KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, April 11, 2017

SARAH SOLO; MWANAMUZIKI NYOTA WA KIKE ANAYETIKISA DRC





WASWAHILI wana msemo unaosema, nyota njema huonekana asubuhi. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha kwa mwanamuziki mpya wa kundi la Wenge Musica Maison Mere, Lisungi Kabedi Sarah Urielle, maarufu kwa jina la Sarah Solo.

Mwanadada huyo ametokea kuwa maarufu baada ya kufuzu majaribio aliyofanyiwa na kundi la Wenge Musica Maison Mere na kutambulishwa mbele ya mashabiki, katika onyesho lililofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa Zamba Playa.

Ukumbi huo ulioko mjini Kinshasa, ndio unaotumiwa na kundi hilo kufanya mazoezi na pia ndio uliotumika kumtambulisha Sarah Solo, ambaye aliwahi kufanya shughuli za muziki nchini Ivory Coast, kwa miaka kadhaa, akiwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Katika onyesho hilo, Werrason alitumia dakika kama 10, kumtambulisha Sarah, akielezea uwezo na umahiri wake wa kupiga gita la solo na kuimba huku mashabiki wakimsikiliza kwa makini.

Baadaye Werrason alimpa nafasi mwanamama huyo ya kuwasalimia mashabiki. Akazungumza maneno machache kisha akalifuata gita la solo mahali lilipokuwa, akalivaa mwilini huku akilitazama kwa makini kama mtu anayeajabia kitu fulani.

Werrason akamtazama binti huyo kwa makini kisha akatabasamu na kutamka neno moja 'solo'. Sarah akaitikia kwa kupiga mdonoo mmoja wa gita. Werrason akaita tena kwa mara ya pili 'solo'. Sarah akajibu kwa kupiga mdonoo wa pili wa gita.

Ni kuanzia hapo mashabiki wakaanza kulipuka mayowe ya kumshangilia. Kuona hivyo, Werrason akawauliza wanataka mipigo gani ya solo kutoka kwa Sarah. Bila kumung'unya maneno wakamjibu kwa pamoja 'Sebene'.

Hapo ndipo Sarah alipoanza kuonyesha kuwa sio wa mchezo mchezo. Akaanza kufanya mavitu yake kwa kulipiga gita hilo kwa umahiri mkubwa na kuwafanya mashabiki wapagawe.

Katika onyesho hilo la utambulisho, mwanadada huyo alipiga gita hilo kwa
kunakili nyimbo zilizopigwa na wacharaza magita wa bendi hiyo, ambao aidha bado wanaitumikia ama walishaondoka, kama vile Flammi Kapaya, Kimbangu, Burkina Wasewa ‘Mbokalia’ na wengineo.

Ilikuwa raha iliyoje kumshuhudia mwanamama huyo akilidonoa gita hilo kwa staili za kuvutia huku baadhi ya mashabiki wakiufananisha umahiri wake huo na ule waliokuwa nao wakongwe Diblo Dibala, Dally Kimoko na Nene Tchakou.

Sarah, aliyekuwa amevalia blauzi iliyoungana na kaptula ya rangi ya kahawia, na ambaye hupenda kusuka nywele zake kwa staili ya mabutu, alikoleza starahamu ukumbini kwa kupiga gita hilo huku akiwa anayumba stejini, mithili ya mtu aliyetaka kuanguka.

Werrason akatoa ishara ya kusimamisha muziki kisha akaanza kuimba kibwagizo cha moja ya nyimbo zake maarufu. Baadaye akatoa ishara ya muziki kuendelea. Sarah akaendelea kufanya mavitu huku akitikisa kichwa chake na kurusha miguu yake huku na huko.

Baadhi ya mashabiki walishindwa kuvumilia, wakavamia stejini na kuanza kumtuza fedha lukuki huku wengine wakicheza kwa kufuatisha mapigo ya ala na kumshangilia kwa nguvu.

Wapiga picha nao wakawa wakipigana vikumbo stejini ili kupata picha nzuri za mwanamama huyo akiwa anacharaza gita la solo. Kwa hakika ilifurahisha kumkodolea macho.

Ili kudhihirisha kwamba Sarah hakuwa wa kawaida, Werrason akampa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuimba na kupiga gita. Naye hakufanya ajizi. Akawaongoza wanamuziki wenzake kupiga kibao cha Nakei Nairobi cha kundi la Afrisa International, kilichoimbwa na mkongwe Mbilia Bel.

Mshangao waliokuwa nao mashabiki kwa Sarah, pia ndio waliokuwa nao wanamuziki wa Wenge Musica Maison Mere. Baadhi ya wakati wanamuziki hao walijikuta wakimkodolea macho mwanadada huyo mithili ya watu waliokuwa wakistaajabu kumuomba kiumbe mpya aliyeteremshwa na Mola moja kwa moja kutoka mbinguni.

Sarah alizaliwa katika Jiji la Kinshasa na kuanza shughuli za muziki akiwa na umri wa miaka 12. Bendi yake ya kwanza ilikuwa Lavoniora Esthetique, iliyokuwa ikiongozwa na Dakumuda New Man.

Baada ya kudumu kwenye bendi hiyo kwa miaka saba, alijiunga na bendi ya Bana Ok inayoongozwa na mkongwe, Lutumba Simaro hadi mwaka 2012, alipoamua kuhamia nchini Ivory Coast kwa lengo la kusaka mafanikio zaidi.

Akiwa nchini humo, Sarah aliamua kuwa mwanamuziki wa kujitegemea, akirekodi na wanamuziki mbalimbali wa DRC waliokwenda huko kufanya maonyesho ya muziki.

Akimuelezea mwanadada huyo, Lutumba alisema ni mwenye uwezo wa kuelewa mafundisho kwa haraka na pia msikivu na mwenye adabu na tabia njema.

No comments:

Post a Comment