KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 3, 2010

Dunga atangaza kikosi kitakachoivaa Tanzania

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
KOCHA Mkuu wa Brazil, Carlos Dunga ametangaza rasmi kikosi cha timu yake kitakachocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Tanzania.
Dunga alitangaza kikosi hicho cha wachezaji 23 juzi, ikiwa ni siku ya mwisho kwa timu zote 32 zitakazoshiriki fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia kuwasilisha majina hayo kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Brazil inatarajiwa kumenyana na Tanzania katika mechi itakayopigwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Kabla ya mechi hiyo, Brazil ilitarajiwa kucheza mechi nyingi jana dhidi ya Zimbabwe mjini Harare.
Wachezaji waliotangazwa na Dunga ni wale wale waliokwenda na timu hiyo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo.
Kocha huyo ameendelea na msimamo wake wa kuwaacha wachezaji saba nyota kwa sababu mbalimbali, akiwemo mshambuliaji Ronaldinho Gaucho. Wengine walioachwa ni Paulo Henrique Ganso, Sandro, Diego Tardelli, Alex, Carlos Eduardo na Marcelo.
Dunga amekifanyia marekebisho makubwa kikosi hicho tangu alipokabidhiwa jukumu la kukinoa baada ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006, akiwaacha Ronaldinho, Ronaldo na Adriano.
Badala yake, kocha huyo amekuwa akiwatumia zaidi wachezaji wasiokuwa na majina, ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika michuano waliyoshiriki, ikiwemo Kombe la Mabara.
“Lengo letu lilikuwa kupata wachezaji wanaohitaji hasa kuwemo kwenye timu ya taifa,”alisema. “Wachezaji wengi hawakutaka kuwepo hapa, sasa ni tofauti.”
Kocha huyo aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa, wachezaji wake wataruhusiwa kufanya mapenzi wakati wa siku za mapumziko.
“Si kila mtu anapenda kufanya mapenzi, kunywa mvino au ice cream,”alisema. “Lakini siku zao za mapumziko, kila mmoja ataruhusiwa kufanya anachokitaka.”
Kikosi kamili cha Brazil ni kama ifuatavyo:
Makipa: Julio Cesar (Inter Milan), Heurelho Gomes (Tottenham), Doni (AS Roma).
Mabeki: Maicon (Inter Milan), Daniel Alves (Barcelona), Michel Bastos (Lyon), Gilberto (Cruzeiro), Lucio (Inter Milan), Juan (AS Roma), Luisao (Benfica), Thiago Silva (AC Milan).
Viungo: Elano (Galatasaray), Kaka (Real Madrid), Gilberto Silva (Panathinaikos), Josue (Wolfsburg), Ramires (Benfica), Felipe Melo (Juventus), Kleberson (Flamengo), Julio Baptista (AS Roma).
Washambuliaji: Luis Fabiano (Sevilla), Nilmar (Villarreal), Robinho (Santos), Grafite (Wolfsburg).
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemwomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania na Brazil.
Habari kutoka ndani ya shirikisho hilo zilieleza jana kuwa, tayari maombi hayo yameshawasilishwa Ikulu na kinachosubiriwa ni majibu.

No comments:

Post a Comment