'
Wednesday, June 2, 2010
RONALDO: Macho yote kwangu Kombe la Dunia
LISBON, Ureno
MSHAMBULIAJI nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo amekiri kuwa, anakabiliwa na shinikizo kubwa la kuiongoza nchi hiyo kufanya vizuri katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Ronaldo (25) alisema juzi mjini hapa kuwa, shinikizo hilo limesababisha kushuka kwa ari yake ya kufanya vizuri katika fainali hizo, zinazotarajiwa kuanza Juni 11 mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Manchester United ya England, amejikuta akiandamwa mara kwa mara na vyombo vya habari tangu alipojiunga na Real Madrid ya Hispania msimu huu.
Amesema akiwa nahodha wa Ureno, anatambua wazi kuwa, macho ya mashabiki wa soka duniani yatakuwa kwake, wakimtarajia afanye maajabu.
Mwanasoka huyo bora wa zamani wa dunia alisema: “Kuvaa nembo ya unahodha ni heshima na kunanifanya nione fahari. Sijali kama kutakuwepo na shinikizo kwangu, lakini baadhi ya wakati kunajitokeza matarajio ya ajabu na siku zote huniangukia mimi.”
Hata hivyo, Ronaldo alisema ameizoea hali hiyo kwa vile imekuwa ikimtokea mara kwa mara na hafikirii iwapo itamuathiri kiuchezaji. Ronaldo alisema amekuwa akikumbwa na shinikizo hilo anapokuwa zaidi kwenye timu ya taifa ya Ureno kuliko akiwa kwenye klabu yake ya Real Madrid.
“Lakini siku zote najaribu kufanya kile ninachoweza kadri ya uwezo wangu na kulipeleka mbali jina la Ureno,”alisema.
Ronaldo alisema hakuna mtu anayeweza kushinda chochote peke yake na timu haiwezi kuwa na mchezaji mmoja. Alisema pia kuwa, timu haiwezi kufanikiwa ikiwa na wachezaji watatu au wanne wazuri pekee, lazima wawepo sita au saba.
Mshambuliaji huyo alisema atafanya vitu vyake kadri awezavyo, hata kama vitasabisha matatizo. Alisema shinikizo la maisha yake binafsi haliwezi kumwathiri.
“Mimi ni mburudishaji, hiyo ni kazi yangu. Yeyote anayependa soka, ananipenda mimi,”alisema.
“Sielewi kwa nini wananizomea. Inawezekana ni kwa sababu wananiona ni mpinzani hatari. Nina uzoefu na naelewa kipi siwezi kukifanya,”aliongeza.
Ronaldo alisema hawezi kuwajibu watu wanaomzomea kwa kufanya vitu vibaya, japokuwa wakati mwingine hujikuta akiwa kwenye wakati mgumu wa kudhibiti hasira zake.
Alisema tabia ya baadhi ya mashabiki kumzomea awapo uwanjani, humwongezea nguvu na kwamba chochote watakachokifanya, anapaswa kuisaidia timu yake.
“Siwezi kujibadili nilivyo na namna ninavyocheza,”alisisitiza.
Ronaldo alisema kila kinachomuhusu Ronaldo, huzua tetesi nyingi na kuongeza kuwa, kila anachokifanya, huvutia vyombo vingi vya habari na jamii.
“Nimezoea kufanywa habari, lakini nyingi huwa si za kweli. Sifikirii iwapo watu wanamfahamu Ronaldo halisi. Najifahamu mimi ni nani na sijali baadhi ya watu wanavyofikiria kuhusu mimi,”alisema.
Ureno, ambayo inashika nafasi ya tatu kwa ubora wa viwango vya soka duniani, ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa njia ya mechi za mtoano wakati Ronaldo alishindwa kufunga bao katika mechi za awali.
Mshambuliaji huyo, ambaye ameshinda mataji mbalimbali katika ngazi ya klabu, amesema mwelekeo wake kwa sasa ni kunyakua tuzo ya kimataifa.
“Licha ya kushinda tuzo nyingi katika ngazi ya klabu, bado nina ndoto ya kushinda tuzo nyingine nikiwa na timu yangu ya taifa. Nina ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia,”alisema.
“Nataka kuwa bora. Nataka kushinda tuzo nyingi na vikombe vingi. Mimi si mchezaji niliyekamilika na naelewa kwamba sifahamu kila kitu,”aliongeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment