KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 3, 2010

Manji anunua tiketi zingine

MFADHILI Mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji ameamua kununua tiketi zingine alfu moja kwa ajili ya wanachama wa klabu hiyo watakaoshuhudia mechi kati ya Tanzania na Brazil.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Manji ametumia sh. milioni 30 kwa ajili ya kununua tiketi hizo na fedha hizo zimeshalipwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Uamuzi wa Manji kununua tiketi hizo umekuja siku moja baada ya kutoa sh. milioni 90 kwa ajili ya kununua tiketi alfu tatu za sh. 30,000.
Kufuatia kuongeza tiketi hizo, Manji sasa atakuwa ametumia sh. milioni 120 kwa ajili ya kuwanunulia wanachama wa Yanga tiketi za kushuhudia mechi hiyo.
Manji amepanga kuwatia tiketi hizo wanachama wa Yanga wakati wa mkutano wa kujadili marekebisho ya katiba unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Kufuatia ahadi hiyo ya Manji, wanachama wengi wa Yanga wamejitokeza kwa wingi makao makuu ya klabu hiyo kulipia ada za uanachama.
Mbali na kulipia ada za uanachama, mashabiki wengi wa klabu hiyo wamejitokeza kuomba uanachama wa klabu hiyo, lakini idadi yao haikuweza kufahamika mara moja.
Pambano kati ya Tanzania na Brazil limepangwa kufanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wenye uwezo wa kuchukua watazamani zaidi ya 60,000 kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment