KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

Humuod atupwa nje Stars

Na Deusdedit Undole
KIUNGO mahiri wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Abdulhalim Humuod ametemwa kwenye kikosi kilichotangazwa na kocha Marcio Maximo.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) uliopo Ilala, Dar es Salaam jana, Maximo alisema amemuacha mchezaji huyo kutokana na kutokuwepo kambini kwenye timu yake ya Mtibwa takriban siku 10.
"Kamwe huwezi kumuita mchezaji aliyekimbia kambi ya klabu yake kwa zaidi ya siku 10. Tumebakiwa na siku chache za kujiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya Rwanda," alisema Maximo.
Alisema licha ya uwezo na kipaji cha hali ya juu alichonacho mchezaji huyo, kiufundi hastahili kuwemo kwenye timu ya taifa kwa sababu wanahitajika wachezaji waliokaa kambini pamoja kwa muda mrefu katika klabu zao.
Maximo alisema kuwa amemrejesha mchezaji mwingine wa Mtibwa Sugar, Dickson Daud baada ya kubaini kiwango chake kimepanda.
"Timu ya taifa ina orodha ya wachezaji wengi na kila mmoja ana nafasi yake kulingana na uwezo anaokuwa nao wakati huo. Hivyo nimemrejesha Dickson Daudi kikosini, baada ya kuridhika na kiwango chake," alisema kocha huyo.
Maximo alisema kambi ya Stars itaanza kesho jioni jijini Dar es Salaam na amewataka wachezaji wote kuripoti isipokuwa wa timu ya Simba, ambao watajumuika na wenzao Jumapili.
Stars itaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya mzunguko wa pili wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) dhidi ya Rwanda.
Mechi hiyo itachezwa Mei Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni;
Makipa: Shabani Kado (Mtibwa Sugar) na Jackson Chove (Ruvu JKT).
Mabeki: Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub 'Cannavaro' (wote Yanga), Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani na David Naftali (wote Simba). Pia wamo Stephano Mwasika (Moro United), Aggrey Morris (Azam FC) na Dickson Daudi (Mtibwa Sugar).
Viungo: Erasto Nyoni, Ibrahim Mwaipopo, Seleman Kassim (wote Azam FC), Nurdin Bakari, Abdi Kassim 'Babi', Kigi Makasi (wote Yanga), Shaban Nditi (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz na Uhuru Seleman (Simba).
Washambuliaji: Mrisho Ngasa, Jerson Tegete (Yanga), John Bocco (Azam FC), Mussa Hassan 'Mgosi' (Simba), Michael Mgimwa (Moro United na U20), Yussuf Soka na Jonas Kajuna (African Lyon na U20).
000

No comments:

Post a Comment