'
Friday, June 14, 2013
KAISHANGILIENI TAIFA STARS KESHO-KAVISHE
WADHAMINI wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager wamewaomba watanzania washikane na kuungana pamoja wakati wa mechi dhidi ya Ivory Coast kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwani kuna watanzania ambao tayari wamekata tamaa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema Taifa Stars inatakiwa kuungwa mkono na kushangiliwa kwa nguvu kwani wachezaji wameonesha kuwa wana uwezo.
“Hawa ni wanajeshi wetu…nawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi…tuwape sapoti na tuoneshe uzalendo kwani kwenye mpira lolote linawezekana,” alisema. Kavishe alisema watanzania lazima welewa timu hii bado ni changa na ina wachezaji wapya wenye umri mdogo ambao wameonesha uwezo mkubwa.
“Hata ikitokea tusifuzu kwenda Kombe la Dunia, vijana wameshaonesha dalili nzuri na tuna imani tutafanya vizuri katika mashindano mengine kama AFCON na CHAN,” alisema.
Aliwataka wachezaji kutulia uwanjani na kutobabaishwa na ukubwa wa timu ya Ivory Coast kwani wana uwezo wa kuwafunga na kushangaza dunia nzima Jumapili.
“Hii ni kama fainali kwa Ivory Coast na wao pia wamebabaika na kuitilia maanani kabisa mechi hii kwa sababu tukiwafunga ina maana hawatakuwa na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata,” alisema Kavishe.
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetimiza mwaka mmoja tangu ianze kuidhamini Taifa Stars na wadau mbalimbali wamesifia udhamini huu kwani umeleta mabadiliko makubwa katika timu ya Taifa.
Timu ya Ivory Coast iliwasili nchini Alhamisi usiku na imeweka kambi katika hoteli ya Bahari Beach, Kunduchi tayari kwa mechi itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa JUmapili hii saa tisa kamili.
Kwa mujibu wa TFF maandalizi yote yamekamilika na mechi hii inatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya watanzania watakaojitokeza uwanjani na kupitia runinga pia. Ivory Coast inaongoza katika kundi C ikiwa na pointi 10, Tanzania ya tatu na pointi 6, Morocco ya tatu na pointi 5 na Gambia ni ya nne na pointi 1.
Wakati timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao kesho.
Mkutano huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast inafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya Gymkhana.
Timu zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9 kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9 kamili alasiri.
Wakati huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana (Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na Uwanja wa Taifa.
Mauzo yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa sh. 50,000 katika ofisi za TFF.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment