KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 6, 2010

Yanga sasa vurugu tupu

WAKATI mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Yanga wa kujadili marekebisho ya katiba unafanyika leo, hali ndani ya klabu hiyo si shwari.
Hilo lilidhihirika jana baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Iman Madega na mfadhili mkuu, Yusuf Manji kutoa taarifa zinazopingana kuhusu mkutano huo na mustakabali wa Yanga.
Mkutano huo umepangwa kufanyika leo kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi uliopo Oysterbay mjini Dar es Salaam.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa wanachama wa Yanga kuhusu mkutano huo, Manji ameutaka uongozi uliopo madarakani kukabidhi madaraka yake kwa Baraza la Wadhamini mara baada ya kufanyika kwa marekebisho hayo.
Mfadhili huyo alisema kamati ya utendaji ya Yanga, iliyo chini ya uenyekiti wa Madega, haina uhalali wa kusimamia mkutano huo kwa vile ilishamaliza muda wake tangu Mei 30 mwaka huu na hakuna ridhaa ya wanachama inayoiruhusu kuendelea kuwepo madarakani.
Manji alisema ni vyema kamati hiyo ijiuzulu na kukabidhi madaraka yake kwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo linalopaswa kuitisha na kusimamia uchaguzi mkuu wa klabu hiyo. Baraza hilo linaundwa na Mama Fatuma Karume na Manji.
“Kwa mujibu wa katiba iliyorekebishwa mwaka 2008, muundo mpya wa uongozi kwa maana ya kamati ya utendaji na sekretarieti wenye kipindi cha miaka minne, utaanza mara tu baada ya uongozi uliopo, ambao uliingia madarakani kwa katiba ya mwaka 2007 kumaliza kipindi chake. Kipindi cha kamati ya Madega na miaka mitatu na si minne,” amesema.
Manji ameutaka uongozi wa Madega kutangaza tarehe ya uchaguzi kabla ya kuingia kwenye mkutano wa leo na ameshauri uchaguzi huo ufanyike Juni 27 mwaka huu.
Mfadhili huyo pia amewataka wanachama wa Yanga kuvifanyia marekebisho vipengele vyote vya katiba vinavyoonekana kuwa na utata badala ya vile vilivyoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Manji alisema amebaini kuwepo kwa mbinu za kijanja za kupenyeza marekebisho ya katiba yenye mwelekeo wa kuwanufaisha watu wachache ndani ya Yanga, jambo ambalo alidai kuwa ni la hatari.
Alivitaja baadhi ya vipengele alivyodai kuwa, vimefanyiwa marekebisho kinyemela kuwa ni pamoja na ibara ya 22 (2), ili idadi ya wanachama inayohitajika kuitisha mkutano wa dharula iongezeke kutoka nusu hadi theluthi mbili.
Alikitaja kipengele kingine, alichodai kimenyofolewa kwa makusudi kuwa ni ibara ya 29 (4), ambacho madhara yake ni kuruhusu uongozi uliomaliza muda wake uendelee kuwa madarakani kwa mwaka mmoja zaidi hadi 2011.
Vipengele vingine, ambavyo Manji amedai vilifanyiwa marekebisho kinyemela ni ibara ya 57 (5) inayohusu majukumu ya kampuni ya umma na ibara ya 62 (h), inayohusu wajibu wa Baraza la Wadhamini.
“Narudia kushauri kwamba,marekebisho yale tu, ambayo ni lazima kwa mujibu wa maelekezo ya TFF ndio yafanyike Jumapili na mengine yasubiri mpaka Yanga itakapofanya uchaguzi na viongozi wapya kuingia madarakani,” ameeleza.
Manji pia ameutaka uongozi wa Madega kuiachia Kamati ya Uchaguzi chini ya Jaji Mkwawa, jukumu la kusimamia uchaguzi mkuu bila kuiingilia ili iweze kufanyakazi yake kwa uhuru na haki.
Hata hivyo, uchunguzi wa MZALENDO umebaini kuwa, marekebisho ya vipengele hivyo yalitolewa na TFF katika barua yake ya Desemba 18, 2009 iliyotumwa kwa uongozi wa Yanga.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba TFF/TECH/LEP 09/045, shirikisho hilo liliutaka uongozi wa Yanga kuvifanyia marekebisho vifungu 24 vya katiba yake vilivyobainika kuwa na mapungufu.
Barua hiyo pia iliutaka uongozi wa Yanga kuweka kwenye katiba yake muda wa uongozi wa kipindi cha miaka minne, sifa za wagombea na viongozi watatu wa kuajiriwa.
Akizungumzia taarifa hiyo ya Manji kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Madega alimshutumu mfadhili huyo na kumwelezea kuwa ni mchochezi, anayetaka kuleta vurugu ndani ya Yanga.
Madega alisema amegundua Manji amekuwa akichochea kuwepo kwa hali ya vurugu ndani ya klabu hiyo, kutokana na kutoa taarifa katika vyombo vya habari Juni 4, mwaka huu.
Ameonya kuwa, endapo zitatokea vurugu wakati wa mkutano huo, Manji anapaswa kuwa muhusika mkuu na kusisitiza kuwa, si kweli kwamba uongozi wake unang’ang’ania kuwepo madarakani kwa vile walishapendekeza uchaguzi mkuu ufanyike Januari 3 mwaka huu kabla ya kusimamishwa na TFF.
Mwenyekiti huyo amewaomba wanachama wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili wapate nafasi ya kuijadili na kuipitisha katiba mpya ya klabu hiyo kabla haijasajiliwa na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini.
Alipoulizwa sababu za kutokuelewana kwake na Manji, Mwenyekiti huyo alisema, ni kutokana na mfadhili huyo kuweka mbele zaidi maslahi yake binafsi kuliko ya klabu.
Akito mfano, alisema haoni kwa nini mfadhili huyo anashinikiza kamati ya utendaji ya Yanga iwe na wajumbe sana na ipewe madaraka ya kumchagua mwenyekiti wa klabu badala ya jukumu hilo kufanywa na mkutano mkuu.
Madega alisema pia kuwa, Manji anataka kipengele kinachohusu utaratibu wa kumchagua mwenyekiti na makamu wake kifutwe kwenye katiba, jambo ambalo alisema haliwezekani kutokana na mfumo wa TFF na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
“Nina imani wanachama wa Yanga watakuwa watulivu wakati wa mkutano huo na sisi kama viongozi, tumechukua hatua zote kuhakikisha usalama unakuwepo,”alisema.
Wakati huo huo, Manji amesema ametoa pesa kwa ajili ya kuwalipia ada ya uanachama wanachama wote 7,155 wa Yanga kwa kipindi cha miaka miwili.
Manji alisema jana kuwa, wanachama hao ni wale waliokuwa hai kuanzia Juni Mosi mwaka huu, siku ambayo alitangaza kuwalipia tiketi wanachama wa Yanga kwa ajili ya kushuhudia pambano la kirafiki la kimataifa kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Brazil, litakalochezwa kesho.

No comments:

Post a Comment