Ureno yailiza Cameroon
Eto’o alimwa kadi nyekundu
COVILHA, Ureno
URENO juzi iliichapa Cameroon mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa mjini hapa.
Timu zote mbili ziliitumia mechi hiyo kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Juni 11 mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Cameroon ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya nahodha wake, Samuel Eto’o kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza.
Eto’o alilimwa kadi hiyo dakika ya 34 kwa kosa la kumkwatua kwa nyuma beki wa kushoto wa Ureno, Duda. Awali, alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano.
Eto’o alijiunga na kikosi cha Cameroon wiki iliyopita baada ya kushinda taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya akiwa na Inter Milan ya Italia.
Mshambuliaji huyo alitishia kujitoa kwenye kikosi cha timu hiyo baada ya kushutumiwa na mwanasoka nyota wa zamani wa Cameroon, Roger Milla kwa kushindwa kujituma anapochezea timu ya taifa.
Kiungo Rail Meireles ndiye aliyeibeba Ureno baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Mchezaji huyo wa FC Porto alifunga mabao hayo dakika ya 32 na 47.
Achille Webo aliifungia Cameroon bao la kujifariji dakika ya 69 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi kutoka pembeni ya uwanja. Alifunga bao hilo dakika saba baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi.
Zikiwa zimesalia dakika tisa pambano hilo kumalizika, Ureno iliongeza bao la tatu kupitia kwa Nani. Alifunga bao hilo kwa mpira wa kubetua uliompita kipa Idriss Kameni wa Cameroon.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Ureno alishindwa kufunga bao licha ya kuingia na mpira mara mbili ndani ya eneo la hatari.
Ushindi huo ulikuwa mafanikio makubwa kwa Ureno baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Cape Verde wiki iliyopita. Ureno imepangwa kundi G pamoja na timu za Ivory Coast, Korea Kaskazini na Brazil.
Cameroon, ambayo wiki iliyopita ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Slovakia, imepangwa kundi E pamoja na timu za Japan, Denmark na Uholanzi.
Portugal: Eduardo; Paulo Ferreira (Miguel 45), Ricardo Carvalho, Bruno Alves (Rolando 63), Duda (Fabio Coentrao 63); Pedro Mendes (Ricardo Costa 73), Raul Meireles, Deco; Cristiano Ronaldo, Simao Sabrosa (Nani 45), Liedson (Danny 45).
Cameroon: Idriss Kameni; Georges Mandjeck, Nicolas Nkoulou, Stephane Mbia, Benoit Assou-Ekotto; Alexandre Song (Landry Nguemo 62), Jean Makoun, Eric Choupo-Moting (Mohamadou Idrissou 62), Achille Emana (Achille Webo 62), Eyong Enoh; Samuel Eto’o
Ghana hoi kwa Uholanzi
ROTTERDAM, Uholanzi
GHANA juzi ilipata kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Uholanzi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa mjini hapa.
Mechi hiyo ilikuwa ya kujipima nguvu kwa Ghana na Uholanzi, ambazo zinajiandaa kwa michuano ya fainali za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kuanza Juni 11 mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Mabao yote manne ya Uholanzi yalifungwa na wachezaji tofauti. Dirk Kuyt alifunga bao la kuongoza kipindi cha kwanza kabla ya Rafael van der Vaart, Wesley Sneijder na Robin van Persie kuongeza matatu dakika 20 za mwisho.
Bao alilofunga Van Persie lilimwezesha kuweka rekodi ya kuifungia Uholanzi mabao 17 katika mechi za kimataifa, sawa na wakongwe, Ruud Gullit na Johan Neeskens.
Bao pekee la Ghana lilifungwa na Asamoah Gyan dakika ya 78, kufuatia uzembe wa mabeki wa kati wa Uholanzi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, nahodha wa Uholanzi, Giovanni van Bronckhorst alisema walicheza vizuri na kustahili kushinda.
