiyo, inayofundishwa na Kocha Carlo Ancelotti iweze kutwaa taji hilo.
“Ukifikiria kwamba, siku hizi zipigi penalti, nilikosekana kwa mwezi mmoja wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na sikucheza katika mechi za mwanzo za ligi ya mabingwa wa Ulaya, kufunga mabao 30 kunamaanisha huu ni msimu mzuri kwangu,”alisema.
“Nilitaka kuwaonyesha watu kwamba bado nipo kwa sababu yalisemwa mambo mengi kuhusu mimi mwaka jana na watu hawakuweza kugundua kwamba nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya mguu,”aliongeza.
Drogba alisema alichanganyikiwa kutokana na kucheza idadi ndogo ya mechi msimu huu, lakini kwa sasa anamshukuru Mungu kwamba yupo fiti na anafurahia kurudi uwanjani.
Hata hivyo, Drogba alisema hafurahii kuona Chelsea imetolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, kufuatia kufungwa jumla ya mabao 3-2 na Inter Milan ya Italia.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alisema mabadiliko makubwa yanahitajika katika wiki chache zijazo kama klabu hiyo inataka kutwaa tena taji hilo baada ya kulikosa kwa miaka minne.
“Tumekuwa tukishutumiwa sana hivi karibuni na nafikiri kwamba ni sahihi kwa sababu hatujacheza kwa kiwango chetu cha kawaida katika wiki chache zilizopita,”alisema.
“Kila timu ilikuwa na wakati mgumu msimu huu, lakini kwetu umekuja kwa wakati mbaya.Kama ingetokea hivyo mapema msimu huu, ingekuwa rahisi kwetu kujirekebisha. Lakini sasa
tunapaswa kupambana na hakuna muda wa kufikiri,”alisema.
tunapaswa kupambana na hakuna muda wa kufikiri,”alisema.
“Tulikuwa na wakati mzuri kutokana na kuongoza ligi, lakini tumepoteza nafasi hiyo na sasa tunapaswa kuikimbiza Manchester United. Sasa tunapaswa kushinda michezo yetu yote kama tunataka kutwaa ubingwa,”aliongeza.
Hata hivyo, Drogba alisema binafsi anaamini Chelsea ina uwezo wa kutwaa taji la ligi hiyo msimu huu.Alisema Manchester United haikukata tama wakati walipokuwa nyuma ya Chelsea na kwamba hata baada ya kuifunga Arsenal mwezi uliopita, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Arsene Wenger alisema bado wanayo nafasi ya kutwaa ubingwa.
Drogba alisema kauli hiyo ya Wenger ilikuwa sahihi kwa sababu japokuwa walichanganyikiwa wakati Manchester United ilipotwaa uongozi, lakini wanapaswa kujirekebisha na kuanza kushinda tena.
“Ni muhimu sana kwamba tuliishinda Aston Villa wiki iliyopita. Ulikuwa ushindi muhimu kwetu.Wiki ijayo tutakuwa ugenini kucheza na Manchester United na tunahitajika kwenda Old Trafford tukiwa na nafasi ya kuwapiku kwenye uongozi iwapo tutashinda,”alisema.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa, tofauti ya pointi kati yetu haiwi kubwa wikiendi hii, hivyo tunapaswa kufanya kila linalowezekana kushinda,”aliongeza.
Drogba aliumia tena mguu mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokuwa akimtengenezea pasi Frank Lampard, aliyeifungia Chelsea bao la tano katika mechi dhidi ya Portsmouth, ukiwa ni ushindi wa pili mkubwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo alishindwa kuichezea Chelsea mwishoni mwa wiki iliyopita, ilipoibanjua Aston Villa mabao 7-1, lakini ana uhakika mkubwa wa kuichezea dhidi ya Manchester United.
“Mguu wangu kwa sasa una maumivu kwa sababu beki (wa Portsmouth) alinikwatua, lakini nafikiri utapona.
“Ni vigumu kuwa fiti na katika shepu ya kawaida wakati unapocheza mechi nyingi. Tumekuwa na wachezaji wengi majeruhi kwa sasa, hasa wa safu ya ulinzi. Lakini bado naamini tunaweza kuwa na msimu mzuri,”alisema.
No comments:
Post a Comment