KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 15, 2017

KAMATI YA SAA 72 YAIPA SIMBA USHINDI WA POINTI TATU DHIDI YA KAGERA SUGAR

HATIMAYE hayawi hayawi yamekuwa. Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, 'Kamati ya Saa 72', imefikia uamuzi wa kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar.

Simba iliikatia rufaa Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi huku akiwa na kadi tatu za njano, wakati timu hizo zilipomenyana katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa Aprili 2, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Kagera Sugar iliichapa Simba mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Ilidaiwa kuwa, Kagera Sugar ilikiuka kanuni za ligi kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba huku akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kamati yake ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.

Kutokana na kupewa pointi hizo, Simba sasa inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 kutokana na mechi 25 walizocheza hadi sasa.

No comments:

Post a Comment