“Tulikuwa hatari kwa mashambulizi ya kushtukiza kipindi cha pili. Tuliumiliki mpira na kufunga mabao ya kuvutia,”alisema.
Katika mechi hiyo, Ghana iliyocheza bila ya kiungo wake, Michael Essien, ilifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Uholanzi, lakini mabeki wa timu pinzani wakiongozwa na Joris Mathijsen walikaa imara.
Kocha Bert van Marwijk wa Uholanzi aliwalaumu mabeki wake kwa kuruhusu Ghana ipate bao moja. Alisema bao hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wake.
Uholanzi inatarajiwa kucheza mechi nyingine keshokutwa kwa kumenyana na Hungary mjini Amsterdam kabla ya kwenda Afrika Kusini. Siku hiyo hiyo, Ghana itamenyana na Latvia mjini Milton Keynes.
Netherlands: Michel Vorm (Sander Boschker, 46), Gregory van der Wiel, John Heitinga, Joris Mathijsen, Giovanni van Bronckhorst, Mark van Bommel, Dirk Kuyt (Ryan Babel, 73), Nigel de Jong, Robin van Persie, Wesley Sneijder (Eljero Elia, 83), Ibrahim Afellay (Rafael van der Vaart, 63).
Ghana: Richard Kingson, John Pantsil, Hans Sarpei, Isaac Vorsah (John Mensah, 46) Lee Addy, Anthony Annan (Kwadwo Asamoah, 77), Derek Boateng, Quincy Owusu-Abeyie (Prince Tagoe, 46), Sulley Muntari (Andre Ayew, 46), Stephen Appiah (Dominic Adiyiah, 46), Matthew Amoah (Asamoah Gyan, 46).
Uswisi bado ‘mdebwedo’
SION, Uswisi
BAO lililofungwa na mshambuliaji Winston Parks juzi liliiwezesha Costa Rica kutoka kifua mbele baada ya kuichapa Uswisi bao 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa mjini hapa.
Parks alifunga bao hilo dakika ya 57 kwa shuti baada ya kuwatoka mabeki watatu wa Uswisi.
Mechi hiyo ilikuwa ya kujipima nguvu kwa Uswisi kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia Juni 11 mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Kipigo hicho kimeifanya Uswisi ipoteze mechi zote tatu ilizocheza kwa ajili ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa fainali hizo, huku ikiwa imefunga bao moja pekee kwa njia ya penalti.
Kocha Mkuu wa Uswisi, Ottmar Hitzfeld anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuiwezesha timu hiyo kuvuka hatua ya makundi kutokana na kuonyesha udhaifu mkubwa.
Uswisi inatarajiwa kuteremka tena dimbani keshokutwa kupambana na Italia mjini Geneva. Timu hiyo imepangwa kundi H pamoja na timu za Hispania, Chile na Honduras.
Katika mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa juzi, Australia iliichapa Denmark bao 1-0. Mechi hiyo ilichezwa mjini Johannesburg.
Bao pekee na la ushindi la Australia lilifungwa na mshambuliaji Josh Kennedy dakika ya 71.
Rossi, Borriello watemwa kikosi cha Italia
ROME, Italia
WASHAMBULIAJI Giuseppe Rossi na Marco Borriello wameachwa kwenye kikosi cha mwisho cha Italia, kinachotarajiwa kushiriki katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Akitangaza kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa timu hiyo juzi mjini hapa, Kocha Mkuu wa Italia, Marcello Lippi pia aliwatema kipa Salvatore Sirigu, beki Mattia Cassani na kiungo Andrea Cossu.
Kiungo Mauro Camoranesi ameendelea kuwemo kwenye kikosi hicho, licha ya kuumia mguu wakati wa mazoezi yaliyofanyika juzi.
Lippi hakutaka kufafanua sababu za kumbakisha kiungo huyo kwenye kikosi chake. Kocha huyo alitarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari jana.
Akizungumzia kutemwa kwake kwenye kikosi hicho, Rossi alisema hana wa kumlaumu. Alisema amekuwa akicheza kwa bidii na kuonyesha kila anachokiweza uwanjani, lakini hana bahati.
“Nahisi kocha alikuwa na mipango mingine. Naitakia kila la heri Italia,”alisema.
Rossi alizaliwa mjini New Jersey nchini Marekani na wazazi wawili kutoka Italia. Aliichezea Italia mwaka jana katika michuano ya Kombe la Mabara.
Kwa upande wake, Borriello aliifungia AC Milan mabao 14 msimu huu, na amekuwa akicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, ambayo Kocha Lippi anapendelea zaidi kuwatumia Alberto Gilardino, Vincenzo Iaquinta na Giampaolo Pazzini.
Katika kikosi hicho, wamo wachezaji tisa waliowezesha Italia kutwaa Kombe la Dunia miaka minne iliyopita nchini Ujerumani. Wachezaji hao ni Gianluigi Buffon, Fabio Cannavaro, Gianluca Zambrotta, Camoranesi, Daniele De Rossi, Gennaro Gattuso, Andrea Pirlo, Gilardino na Iaquinta.
Kikosi kamili cha Italia ni kama ifuatavyo: Makipa ni Gianluigi Buffon (Juventus), Morgan De Sanctis (Napoli), Federico Marchetti (Cagliari).
Mabeki: Salvatore Bocchetti (Genoa), Leonardo Bonucci (Bari), Fabio Cannavaro (Juventus), Giorgio Chiellini (Juventus), Domenico Criscito (Genoa), Christian Maggio (Napoli), Gianluca Zambrotta (AC Milan).
Viungo: Mauro Camoranesi (Juventus), Daniele De Rossi (AS Roma), Gennaro Gattuso (AC Milan), Claudio Marchisio (Juventus), Riccardo Montolivo (Fiorentina), Angelo Palombo (Sampdoria), Simone Pepe (Udinese), Andrea Pirlo (AC Milan).
Washambuliaji: Antonio Di Natale (Udinese), Alberto Gilardino (Fiorentina), Vincenzo Iaquinta (Juventus), Giampaolo Pazzini (Sampdoria), Fabio Quagliarella (Napoli).
Maradona bado hajapata kikosi cha kwanza
PRETORIA, Afrika Kusini
KOCHA Mkuu wa Argentina, Diego Maradona amesema bado hana hakika na kikosi chake cha kwanza kitakachocheza fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Kauli hiyo ya Maradona imekuja siku 11 kabla ya Argentina kushuka dimbani kucheza mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Nigeria.
Maradona aliitisha mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari juzi mjini hapa na kusema hatatangaza kikosi hicho hadi siku chache kabla ya kucheza na Nigeria.
Kocha huyo alisema kwa sasa bado anawatafutia nafasi kwenye kikosi hicho wachezaji wake wote nyota, wakiwemo Lionel Messi, Carlos Tevez, Gonzalo Higuain na Diego Milito.
“Itakuwa siku chache kabla ya mchezo wetu wa ufunguzi, nitaelewa nini la kufanya,”alisema Maradona. “Nina wachezaji 23 ambao wote uwezo wao ni mkubwa uwanjani.”
Maradona alisema kikosi chake cha sasa ni kizuri kuliko cha mwaka 1986, alichokiongoza kutwaa kombe hilo.
“Mwaka 1986 kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kikosi chetu’ Lakini wachezaji tulionao sasa wapo kwenye kiwango cha juu kuliko wa mwaka 86 na wanaelewa mambo vizuri kuliko sisi tulivyokuwa,”alisema.
Kocha huyo alisema pia kuwa, ushindani wa wachezaji wakati wa mazoezi ni mkubwa kwa vile kila mchezaji anafanya kila analoweza ili apewe nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Argentina imepangwa kundi B pamoja na timu za Nigeria, Ugiriki na Korea Kusini.
No comments:
Post a Comment