KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 22, 2010

Maftah, Ndhlovu, Nurdin wakalia kuti kavu

WISDOM Ndhlovu
NURDIN Bakari

AMIR Maftah
Na Emmanuel Ndege
UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanza uchunguzi wa kina kujua chanzo kilichosababisha kikosi chao kupokea kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka ndani ya klabu hiyo, uchunguzi huo unafanywa na viongozi kwa kuwaita baadhi ya wachezaji na kuwahoji, ambapo wachezaji wanaohusishwa na sakata hilo ni Amir Maftah, Wisdom Ndhlovu, Boniface Ambani, Obren Cirkovic na Nurdin Bakari.
Kocha wa Yanga Kostadin Papic, Jumatatu ya wiki hii alitoa maelezo kwa uongozi juu ya kilichosababisha timu hiyo kubugizwa mabao hayo katika mchezo huo wa wapinzani wa jadi nchini, na inadaiwa kwenye ripoti hiyo ametaja baadhi ya wachezaji waliocheza chini ya kiwango.
Habari zinadai kuwa viongozi wanaoongoza mchakato huo ni Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako, Katibu wa Kamati ya Mashindano, Emmanuel Mpangala, ambao walikutana na Papic siku ya pili baada ya mechi hiyo na kumwangushia maswali, ili kujua sababu ya Yanga kupata kibano hicho.
Taarifa hizo zimedai viongozi hao baada ya kupata maelezo ya kina watawasilisha ripoti kamili kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, ambayo inatarajiwa kukutana leo au kesho mara wachezaji watakaporejea Dar es Salaam kutoka Mbeya.
Kikosi hicho juzi kilikwenda jijini Mbeya kuikabili Prisons jana katika mechi ya kufunga pazia la ligi kuu msimu huu.
Mwalusako alipoulizwa kwa njia ya simu juzi kuhusu uchunguzi huo, alikiri kuwepo suala hilo na kufafanua kuwa wanataka kujua kwa nini Maftah alimtandika kichwa Juma Nyoso wa Simba wakati alifahamu timu hiyo ilikuwa na pengo la Ndhlovu aliyetolewa kwa kadi nyekundu.
“Ni kweli tunataka kujua kwa nini Maftah na Ndhlovu walifanya vile, lakini tutakuwa makini kabla ya kutoa uamuzi,” alisema Mwalusako.

No comments:

Post a Comment