KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 3, 2010

CHOKORAA: Hakuna rapa anayeweza kunifikia


MWANAMUZIKI Khalid Chuma ‘Chokoraa’ wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International amejigamba kuwa, hakuna rapa anayeweza kushindanishwa naye kwa sasa hapa nchini.
Chokoraa alitoa majigambo hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi kipya cha Ben and Mai kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC1.
Alisema marapa wote alioshindanishwa nao katika tuzo za muziki za Kilimanjaro ni wazuri, lakini hakuna anaweza kumfikia iuwezo katika fani hiyo.
Chokoraa aliibuka kuwa rapa bora wa mwaka 2010 katika tuzo za muziki za Kilimanjaro baada ya kuwashinda Msafiri Diouf, Totoo ze Bingwa na Ferguson.
“Mimi nipo tofauti na marepa wengi hapa nchini kwa sababu nafanya muziki kuwa ni kazi, sio starehe kama wanavyouchukulia watu wengine,”alisema.
Mwanamuziki huyo wa zamani wa bendi ya Extra Bongo alisema, repa pekee anayemzimia ni Papii Nguza, ambaye alimwelezea kuwa ndiye anayepaswa kushindanishwa naye.
Kwa sasa, Nguza anatumikia kifungo cha maisha jela pamoja na baba yake, Nguza Vicking. Ndugu zake wawili, Nguza Mbangu na Francis Nguza waliachiwa huru hivi karibuni.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuwepo kwa uchawi katika muziki, Chokoraa alikiri kuwa ni kweli zipo, lakini alisisitiza kuwa, mafanikio katika fani hiyo yanapatikana kutokana na juhudi binafsi za mwanamuziki.
“Uchawi kwenye muziki upo, na si kwenye muziki tu, upo katika vitu vingi, lakini kikubwa ni kufanyakazi kwa umakini na kuwa na ubunifu,”alisema.
“Lakini tukumbuke kuwa, muziki ni kama mashetani ndio maana wakati mwingine utaona mtu anacheza muziki hadi anavua nguo na kubaki mtupu,”aliongeza.
Kabla ya kujiunga na fani ya muziki, Chokoraa alipitia kazi nyingi, ikiwemo kupiga debe, ufundi rangi, umeme, useremala na kuendesha daladala.
“Hili jina la Chokoraa limetokana na maisha duni niliyokuwa naishi zamani. Sikuwa tofauti na watoto wa mitaani,”alisema.
Akijibu swali iwapo wimbo wa ‘Kuachwa’ alioutunga na kuurekodi kwa kushirikiana na Jose Mara, Kalala Junior na Chalz Baba ni tukio lililomkuta, mwanamuziki huyo alisema si kweli.
“Huu wimbo niliutunga kutokana na mambo ya kidunia, jinsi gani tunaishi, sijamwimbia mtu yeyote. Kwa Chokoraa kuachwa ni vigumu sana,”alisema.
Rapa huyo alisema kundi lao la Mapacha Wanne bado lipo na linajiandaa kupakua albamu yao ya kwanza mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
Alijigamba kuwa, uzinduzi wa albamu hiyo utakuwa babu kubwa na haujawahi kutokea kwa bendi yoyote hapa nchini kwa vile wamejiandaa kufanya mambo mazito.
“Sisi ni vijana wa mjini, tunajua tuingie wapi na tutoke wapi na damu zetu bado zinachemka, hivyo tumepania kufanya maajabu,”alisema.
Chokoraa alisema hapati matatizo kuitumikia bendi yake ya Twanga Pepeta na kundi la Mapacha Wanne kwa wakati mmoja kwa sababu amejigawa vyema bila kuathiri kazi zake.
Hata hivyo, Chokoraa hakuwa tayari kuzungumzia vurugu zilizotokea katika onyesho la kwanza la kundi hilo baada ya mwanamuziki Chalz Baba kukamatwa na polisi.
Ilidaiwa kuwa, Chalz alikamatwa kutokana na agizo la mmiliki wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka kwa vile yeye, Chokoraa na Kalala hawakupata baraka za uongozi.
Chokoraa alikiri kuwa, hadi sasa bado hajafunga ndoa, lakini anao watoto watatu aliozaa kwa wanawake tofauti. Aliwataja watoto hao kuwa ni Issack, Abdul na Chuma. Alisema hana mpango wa kuzaa mtoto mwingine kwa vile ameamua kufunga uzazi.
Ametoa mwito kwa wanamuziki nchini kuacha kubweteka kutokana na mafanikio machache wanayoyapata, badala yake waongeze bidii kwa kubuni vitu vipya mara kwa mara.
Alisema wanamuziki wengi wanashindwa kupata mafanikio kutokana na kuichukulia fani hiyo kama sehemu ya kuuza sura na kujipatia umaarufu.
Amewashukuru mashabiki wa muziki nchini kwa kuwaunga mkono wanamuziki kutokana na kununua kazi zao kwa wingi, hali inayowapa moyo wa kufanyakazi kwa bidii zaidi.

No comments:

Post a Comment