'
Thursday, June 10, 2010
PATRICK MTILIGA, Mtanzania atakayecheza fainali za Kombe la Dunia
SOKA ya Tanzania inatarajiwa kuingia kwenye historia mpya, kutokana na kuwa na mwakilishi katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kuanza kesho nchini Afrika Kusini.
Katika fainali hizo, mchezaji Patrick Mtiliga, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Malaga ya Hispania, anatarajiwa kuwa Mtanzania wa kwanza kupeperusha bendera ya Tanzania.
Hata hivyo, Mtiliga atacheza fainali hizo akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya Denmark, ambako ndiko alikozaliwa. Baba wa mchezaji huyo ni mtanzania wakati mama yake ni raia wa Denmark.
Mtiliga alizaliwa Januari 28, 1981 katika mji wa Copenhagen. Ni mchezaji anayecheza nafasi ya beki wa kushoto. Ameichezea timu ya taifa ya Denmark katika mechi tatu za kimataifa.
Alianza kucheza soka katika timu ya vijana ya Boldklubben ya Copenhagen mwaka 1993. Alikuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Alianza kuichezea timu ya wakubwa ya klabu hiyo mwaka 1998 hadi 1999. Baada ya kuichezea klabu hiyo mechi 13 za ligi, aliihama na kujiunga na Feyenoord Rotterdam ya Uholanzi.
Klabu ya Feyenoord ilimuuza Mtiliga kwa mkopo kwa klabu ya vijana ya Excelsior Rotterdam kwa kipindi, ambacho hakikuweza kufahamika. Alianza kuichezea timu ya wakubwa katika mwaka wake wa kwanza ndani ya klabu hiyo.
Aliichezea timu hiyo kwa misimu miwili na nusu, akiwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha kupanda daraja msimu wa 2001-02. Timu hiyo ilishuka daraja msimu uliofuata.
Msimu wa 2003-04, Mtiliga alijihakikishia namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kuichezea mechi 23 kabla ya kurejeshwa kwenye klabu ya Feyenoord.
Januari 2005, Mtiliga alikumbwa na balaa baada ya kuumia msuli wa paja, baada ya kuichezea Feyenoord mechi 11 za ligi. Baada ya kupona Januari 2006, Feyenoord iliamua kumuuza tena kwa mkopo, lakini Mtiliga aligoma na kuamua kusugua benchi hadi mkataba wake ulipomalizika.
Agosti 2006, Mtiliga alijiunga na klabu ya NAC Breda kwa mkataba wa mwaka mmoja, ukiwa na kipengele kinachoruhusu kuongezwa iwapo atafanya vizuri.
Baada ya kuonyesha kiwango cha juu, ilipofika Januari 2007, aliamua kuongeza mkataba wake na kuwa wa miaka miwili na nusu. Aliichezea timu hiyo katika mechi 34 na kumaliza msimu wa 2007-08 ikiwa ya tatu kwenye ligi.
Mkataba wake ulipomalizika mwaka 2009, Mtiliga alianza kuwaniwa na klabu mbalimbali za Ulaya kabla ya kuamua kujifunga kitanzi katika klabu ya Malaga ya Hispania
Mtanzania huyo mwenye uraia wa Denmark alikumbwa na balaa la kuumia katika mechi yake ya kwanza akiwa na Malaga na kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Baada ya kupona, Kocha Juan Ramon Lopez wa Malaga alimshauri abadili namba na kucheza nafasi ya ushambuliaji na muda si mrefu uliofuata, akaanza kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza.
Januari 24 mwaka huu, Mtiliga alikumbwa na balaa lingine la kuumia baada ya kuvunjika pua, kufuatia kupigwa kwa kiwiko cha mkono na mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Real Madrid. Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa hilo na Mtiliga alikaa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Mtiliga alianza kucheza soka ya kimataifa mwaka 1997 katika timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Denmark. Amecheza mechi 28 katika timu tofauti za vijana za nchi hiyo na kufunga mabao manne.
Wakati akiwa klabu ya Feyenoord, Kocha Ruud Gullit alimwelezea mchezaji huyo kwamba, atakuwa tegemeo kubwa la Denmark katika miaka ijayo.
Alianza kuichezea timu ya wakubwa ya Denmark, Novemba 2008 baada ya kuitwa na kocha Morten Olsen. Aliichezea kwa mara ya kwanza ilipocheza na Wales kabla ya kutemwa.
Aliitwa tena kwenye kikosi hicho Mei mwaka huu kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment